1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yatangaza hatua mpya za kupambana na corona

4 Novemba 2020

Muda wa kutotoka nje usiku nchini Kenya umebadilishwa na sasa utaanzia saa nne usiku hadi kumi alfajiri. Wakati huo huo, mikutano ya kisiasa imesitishwa kwa siku 60 zijazo.

https://p.dw.com/p/3ks1b
Kenia Corona-Pandemie
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Inganga

Kwenye hotuba yake ya 13 kuhusu janga la COVID 19, Rais Uhuru Kenyatta aliweka bayana kuwa Kenya inakitazama ana kwa ana kipindi cha wimbi kubwa la maambukizi mapya ya corona. Ili kupambana na hali hiyo, kuanzia usiku wa leo vilabu vya pombe na mikahawa itafungwa mapema kwa saa moja yaani saa 9 usiku kabla ya muda wa kutotoka nje kuanza kutekelezwa saa nne usiku hadi kumi alfajiri. Marufuku hiyo itaendelea hadi tarehe 3 mwezi Januari mwakani. Itakumbukwa kuwa muda wa kutotoka nje ilikuwa kuanzia saa tano usiku hadi kumi alfajiri.

Rais Kenyatta amewahimiza wamiliki na wasimamizi wa mikahawa na vilabu vya pombe kuchukua tahadhari zote kuhakikisha kuwa sera za kuzuwia kutangamana na kusogeleana zinafuatwa kikamilifu.

Coronavirus Afrika Kenia Nairobi Kibera Slum Essensausgabe
Mikusanyiko ya watu wengi imepigwa marufukuPicha: picture-alliance/AP/B. Inganga

Tangazo hilo jipya linasisitiza pia kuwa sheria za kuhudhuria ibada na mikutano ya kidini bado ziko pale pale. Haya yanajiri baada ya kikao cha Rais Kenyatta na baraza la magavana kufanyika mapema hii leo kwenye ikulu ya Nairobi. Kwenye mkutano huo, mwenyekiti wa baraza la magavana, Wyclif Oparanya alimsisitizia Rais Kenyatta kuubana zaidi muda wa kutotoka nje wakati wa usiku kwani hali ni mbaya mikoani hususan kwenye hospitali za kaunti.

Takwimu zinaashiria kuwa idadi ya wagonjwa wanaolazwa kwenye hospitali kwa kuambukizwa COVID-19 imeongezeka kwa asilimia 140 katika kipindi cha siku 38 tangu sheria za kutangamana na kutoka nje kulegezwa. Kwa mantiki hii shule za msingi pia nazo zitafunguliwa tena Januari mwakani.

Maafisa wa serikali na umma walio na umri uliozidi miaka 58 wameagizwa kufanya kazi kutokea nyumbani ila wanaohudumu kwenye sekta muhimu hawapo kwenye orodha hiyo. Kwa sasa kampeni ya ''bila barakoa hakuna huduma'' ndio imezinduliwa rasmi kote nchini ili kupambana na wimbi jipya la virusi vya corona. Kisa cha kwanza cha COVID-19 kiliripotiwa mwezi Machi mwaka huu na ndipo serikali ilipoanza rasmi kutangaza sheria za kutotangamana na kusogeleana kadhalika kuosha mikono kila wakati. TM, DW Nairobi.

Thelma Mwadzaya, DW Nairobi