1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi kuhusu vibonzo vya Mtume Mohammed

13 Aprili 2012

Raia wanne wa Sweden wamepandishwa kizimbani Denmark ili kujibu mashtaka ya kupanga shambulio katika ofisi za gazeti moja la Denmark ambalo mwaka 2005 lilichapisha vibonzo vya kumkashifu Mtume Mohammed.

https://p.dw.com/p/14dP7
Vibonzo vya Mtume Mohammed katika magazeti
Vibonzo vya Mtume Mohammed katika magazetiPicha: picture-alliance/dpa

Jengo la gazeti hilo liitwalo Jylands Posten liko mjini Copenhagen, nchini Denmark. Kwa sasa jengo hilo lina vyombo vya usalama vya kila aina pamoja na walinzi ambao kazi yao ni kuwazuia watu wasio na kibali kuingia katika jengo hilo. Gazeti la Jylands Posten lina maadui wengi, kwani mwishoni mwa mwaka 2005 gazeti hilo lilichapisha vibonzo 12 vilivyomwonyesha Mtume Mohammed. Vibonzo hivyo vilizua wimbi la hasira miongoni mwa waumini wa dini ya kiislamu. Katika nchi nyingi zenye utawala wa kiislamu, yalifanyika maandamano yaliyoambatana na vurugu ambapo watu wapatao 150 waliuwawa.

Hasira za waislamu wenye itikadi kali zimekuwa zikielekezwa kwa gazeti la Jylands Posten pamoja na mchoraji wa katuni aitwaye Kurt Westergaard, ambaye alichora katuni ya Mtume Mohammed akiwa amevaa kilemba chenye umbo la bomu. Mara kwa mara wafanyakazi wa gazeti hilo pamoja na mchoraji Westergaard walitishiwa kuuwawa au kulipuliwa wakiwa ofisini kwao.

Waandamanaji wakiirarua bendera ya Denmark
Waandamanaji wakiirarua bendera ya DenmarkPicha: picture-alliance/dpa

Mashtaka yote yamekanushwa

Miongoni mwa watu wanaoshukiwa kupanga shambulizi la kigaidi katika ofisi za gazeti hilo ni raia wanne wa Sweden ambao ni Munir Awad, Omar Abdalla Aboelazm, Munir Ben Mohammed Dhahri na Sabhi Ben Mohammed Zalouti. Washukiwa hao walikamatwa na polisi mwaka 2010 baada ya mashirika ya ujasusi ya Denmark na Sweden kuwafuatilia kwa miezi kadhaa. Mbali na kushtakiwa kwa kosa la ugaidi, watu hao watajibu pia shtaka la kubeba silaha bila kibali.

Iwapo watapatikana na hatia, washukiwa hao wanaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 16. Waendesha mashtaka wameeleza kwamba wataiomba serikali ya Denmark iwafukuze watu hao watakapokuwa wamemaliza kifungo chao. Hata hivyo washtakiwa wote wanne wamekanusha mashtaka hayo.

Mchoraji wa vibonzo Kurt Westergaard
Mchoraji wa vibonzo Kurt WestergaardPicha: dapd

Hii ni mara ya pili kuwepo kwa kesi ya namna hiyo, inayohusisha wachoraji wa katuni. Mwaka 2011, makahama moja ya Denmark ilimhukumu raia mmoja wa nchi hiyo mwenye asili ya kisomali kwa kosa la ugaidi kwa sababu aliingia katika nyumba ya mchoraji mmoja wa vibonzo aliyekuwa amechora katuni za Mtume Mohammed. Msomali huyo alimtishia mchoraji kwa shoka lakini mchoraji huyo alifanikiwa kujifungia katika chumba kimoja. Mahakama ilimhukumu Msomali huyo kifungo cha miaka 9 jela.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/Jan Bruck/APE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman