1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yapitisha sheria kali dhidi ya vyombo vya habari

1 Novemba 2013

Vyombo vya habari vya Kenya vimekasirishwa na hatua ya bunge kuupitisha mswaada wa sheria unaoipa serikali nguvu za kuwapiga faini kubwa waandishi wa habari kwa kwenda kinyume na kile kinachoitwa 'maadili ya uandishi.'

https://p.dw.com/p/1AA1g
Gazeti la Daily Nation la Kenya.
Gazeti la Daily Nation la Kenya.Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Katika mswaada huo uliopitishwa katika kikao kilichokaa usiku sana siku ya Alhamis (tarehe 31 Oktoba), wabunge wameridhia kuundwa kwa Baraza la Rufaa ya Vyombo vya Habari na Mawasiliano linaloteuliwa na serikali na ambalo wamelipa uwezo wa kutoza faini ya hadi shilingi milioni 20 za Kenya (sawa na euro 173,000 ama dola 234,000 za Kimarekani) kwa wale watakaokutikana na makosa.

Sheria hiyo pia imelipa Baraza hilo la Rufaa nguvu za hata kumfungia mwandishi wa habari asifanye kazi zake.

Sheria hiyo, ambayo sasa inasubiri kusainiwa na Rais Uhuru Kenyatta, inaweka pia udhibiti mkali kwa matangazo ya redio na televisheni, ambapo vituo hivyo vinatakiwa kuhakikisha kuwa asilimia 45 ya kile wanachokitangaza kiwe kimetengenezwa nchini Kenya.

"Sheria ya ukandamizaji"

Gazeti la Daily Nation la Kenya limesema mswaada huo "unaiweka Kenya kwenye kiwango sawa na Zimbabwe, Cuba, Ethiopia na Kuwait" na kwamba utairudisha nchi hiyo kwenye "zama za giza".

Jengo la Westgate wakati lilipokuwa likishambuliwa mwezi Septemba 2013.
Jengo la Westgate wakati lilipokuwa likishambuliwa mwezi Septemba 2013.Picha: Reuters

Gazeti hilo linaloheshimika nchini Kenya limesema katika tahariri yake ya siku ya Ijumaa (tarehe 1 Novemba) kwamba "ghafla moja, bunge limezifuta haki za vyombo vya habari" na kuiita hatua hiyo kuwa ni ya kuogofya ambayo inazua mashaka kwamba bunge hilo halitashindwa hata kuondoa uhuru wa mahakama hapo baadaye.

Kwa mujibu wa gazeti la The Star, sheria hiyo mpya ya vyombo vya habari utaipa serikali "uwezo mkubwa sana" juu ya vyombo hivyo, huku gazeti jengine, The Standard, limesema sasa demokrasia na uhuru wa maoni nchini Kenya "vimepigwa dafrau", likiongeza kwamba sheria hiyo ni ya "ukandamizaji."

Kisingizio cha usalama wa taifa

Kupitishwa kwa mswaada huo kunakuja wakati kukiwa na mkururo wa kile kinachoitwa "hatua za kuimarisha usalama wa taifa" kufuatia mashambulizi ya hapo mwezi Septemba kwenye jengo la maduka la Westgate lililofanywa na wanamgambo wa al-Shabaab.

Wanajeshi wa Kenya wakati wa juhudi za kulikomboa jengo la Westgate, Nairobi, mwezi Septemba 2013.
Wanajeshi wa Kenya wakati wa juhudi za kulikomboa jengo la Westgate, Nairobi, mwezi Septemba 2013.Picha: Reuters/Thomas Mukoya

Vyombo vya habari vya Kenya viliingia kwenye mgogoro na mamlaka nchini humo kwa kutangaza picha zilizochukuliwa kwenye kamera za usalama jengoni humo, ambazo zinawaonesha wanajeshi wakichukua vitu kutoka baadhi ya maduka na kutoka navyo nje kwenye mifuko ya plastiki.

Mara tu baada ya kurushwa kwa picha hizo, mkuu wa polisi, David Kimaiyo, aliwaita waandishi wawili wa habari na mkuu wa kituo cha televisheni cha KTN kwa ajili ya kuwahoji.

Kimaiyo alikuwa amesema kwamba "uhuru wa habari una mipaka yake na kwamba polisi ilikuwa inawafuatilia kwa karibu waandishi wanaopotosha ambao wangelipandishwa mahakamani hivi punde.

Baadaye serikali ilifuta wito huo, baada ya kushambuliwa vikali na vyombo vya habari.

"Baada ya mashauriano ya kina, wito huo umefutwa," alisema afisa mmoja kutoka Wizara ya Ndani, akiongeza kwamba waandishi hao wa habari, Mohammed Ali na Allan Namu wanaoendesha kipindi cha habari za uchunguzi cha Jicho Pevu, na mkuu wao hawakupaswa tena kuhudhuria kwenye kituo cha polisi kwa mahojiano.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf