1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katiba mpya yaelekea kukubalika Kenya

Halima Nyanza5 Agosti 2010

Matokeo ya kura ya maoni iliyopigwa jana nchini Kenya ya kuikataa ama kuikubali katiba mpya, yanaonesha kuwa Wakenya wanataka mabadiliko ya katiba hiyo

https://p.dw.com/p/OcJ3
Rais Mwai Kibaki wa Kenya akipiga kura yake.Picha: AP

Kenya, inaelekea kuikubali katiba mpya baada ya matokeo ya awali ya kura ya maoni iliyopigwa jana ya kuikubali ama kuikataa katiba hiyo, kuonesha kwamba zaidi ya theluthi mbili ya kura zilizopigwa katika kura hiyo ya maoni zinapendelea katiba mpya.

Kura zaidi ya milioni sita ambazo zimehesabiwa hadi kufikia saa sita ya usiku, zimeonesha kuwa asilimia 66.9 wamepigia kura ya ndio kutaka katiba mpya, huku matokeo kamili yakitarajiwa kutangazwa baadaye leo, mara tu kura zote zitakapohesabiwa.

Nao waangalizi wa zoezi hilo wamesema wameridhishwa mwenendo mzima wa upigaji kura na kutaka utulivu wakati kura hizo zikiendelea kuhesabiwa.

Zoezi hilo la upigaji kura lilifanyika jana kwa amani na utulivu katika maeneo yote nchini humo.

Referendum in Kenia Dossierbild 3/3
Misururu mirefu ya Wakenya wakisubiri kupiga kura kwa amani kuamua hatma ya katiba mpya.

Jumla ya watu milioni 12.5 walijiandikisha kupiga kura.

Katiba hiyo mpya ina lengo la kupunguza madaraka ya rais na kuwapa haki zaidi raia.

Kambi ya wanaoiunga mkono katiba hiyo inaongozwa na  Rais Mwai Kibaki na Waziri mkuu Raila Odinga.