1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya, Uganda kushiriki mazungumzo kuhusu mvutano mpakani

Shisia Wasilwa, DW, Nairobi4 Septemba 2020

Kenya kupitia Wizara yake ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, imeanzisha mazungumzo ya kidiplomaisia ya kusuluhisha mkwamo uliopo kwenye mpaka wake na Uganda.

https://p.dw.com/p/3i1JU
COVID-19 I Stau im Grenzgebiet Kenia und Uganda
Picha: Getty Images/AFP/B. Ongoro

Hatua hiyo inafuatia ripoti mpya kuwa Uganda imetoa maagizo mapya yanayohitaji madereva wote wa malori ya masafa marefu, wanaoingia nchini humo kupitia Malaba na Busia kupimwa virusi vya corona hata kama wana vibali kutoka Kenya. 

Msongamano mrefu wa malori ya masafa marefu, wenye urefu wa kati ya kilomita 20 na 30 unashuhudiwa katika mpaka wa Kenya na Uganda. Msongomano huo huenda ukaongezeka iwapo  Uganda na Kenya hazitaafikiana kwa haraka. Madereva wa  Kenya wamekwama baada ya Uganda kuanzisha ada mapya ya kupimwa virusi vya corona.

Madereva wa Kenya wanatakiwa kulipa dola 65 kwa vipimo hivyo.

Makubaliano ya awali kati ya mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliagiza madereva hao kupimiwa ugonjwa wa Covid-19 katika nchi zao, kabla ya kuanza safari. Elisha Abubakar ni dereva aliyekuwa akisafirisha bidhaa katika Jamhuri ya Demokrasia ya Jamhuri ya Congo. Alifika katika mpaka wa Kenya na Uganda tarehe 29 mwezi uliopita, angali anasubiri matokeo ya vipimo alivyochukuliwa.

" Kwa kweli shilingi elfu saba, ni pesa nyingi mno. Hakuna atakayeweza kulipa fedha hizo. Kampuni nyingi zitalazimika kuongeza bei ya usafiri. Serikali ya Kenya na Uganda zije pamoja kutafuta suluhisho.” Amesema  Elisha.

Uganda imetoa maagizo mapya yanayohitaji madereva wote wa malori ya masafa marefu, wanaoingia nchini humo kupitia Malaba na Busia kupimwa virusi vya corona hata kama wana vibali kutoka Kenya
Uganda imetoa maagizo mapya yanayohitaji madereva wote wa malori ya masafa marefu, wanaoingia nchini humo kupitia Malaba na Busia kupimwa virusi vya corona hata kama wana vibali kutoka KenyaPicha: Getty Images/AFP/B. Ongoro

Ada hiyo mpya inaongeza gharama kubwa ya uchukuzi wa bidhaa katika kanda hii ambayo tayari imeathiriwa na janga la Corona. Asilimia 87 ya madereva hao wanasafirisha bidhaa kutoka bandari ya Mombasa nchini Kenya. Naibu Waziri wa Afya nchini Kenya Rashid Aman amesema kuwa, hana ufahamu kwanini Uganda imechukua hatua hiyo. Hata hivyo ameongeza kuwa kutakuwepo na mazungumzo kati ya serikali za mataifa hayo.

"Hili ni suala ambalo linalozungumziwa katika ngazi ya juu. Linajadiliwa katika ngazi ya marais.” Amesema Aman.

Taarifa zinasema kuwa, Uganda iliamua kuchukua hatua hiyo baada ya Kenya kushindwa kuwapima madereva hao, huku ikiwa inakabiliana na mlipuko wa janga hilo. Moses Mulomi ni Naibu wa Gavana wa jimbo la Busia linalopakana na taifa la Uganda.

 Mulomi ameongeza kuwa: "Tukiendelea hivyo wengi watakuja kenya kwa sababu hapa upimaji ni bure, lakini itakuwa changamoto kubwa, kwa sababu ya idadi ya watu watakaohitaji kupimwa. Ni jambo linalostahili kushughulikiwa kwa haraka kwa njia ya kidiplomasia."

Kenya limerekodi visa 34,705 vya maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19. Idadi ya watu walioaga dunia kutokana na janga hilo hadi sasa imefikia 586, huku ya wagonjwa waliopona ikifikia 20644.