1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ashutumiwa vikali

25 Julai 2010

Kimbunga cha kisiasa chaikumba Umoja wa Mataifa kufuatia kuvuja kwa vyombo vya habari shutuma kali dhidi ya Katibu Mkuu wa umoja huo, Ban Ki-moon.

https://p.dw.com/p/OUL0
UN Secretary General Ban Ki-moon speaks to the media as he visits a UN housing project in Khan Younis refugee camp, southern Gaza Strip, Sunday, March 21, 2010. U.N. chief Ban Ki-moon has entered the blockaded Gaza Strip, where 1.5 million people have been under lockdown by Israel and Egypt for nearly three years .(AP Photo/Khalil Hamra)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon.Picha: AP

Afisa mwandamizi wa Umoja wa Mataifa ashutumu vikali uongozi wa Katibu Mkuu Ban Ki-moon kwa kutokuwa na ushirikiano,kuvuka mipaka ya madaraka yake na undumila kuwili. Akijibu shutuma hizo kali zilizotolewa na Msaidizi wa Katibu Mkuu anayeondoka madarakani Inga Ahlenius mojawapo wa maafisa wa ngazi ya juu kabisa wa Umoja wa Mataifa Ban amesema anakaribisha shutuma kwa nia ya kuleta tija.

Amesema na hapa nakariri 'lakini kama watumishi wa umma kuna sheria na taratibu.Katika kesi hii uaminifu na mshikamano vimevunjwa." mwisho wa kukariri.

Ban ameuambia mkutano wa wasaidizi wake waandamizi ilikuwa inasikitisha kwamba waraka huo wa siri umevuja kwa vyombo vya habari.

Gazeti la Washington Post lilitowa habari hizo hivi karibuni lakini ilinukuu tu baadhi ya dondoo kutoka repoti hiyo ambapo kwayo Ahlenius mkaguzi mkuu wa zamani wa mahesabu nchini Sweden aliutilia mashaka uongozi wenyewe binafsi wa Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.

Mwanamama huyo alimshutumu Ban kwa kutokuwa na ushirikiano kupindukia mipaka ya madaraka yake katika uteuzi fulani wa ngazi za juu, undumila kuwili katika suala la kutimua wafanyakazi na ukosefu wa utawala bora.

Angela Kane msaidizi wa katibu mkuu kwa idara ya usimamizi amewaambia waandishi wa habari kwamba kuna makosa mengi katika repoti hiyo ya Ahlenius lakini maudhui yake yataangaliwa kwa makini.

Alipoulizwa iwapo repoti hiyo itatolewa hadharani amesema huo ni waraka wa ndani na nyenzo ya idara ya usimamizi ambayo haikukusudiwa kuanikwa hadharani.

IPS ni shirika pekee la habari lililoufuma waraka huo wa kurasa 50 uliotumwa kwenye mtandao wake.

Baada ya kuusoma waraka huo balozi mmoja kutoka nchi zinazoendelea ameliambia shirika la habari la IPS kwamba madai hayo yanafadhaisha na inawezekana kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kumtaka katibu mkuu ajibu madai hayo kwa kujieleza kipengele kwa kipengele.

Baada ya kutumikia mamlaka ya Umoja wa Mataifa kwa miaka saba Ahlenius alitumia miaka yake mitano ya mwisho akiwa mkuu wa Ofisi ya Usimamizi wa Ndani ambacho ni kitengo cha uchunguzi cha chombo hicho cha dunia.

Ahlenius ameandika katika 'Repoti ya Kumaliza Majukumu' kwamba hakuna uwazi na kuna ukosefu wa uwajibikaji na badala ya Ban kukiunga mkono kitengo hicho ambayo ni ishara ya uongozi madhubuti na utawala bora kiongozi huyo amekuwa akijitahidi kutaka kukidhibiti kitengo hicho na hiyo kukidhoofisha.Kutokana na hayo ameandika kwamba haoni kama kuna mageuzi yoyote yale katika Umoja wa Mataifa.

Katika shutuma hizo kali mwanamama huyo amesema itachukuwa muda kuona madhara yaliosababishwa na katibu mkuu huyo dhaifu kwa sababu mchakato wa kushuka kwa hadhi na kudhoofika kwa umoja huo unakwenda kimya kimya.

Pia amemshutumu katibu mkuu Ban kwa kudhoofisha madaraka ya washauri wake waandamizi kwa kuwapa mikataba mifupi ya mwaka mmoja na pia kutumia mamlaka yake moja kwa moja katika ajira ya wafanyakazi wao.

Kwa mujibu wa Ahlenius nyadhifa za ngazi za juu zimegeuzwa kuwa za kisiasa mtindo ambao unahatarisha ajira inayozingatia sifa na kushusha morali pamoja na kupuuzwa kwa uwezo wa sekreteriati ya Umoja wa Mataifa idara ya uongozi ya umoja huo.

Repoti yake pia inataja utamaduni wa kufanya mambo kwa siri uliojengeka kwenye umoja huo ambao hausaidii ziada ya kuchochea uvumi na umbea na hatimae kutoaminiana ndani ya umoja huo na kati ya umoja huo na washika dau wake wa nje vikiwemo vyombo vya habari.

Kwa ufupi kiongozi huyo mwandamizi wa Umoja wa Mataifa anatanabahisha chombo hicho kiko kwenye mchakato wa kushuka kwa hadhi yake na kuzidi kupoteza umuhimu wake kama mshirika anayefaa katika utatuzi wa matatizo ya dunia jambo ambalo hatimae litaathiri amani na utengamano duniani.

Mwandishi: Mohamed Dahman/IPS

Mhariri:P.Martin