1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kerry ziarani Afrika

30 Aprili 2014

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry anawasili mjini Addis Ababa, Ethiopia leo kituo cha kwanza cha ziara yake barani Afrika akiandamana na zana mbili kuu za diplomasia mazungumzo ya amani na tishio la vikwazo.

https://p.dw.com/p/1BrFZ
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry.
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry.Picha: Reuters

Tishio la vikwazo litatumika kusaidia kutafuta njia ya kukomesha mauaji yaliyodumu kwa miezi kadhaa ambayo yanatishia kulisambaratisha taifa jipya kabisa duniani la Sudan Kusini.

Lakini ni jambo ambalo haliko wazi iwapo Marekani itaiwekea vikwazo Sudan Kusini wakati Kerry atakapolizuru taifa hilo katika ziara yake ya wiki moja barani Afrika inayojumuisha nchi za Ethiopia,Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Angola.

Maafisa wa serikali ya Marekani bado wamekuwa wakijaribu kuzishawishi nchi hizo jirani na Sudan Kusini kutowa adhabu kwa watu wanaohusika na mapigano ya kinyama katika nchi hiyo.

Marekani yaandaa vikwazo

Afisa mwandamizi wa serikali ya Marekani anayeandamana na Kerry katika ziara hiyo amesema Marekani bado ingali inaandaa orodha yake yenyewe ya watu binafsi ambao mali zao zinaweza kuzuiliwa na wao wenyewe kupigwa marufuku kusafiri kwenda Marekani.

Vikosi vya serikali ya Sudan Kusini.
Vikosi vya serikali ya Sudan Kusini.Picha: Samir Bol/AFP/Getty Images

Kerry anawasili katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Abba leo hii ambapo atakutana na viongozi wa Umoja wa Afrika kujadili masuala mbali mbali ya usalama yanayolikabili eneo la kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika ikiwemo Sudan Kusini.Kwa mujibu wa afisa huyo wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani ambaye hakutaka kutajwa jina Marekani inautaka Umoja wa Afrika kuweka vikosi vya kulinda amani Sudan Kusini lakini suala hilo bado linajadiliwa.

Ethiopia imekuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Sudan Kusini na waasi yenye lengo la kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miezi minne vilivyosababisha maafa ambapo maelfu wamepoteza maisha yao na zaidi ya watu milioni moja kupoteza makaazi yao.

Kuvunja makundi ya waasi Congo

Kerry anatarajiwa katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Kinshasa hapo Jumamosi kukutana na Rais Joseph Kabila kwa mazungumzo juu ya kuyavunja makundi ya waasi na kusalimisha silaha zao na kuanzisha demokrasia kabla ya uchaguzi uliopangwa kufanyika mwakani.

Waasi wa kundi la M23 lililosambaratishwa na vikosi vya serikali vikisaidiwa na vya Umoja wa Mataifa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Waasi wa kundi la M23 lililosambaratishwa na vikosi vya serikali vikisaidiwa na vya Umoja wa Mataifa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.Picha: picture-alliance/AP

Kerry ataandamana na mjumbe maalum wa Marekani kwa nchi za Maziwa Makuu Russ Feingold ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kufanikisha makubaliano ya amani na waasi wa kundi la M23 ambao wamekuwa na uhasama na serikali ulioanzia mwaka 1994.

Katika kituo chake cha mwisho katika nchi yenye utajiri wa mafuta Angola Kerry atakutana Rais Eduardo dos Santos. Afisa wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani amesema Waangola wamekuwa wakitimiza dhima isio ya kawaida hususan kuhusiana na suala la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na hivi karibuni pia katika suala la Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Mwandishi: Mohamed Dahman /AFP/AP

Mhariri : Josephat Charo