1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KATIBA YA KENYA

12 Machi 2010

Suala kwamba vyama vya kisiasa nchini Kenya vimekuwa viking'ang'ana kuikarabati katiba tangu Februari 2008 katika jitihada za kumaliza vurugu baada ya uchaguzi na kuleta haki, lina maana kubwa kwa mwananchi wa kawaida.

https://p.dw.com/p/MRKS
Wananchi wa Kenya wataka mabadiliko ya KatibaPicha: picture-alliance/dpa
Ingawa baadhi yao hawaelewi maneno makubwa yanayotumika ndani ya katiba yenyewe, mwananchi huamini kwamba katiba mpya itaifanya kuwa jukumu kuu la serikali nchini humo kuhakikisha kwamba familia mbali mbali zinapata vitu kama chakula, hifadhi, maji pamoja na huduma za afya kwa urahisi.

Kwa mkenya kama Lilian Mutuku, aliye na umri wa miaka 3, na mama wa watoto wawatatu, yeye anasema kwamba kila siku masuala yanayomwacha na fikra nyingi ni jinsi gani atakavyoweza kuwafundisha na kuwalisha wanawe, ijapokuwa serikali ya Kenya imetangaza mpango wa elimu ya bure kwa shule za msingi, bado analo tatizo la kuwepo kwa idadi ndogo ya waalimu shuleni, suala linalomlazimu kulipa shilingi100 ambayo kwake yeye ni pesa nyingi kutoka kwenye pato lake .

Mashirika mbalimbali ya kutetea haki za wanawake sasa yamejitokeza na kulaumu kamati ya bunge iliyoteuliwa kushughulikia katiba kwa kuondoa matumaini kwa familia kama vile za Mutuku kuwa na uwezo wa kuilaumu serikali ya Kenya, iwapo watashindwa kupata haki zao za kibinadamu.

Mashirika hayo yameilaumu kamati hiyo teule kwa kuigeuza lugha kwenye kielelezo cha katiba iliyotayarishwa na kamati ya  wataalam, ambapo rasimu ya awali iliyotayarishwa na kamati hiyo ya wataalam ilitoa hakikisho la haki za kijamii  na kiuchumi kwenye katiba, lakini wanasema kwamba kamati  teule kuhusu katiba ilibadilisha lugha na kuwacha dhima ya utekelezaji wa haki hizo kwa bunge.

Katika warsha ya siku moja iliyoandaliwa na mashirika mbalimbali ya wanawake katika mji mkuu wa Nairobi, iliyonuia kuzipitia rasimu zote za kamati  teule ya bunge kuhusu katiba pamoja na ile iliyotayarishwa na kamati ya wataalam,Grace Maingi Kimani, ambaye ni  mkurugenzi wa shirika lisilo la serikali la muungano wa mawakili nchini Kenya, ameeleza kwamba kamati teule ya bunge kuhusu katiba ilivuka mpaka kwa kufanya uamuzi bila kufikiria kwa kuubadili mswada wa haki.

Kimani vilevile ameeleza kwamba kamati hiyo ilikosa kwa kupendekeza kufutwa kwa  jukumu la serikali kutilia mkazo  sheria za kimataifa kuhusu haki za kibinadamu pamoja na kufutwa kwa utoaji wa haki  za kijamii na kiuchumi na kuacha maamuzi kwa bunge kuamua lini na kwa jinsi gani haki hizo na viwango vyake  vinapoweza kutumika katika hadhi ya kitaifa.

Hata hivyo, mwenyekiti wa kamati hiyo teule ya bunge,  Mohammed Abdikadir,  anasema kwamba katiba ni stakabadhi inayotoa mwongozo wa uongozi wa taifa, na mambo mengine yanapaswa kujumuishwa kuwa sheria. 

Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu, hata hivyo, yanasalia kuwa na shauku iwapo swala la haki za binadamu linaweza kukabidhiwa wabunge ambao mara kwa mara huzozana.

Hivi sasa rasimu hiyo ipo bungeni ambapo bunge lina muda wa siku 30 kuijadili na kuamua iwapo itapasishwa. Wabunge wanahitaji wingi wa thuluthi mbili ya kura kuwezesha kufanywa mabadiliko kwenye kielelezo hicho .

Kupinga kubadilishwa kwake, mashirika yanayohusika na haki za wanawake, likiwemo shirika la Muungano wa Mawakili Wanawake la FIDA Kenya, shirika la msaada la Urgent Action Fund, na kituo cha elimu na uhamasisho kuhusu haki cha Center For Rights Education Awareness na kile cha African Woman and  Child Feature Services, yamewasilisha taarifa kwa bunge kutaka kutumika rasimu ile ya kamati ya wataalam ambayo imetajwa kutambua haki za wanawake.

Mwandishi: Maryam Dodo Abdalla/IPS

Mhariri: Miraji Othman