1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kashfa ya Marekani kutega mawasiliano kuathiri uchumi

3 Julai 2013

Imani kati ya Marekani na Ujerumani imetikiswa na kashfa ya kutegwa kwa mawasiliano ya balozi za Ulaya kunakofanywa na shirika la usalama la Marekani na wengi wanahofia athari za kiuchumi na za kisiasa za kashfa hii.

https://p.dw.com/p/1916M
NSA whistleblower Edward Snowden, an analyst with a U.S. defence contractor, is seen in this still image taken from video during an interview by The Guardian in his hotel room in Hong Kong June 6, 2013. Former U.S. spy agency contractor Snowden has applied for political asylum in Russia, a Russian immigration source close to the matter said on July 1, 2013. Picture taken June 6, 2013. REUTERS/Glenn Greenwald/Laura Poitras/Courtesy of The Guardian/Handout via Reuters (CHINA - Tags: POLITICS MEDIA) ATTENTION EDITORS - THIS IMAGE WAS PROVIDED BY A THIRD PARTY. FOR EDITORIAL USE ONLY. NOT FOR SALE FOR MARKETING OR ADVERTISING CAMPAIGNS. NO SALES. NO ARCHIVES. THIS PICTURE WAS PROCESSED BY REUTERS TO ENHANCE QUALITY. NO THIRD PARTY SALES. NOT FOR USE BY REUTERS THIRD PARTY DISTRIBUTORS. MANDATORY CREDIT
Edward SnowdenPicha: Reuters

Wanasiasa wa Ujerumani wameonesha hasira zao kwa kile kinachoonekana kama kiwango kikubwa kabisa cha taarifa ambazo Marekani huzikusanya kutoka nchi hii kupitia utegaji wa mawasiliano ya simu na mitandao. Kiasi cha taarifa nusu bilioni hukusanywa kila mwezi.

Lakini licha ya kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka, jambo ambalo haliwezi kusahaulika ni kwamba Ujerumani, Umoja wa Ulaya na Marekani ni marafiki wakubwa.

Hapo jana Ujerumani ilikataa maombi ya hifadhi yaliyotumwa na Edward Snowden, mtu aliyevujisha taarifa kadhaa za kijasusi ikiwemo hii ya Marekani kuwachunguza washirika wake wa jadi, licha ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, kukiri kwamba kupokea maombi hayo.

“Ninaweza kuthibitihsa kwamba leo majira ya asubuhi kiasi cha saa 8 na dakika 11 tumepokea maombi ya hifadhi ya Bwana Snowden. Sasa tutayapitia maombi haya kwa haki na kwa sheria.“ Alisema Westewelle.

Ulaya haiko tayari kukwaruzana na Marekani

Kuonesha kwamba hakuna nchi ya Ulaya inayotaka kuingia kwenye mgogoro na Marekani, hata baada ya kuibuliwa kwa kashfa hii, usiku wa jana ndege iliyomchukua Rais Evo Morales wa Bolivia ilikataliwa kuruka kwenye anga za mataifa kadhaa ya Ulaya, kufuatia uvumi kwamba Snowden alikuwamo kwenye ndege hiyo.

Rais Evo Morales wa Bolivia ambaye ndege yake ililazimika kutua Vienna ikihofiwa kumbeba Edward Snowden siku ya tarehe 3 Julai 2013.
Rais Evo Morales wa Bolivia ambaye ndege yake ililazimika kutua Vienna ikihofiwa kumbeba Edward Snowden siku ya tarehe 3 Julai 2013.Picha: Reuters

Kuna wengine wanaoamini kwamba hasira zinazoelezewa kuwapo miongoni mwa wanasiasa barani Ulaya zimetiwa chumvi mno, ingawa suala la nini Marekani inafanya na kiwango kikubwa cha taarifa inachokusanya kutoka Ulaya linagusa upande wa kiuchumi pia.

Hans Michelbach, kiongozi wa wabunge wa CSU, amesema kwamba kuna zaidi ya siasa kwenye suala hili, kwani Marekani inafahamu kuwa Umoja wa Ulaya hauungi mkono magaidi, lakini ni mshindani mkubwa kwenye soko la dunia.

Kwa mujibu wa Michelbach, hilo linazusha wasiwasi kwamba sio tu taasisi za serikali za Ujermani na Ulaya zinachunguzwa, bali pia kampuni na taasisi za kibiashara, na hivyo kuipatia Marekani fursa isiyo ya haki kwenye biashara.“

Tayari Waziri wa Maslahi ya Watumiaji wa Ujerumani, Ilse Aigner, ameshaonya kwamba kutumia kisingizio cha vita dhidi ya ugaidi kunaweza kuziba harakati za kuuhujumu uchumi na serikali kwa wakati mmoja.

Wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema kwamba hujuma za mawasiliano zilizigharimu kampuni za Ujerumani euro bilioni 4.2 mwaka jana pekee.

Mwandishi: Jeniffer Fraczek
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Iddi Ssessanga