1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya kuomba kupatiwa muda wa hadhi maalum katika sekta ya sukari

Sekione Kitojo28 Mei 2007

Kenya inafanya mazungumzo na soko la pamoja la kusini na mashariki ya Afrika, COMESA juu ya kurefushwa kwa muda wa hadhi maalum , uliotolewa kwa sekta ya sukari nchini humo miaka minne iliyopita. Hii ni kutokana na hofu kuwa wazalishaji wa sukari nchini humo hawataweza kupambana na ushindani na wenzao katika kundi hilo la kibiashara wakati muda huo utakapomalizika March 2008.

https://p.dw.com/p/CHDh
Miwa
MiwaPicha: Geraldo Hoffmann

Hadhi hiyo maalum ilitolewa ili Kenya iweze kufanya mageuzi katika viwanda vyake vya sukari ili kuifanya sukari inayozalishwa nchini humo kuweza kushindana na sukari hususan kutoka Malawi, Mauritius na Sudan.

Chini ya makubaliano hayo, Kenya inaruhusiwa kuzuwia uingizaji sukari kutoka mataifa wanachama wa COMESA kwa kiwango cha tani 200,000 kwa mwaka , ikiwa ni upungufu uliopo kati ya uzalishaji wa wastani kwa mwaka na matumizi.

Waziri wa biashara na viwanda nchini Kenya Mukhisa Kituyi ameliambia shirika la habari la IPS kuwa mageuzi ambayo yameahidiwa yanaendelea.

Hayo ni pamoja na kuimarisha uwezo wa hatua za kutengeneza sukari viwandani.

Lakini ameongeza kuwa nchi hiyo haitaweza kushindana ifikapo mwishoni mwa mwezi Februari mwakani.

Maoni hayo yanaungwa mkono pia na Josephat Akoyo, katibu mkuu wa chama cha wazalishaji wa sukari nchini Kenya. Bado tuna safari ndefu mno , ameliambia shirika la IPS. Sekta ya uzalishaji sukari itahitaji muda zaidi ili kuweza kushindana katika soko, katika hali ya sasa iliyomo sekta ya sukari , itasababisha kuathirika.

Amesema kuwa inagharimu kiasi cha dola 450 hadi 600 kuzalisha tani moja ya sukari nchini Kenya, lakini katika nchi nyingine za COMESA uzalishaji unagharimu kiasi cha dola 250.

Kamati ya biashara ya COMESA inatarajiwa kuwasili nchini Kenya mwishoni mwa mwaka huu ili kutathmini uwezo wa mpango wake wa mageuzi na iwapo itoe muda zaidi ya hadhi maalum.

Wakulima wa Kenya wanadai kuwa maoni yao pia yachukuliwe katika suala hili.

Matatizo yanayokumba uzalishaji wa sukari nchini humo ni mengi na lazima yaangaliwe. Wakulima ndio wanaoathirika zaidi, Peter Kadima , mkulima wa miwa ya sukari katika eneo la Mumias , magharibi ya Kenya , amesema katika mahojiano na IPS.

Moja ya malalamiko ya wakulima ni juu ya bei ya juu sana ya mbolea.

Makampuni ya sukari kwa hivi sasa yanawapatia wakulima mbolea kwa mkopo, na kuchukua fedha zao kutokana na mauazo ya miwa ya sukari.

Lakini wakulima wengi wanalalamika kuwa wanalipishwa bei ya juu mno kwa ajili ya mbolea, na kwamba wanapata fedha kidogo kwa mazao yao baada ya kulipa deni la mbolea.

Malipo yanayochelewa ama kutolipwa kabisa , kwa ajili ya miwa inayopelekwa kiwandani pia ni suala la kuangaliwa.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanyika mwaka 2005 katika sekta ya sukari nchini Kenya iliyofanywa na tawi la kundi la Action Aid International nchini Kenya , athari za uingizaji wa sukari kutoka nje inaongezeka nchini Kenya , wenye viwanda hawajawalipa wakulima miwa yao iliyopelekwa kiwandani tangu mwaka 1998. Ilipofika Juni 2004, uchunguzi huo umesema , fedha ambazo ni deni kwa wakulima zilifikia zaidi ya dola milioni 20.

Kutokana na matatizo haya wengi wameacha kilimo cha miwa ya sukari, na kupunguza uwezo wa Kenya kufikia kiwango cha mahitaji yake ya sukari.