1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kashfa ya rushwa Uturuki, mashambulizi ya Volgograd magazetini

Admin.WagnerD30 Desemba 2013

Wahari wanazungumzia kashfa kubwa ya rushwa inayoitikisa Uturuki, hoja ya kudhibiti wahamiaji wa kiuchumi nchini Ujerumani na mashambulizi katika mji wa Volgograd nchini Urusi.

https://p.dw.com/p/1AiSs
Türkei Korruptionsskandal Ausschreitungen Istanbul 27.12.13 Premierminister Recep Tayyip Erdogan
Picha: picture-alliance/landov

Mhariri wa gazeti la Märkische Oderzeitung juu ya hali nchini Uturuki na anasema dunia inafuta macho kwa mshangao kutokana na kinachoendelea nchini Uturuki. Uturuki inakabiliwa na kashfa kubwa zaidi ya rushwa kuwahi kushuhudiwa katika historia yake, na mkuu wa serikali ya nchi hiyo anaishughulikia kashfa hiyo kwa kutumia dhana za njama.

Amewaondoa majaji na maafisa wa polisi katika uchunguzi wa kashfa hiyo kwa kuwahisi kuwa wanawasaidia wapinzani wake, na anatumia ukandamizaji dhidi ya waandamanaji katika mji wa zamani wa Istanbul. Inavyoelekea ni kama Erdogan anataka kujenga mfumo wa utawala wa kimabavu kama wa rais Putin wa Urusi na ambako wanasiasa wanajaza mifuko yao bila kuchunguzwa.

Kuhusu suala hilo la Uturuki, mhariri wa gazeti la Landeszeitung anazungumzia udhibiti wa vyombo vya habari, kubadilishwa kwa mawaziri, kuachishwa kazi kwa maafisa kadhaa wa polisi, na mapambano ya madaraka kati ya serikali na mahakama. Mhariri huyo anasema:

Erdogan anafanya kama waziri mkuu ambaye amesimama huku mgongo wake ameuegemeza kwenye ukuta. Hadi sasa bado ana uungwaji mkono hasa katika maeneo ya vijijini. Lakini kashfa hiyo kubwa ya rushwa ambayo inawagusa pia wanafamilia wake inaweza kumsambaratisha waziri mkuu huyo. Kwa sababu inahusu kujitajirisha kwa wanasiasa, ambako hakuna Muturuki yeyote anaweza kukubaliano nako. Na hilo linaweza kujionyesha wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi Machi.

Mhariri wa gazeti la Volksstimme anazungumzia hoja ya chama cha Christian Social Union CSU kutaka kudhibitiwa kwa kile kinachojulikana kama wahamiaji wa kiuchumi, na anasema:

Chama hicho kinataka kurudisha nyuma magurudumu ya historia kwa kuifunga mipaka. CSU kinahofu kwamba kuanzia mwezi Januari wahamiaji wa kiuchumi kutoka Romania na Bulgaria wataanza kuingia nchini Ujerumani. Kwa kaulimbiu ya "anaedanganya arudishwe," chama hicho kinajisafishia njia ya kushinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi Machi na pia uchaguzi wa bunge la Ulaya mwezi Mei. Ni mchezo mchafu unaoendeshwa na CSU. Kaulimbiu hizo ni sawa na matashi ya wanasiasa wanaotafuta umaarufu.

Lakini Mhariri wa gazeti la Straubinger Tagblatt, anasema hakuna asiyejua kwamba watu maskini kama vile wa kabila la Roma wanaobaguliwa, watakimbilia kuja Ujerumani wakijua kwamba watapokea kiasi kizuri tu cha pesa bila ya kufanya kazi. Anasema wanasiasa hawapaswi kuwatisha sana raia juu ya suala hili, lakini wanapaswa kulichukulia kwa uzito.

Mhariri wa gazeti la Frankfurter Allgemeiner anazungumzia juu ya mashambulizi katika mji wa Volgograd nchini Urusi na anaanza kuwa kusema:

Rais Putin aliwaachilia huru wanamuziki wa kundi la Pussy-Riot na wanaharakti wa shirika la kutetea mazingira la Greenpeace, na pia kumsamehe Mikhail Khodorkovsky. Hizi zilikuwa ishara za kujenga taswira yake nje ya Urusi, lakini pia kutoa ishara ya kwa ndani.

Putin ana nguvu ya kutosha kuweza kukabiliana na wapinzani wake kwa upole. Wahusika wa mashambulizi ya Volgograd ikiwa wanakamatwa na walinusirika katika mashambulizi hayo, hawawezi kupata msamaha wa rais.

Katika mapambano dhidi ya makundi yenye itikadi kali za Kiilsamu, vyombo vya usalama vya Urusi vinatumia unyama wa kupita mpaka. Huu ndiyo upande wa pili wa sera ya matumizi ya nguvu - ambayo inachangia kuwapeleka watu wengi zaidi katika maficho.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman