1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenyatta rais wa nne wa Kenya

Mohamed Dahman9 Machi 2013

Mwana wa kiume wa muasisi wa taifa la Kenya, Uhuru Kenyatta, ameshinda uchaguzi wa rais kwa asilimia 50.07 ya kura kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi na hivyo kuepuka marudio ya uchaguzi.

https://p.dw.com/p/17uCM
Kenya's Deputy Prime Minister Uhuru Kenyatta (L), who is also the Jubilee alliance presidential candidate (R), and his running mate former cabinet minister William Ruto wave to their supporters during a rally in Kenya's capital Nairobi in this January 12, 2013 file photo. East Africa's most powerful economy and a key regional ally in the U.S.-led war against militant Islam could next month elect a president accused of crimes against humanity, posing a diplomatic headache for Western capitals. If Kenyatta wins the March 4 poll, Kenya will become the second country after Sudan to have a sitting president facing trial at the International Criminal Court in The Hague. Picture taken January 12, 2013. To match story KENYA-ELECTIONS/SANCTIONS REUTERS/Noor Khamis/Files (KENYA - Tags: ELECTIONS POLITICS)
Kenia Wahlen Uhuru Kenyatta und William RutoPicha: Reuters

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo Isaack Hassan Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi amesema Kenyatta amejipatia asilimia 50.07 ya kura ambazo ni kura milioni 6.13 kulinganishwa na kura milioni 5.3 alizopata mpinzani wake Raila Odinga.Kutokana na matokeo hayo Hassan amemtangaza rasmi Kenyatta kuwa rais mteule wa Kenya.

Kenyatta anakabiliwa na mashtaka ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu kufuatia uchaguzi wa Kenya wa mwaka 2007 uliozusha umwagaji damu wa kikabila.

Baada ya kuibuka kwa matokeo ya awali leo alfajiri wafuasi wa Kenyatta wenye furaha walimiminika katika mitaa ya Nairobi na katika miji yenye wafuasi wake wakuu wa kikabila wakishehereka kwa kuwasha fataki na kupeperusha matawi ya miti huku wakiimba: "Uhuru, Uhuru, Uhuru!"

Jumuiya ya kimataifa na ushindi wa Uhuru

Kufuatia kutangazwa kwake na Tume ya Uchaguzi kuwa mshindi wa uchaguzi huo Kenya inakuwa nchi ya pili ya Afrika baada ya Sudan kuwa na rais aliyeko madarakani anayekabiliwa na mashataka katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC yenye makao yake huko The Hague nchini Uholanzi.

Wafuasi wa Uhuru Kenyatta wakishangiria ushindi wa kiongozi wao.
Wafuasi wa Uhuru Kenyatta wakishangiria ushindi wa kiongozi wao.Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Marekani na mataifa mengine ya magharibi yalisema kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo kwamba ushindi wa Kenyatta utafanya uhusiano wa kidiplomasia na nchi hiyo kuwa mgumu ambayo ni mshirika muhimu katika vita dhidi ya wanamgambo wa itikadi kali za Kiislam katika kanda hiyo.

Mwanadiplomasia mmoja wa mataifa ya Magharibi amesema kwamba halitokuwa tatizo iwapo Kenyatta atatowa ushirikiano wake kwa mahakama ya ICC na kwamba wanaheshimu uamuzi wa wapiga kura walio wengi nchini Kenya.

Vipi serikali za nchi za Magharibi zitaishughulikia Kenya chini ya utawala wa Kenyatta na kwa kiasi gani zitakuwa tayari kushikiana na serikali yake itategemea sana jinsi Kenyatta mwenyewe na mgombea mwenza wake William Ruto ambaye pia anashtakiwa katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC watakavyotowa ushirikiano wao kwa mahakama hiyo.

Wote wawili Kenyatta na Ruto wamesema kwamba watajitahidi kusafisha majina yao juu ya kwamba Kenyatta ilibidi azime vijembe vya Odinga wakati wa kampeni kwamba itabidi aongoze serikali kwa kutumia Skype kutoka The Hague makao makuu ya mahakama ya ICC.

