1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

Waziri mkuu wa zamani wa China Li Keqiang afariki dunia

Lilian Mtono
27 Oktoba 2023

Waziri mkuu wa zamani wa China Li Keqiang amefariki dunia baada ya kupata shambulizi la moyo lililompata ghafla akiwa mapumzikoni, Shanghai.

https://p.dw.com/p/4Y5Gm
Li Keqiang enzi ya uhai wake akizungumza katika mkutano kati ya China, Korea Kusini na Japan uliofanyika Chengdu, kusinimagharibi mwa China Disemba 24, 2019
Li Keqiang enzi ya uhai wake akizungumza katika mkutano kati ya China, Korea Kusini na Japan uliofanyika Chengdu, kusinimagharibi mwa China Disemba 24, 2019Picha: Wang Zhao/Pool/Getty Images

Kituo cha utangazaji cha CCTV kimearifu kwamba Li Keqiang aliyekuwa mapumzikoni jijini Shanghai katika siku za karibuni alipata shambulizi la ghafla la moyo jana Alhamisi na jitihada za kunusuru maisha yake hazikufanikiwa na hatimaye kufariki majira ya mapema hii leo, Ijumaa. 

Keqiang aliyekuwa na miaka 68 amefariki ikiwa ni miezi 10 baada ya kustaafu shughuli za kiserikali. Alikuwa waziri mkuu na kiongozi wa baraza la mawaziri chini ya rais Xi Jinping kwa miaka kumi hadi alipojiuzulu mwezi Machi.

Keqiang anakumbukwa kama kiongozi aliyependelea mageuzi, tofauti na wenzake wanaopenda kuonyesha misimamo mikali na kutobadilika.