Kisumu kuna wasiwasi

Lakini hali ya wasi wasi imetanda katika mji wenye wafuasi wengi wa mpizani wa Kenyatta Waziri Mkuu Raila Odinga ambaye yuko nyuma ya Kenyatta baada ya kujipatia asilimia 43.28 ya kura .Wafuasi wake walikuwa wakipiga mayowe kwamba "bila ya Raila hakuna amani" huku vikosi vya usalama vikiangalia huko Kisumu ambapo kulizuka ghasia kufuatia uchaguzi wa mwaka 2007.

Wafuasi wa Uhuru Kenyatta wakishangiria ushindi wa kiongozi wao.
Wafuasi wa Uhuru Kenyatta wakishangiria ushindi wa kiongozi wao.Picha: Reuters

Mshauri wa karibu wa Odinga ambaye alishindwa katika uchaguzi wa mwaka 2007, Salim Lone, amesema mgombea wake hatoyakubali matokeo hayo na atawasilisha pingamizi la sheria mahakamani.

Akizungumza kwa niaba ya Odinga kabla ya kutangazwa kwa matokeo ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba Odinga hakubali matokeo hayo ya uchaguzi na kwamba iwapo Uhuru Kenyatta anatangazwa kuwa rais mteule moja kwa moja atakwenda mahakamani kupinga matokeo hayo.

Kambi ya Odinga imesema wakati kura zilipokuwa zikihesabiwa kwamba kuhesabiwa kwa kura kulikuwa na kasoro kubwa sana na kutaka usitishwe. Lakini imeahidi kushughulikia mizozo yoyote ile katika mahakama na sio barabarani.

Wakenya wanatarajia uchaguzi huu ambao hadi sasa umepita salama na kuwepo kwa vurugu kidogo tu wakati wa siku ya kupiga kura utarudisha sifa ya nchi hiyo kama mojawapo ya taifa lenye demokrasia imara barani Afrika baada ya vurugu za baada ya uchaguzi kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1,200 hapo mwaka 2007.

Wakenya waazimia amani

Wakenya wengi wamesema wameazimia kuepuka marudio ya vurugu za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ambazo ziliukwamisha uchumi wa nchi hiyo.

Aliyekuwa mgombea urais nchini Kenya, Peter Kenneth.
Aliyekuwa mgombea urais nchini Kenya, Peter Kenneth.Picha: picture-alliance/dpa

Viongozi wa makanisa huko Kisumu magharibi ya Kenya ambapo miaka mitano iliopita uliathirika vibaya safari hii wamechukuwa juhudi za kuondowa hali ya mvutano.

Waangalizi wa kimataifa kwa kiasi kikubwa wamesema kwamba uchaguzi huo na zoezi la kuhesabu kura vimefanyika kwa uwazi hadi sasa na tume ya uchaguzi ambayo imechukuwa nafasi ya ile ya zamani iliopoteza sifa iliahidi kuwepo kwa uchaguzi wa kuaminika.

Ili kuweza kushinda duru ya kwanza, mgombea alikuwa anahitajika kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura.

Takwimu za kura

Takwimu za tume ya uchaguzi zimeonyesha kwamba Kenyatta ameshinda kura 6,173,433 kati ya jumla ya kura 12,338,667 zilizopigwa.Odinga amejipatia kura 5,340,546.

Uhuru Kenyatta siku ya kupiga kura.
Uhuru Kenyatta siku ya kupiga kura.Picha: Getty Images

Ushindi huo wa duru ya kwanza unamaanisha kwamba Wakenya waliokuwa wamesubiri kwa siku tano kujuwa matokeo hivi sasa hawatokuwa na duru ya pili ya uchaguzi ambayo ingeongeza hali ya wasi wasi nchini humo.

Pande zote mbili zimekuwa zikitegemea mno makundi yao ya kikabila katika taifa ambapo utiifu wa kikabila mara nyingi umekuwa juu kuliko itikadi wakati wa kupiga kura. Kenyatta ni Mkikuyu ambalo ni kabila kubwa nchini Kenya, Odinga ni Mjaluo. Wote waili wana wagombea wenza kutoka makabila mengine.

Wakenya wengi wanasema uchaguzi huu ulikuwa na uwazi zaidi. Idadi ya watu iliojitokeza kupiga kura ni asilimia 86 kati ya watu milioni 14.3 waliostahiki kupiga kura.

Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters
Mwandishi: Mohamed Khelef