1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Zuma kusikilizwa Agosti 25 mwaka huu

AFP/ Charo Josephat5 Februari 2009

Zuma afunguliwa mlango wa kushinda urais wa Afrika Kusini

https://p.dw.com/p/GnDp
Kiongozi wa chama cha ANC Jacob Zuma akiwahutubia wafuasi wakePicha: picture-alliance/dpa

Mahakama moja nchini Afrika Kusini leo imeweka Agosti 25 kuwa tarehe ya kusikilizwa kwa kesi ya ufisadi inayomkabili kiongozi wa chama cha African National Congress, ANC, bwana Jacob Zuma. Bwana Zuma anakabiliwa na mashtaka ya rushwa, ulaghai, ulanguzi wa fedha na utapeli katika kesi inayoendelea kwa muda mrefu.

Uamuzi wa mahakama ya Pietermaritzburg katika jimbo la KwaZulu-Natal nchini Afrika Kusini anakotokea bwana Jacob Zuma una maana kesi ya kiongozi huyo mashuhuri itasikilizwa baada ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika katikati ya mwezi Aprili mwaka huu. Chama cha ANC kikiwa kikubwa nchini Afrika Kusini kinatarajiwa kushinda uchaguzi huo na Zuma huenda akachaguliwa kuwa rais mpya na bunge jipya litalitakalokuwepo. Kiongozi huyo wa chama cha ANC amefika kwenye mahakama ya Pietermaritzburg na baadaye kuwaambia wafuasi wake waliokuwa wamekusanyika nje ya mahakama hiyo kwamba hatoacha kugombea urais wa Afrika Kusini.

Bwana Zuma amesema na hapa namnukulu, '' Sitajiondoa kwa sababu sijapatikana na hatia na mahakama yoyote ya sheria. Kilichonikuta ni kwamba watu kadhaa wameunda njama wakiwa na lengo la kunifanya nionekane mtu muovu. Kwa hiyo nikijiondoa nitaweka mfano mbaya. Watu watajua unapomchukia mtu, buni hadithi ya uongo na mambo yake yatakwisha,'' mwisho wa kumnukulu.

Bwana Jacob Zuma atarejea mahakamani Juni 24 mwaka huu kuwasilisha ombi la kuifutilia mbali kesi inayomkabili. Mashitaka dhidi ya kiongozi huyo wa chama cha ANC yalifufuliwa tena mwezi uliopita baada ya mahakama ya rufaa kubatilisha uamuzi wa mahakama ya chini iliyofutilia mbali kesi hiyo ya bwana Zuma katika uamuzi uliozitikisa siasa za Afrika Kusini. Uamuzi wa mahakama hiyo ndogo pia ulidokeza kuwa rais wa zamani Thabo Mbeki alihusika katika kesi ya Zuma na hivyo chama cha ANC kikamuondoa madarakani.

Bwana Zuma alizindua kampeni ya chama cha ANC mwezi uliopita kwa ahadi ya kibinafsi ya kuangamiza ufisadi. Chama hicho kimeelezea wasiwasi wake kuhusu jinsi mashtaka dhidi ya kiongozi wake yalivyoendeshwa. Katika taarifa yake chama cha ANC kimesema muda mfupi baada ya tarehe mpya ya kusikilizwa kesi ya kiongozi wake kuwa kitamuunga mkono rais wake katika changamoto zote zinazomkabili. Kimesema kitafuata njia zote za kisheria kuhakikisha rais wake, aliyevumilia miaka minane ya kashfa, fedheha na kushambuliwa kwa maneno makali, anafutiwa mashitaka.

Chama cha ANC kimesema bwana Zuma ataendelea kuwa mgombea wake wa wadhifa wa uraisi katika uchaguzi ujao hata kama kampeni yake itagubikwa na wingu jeusi la kesi inayomsubiri mahakamani. Licha ya mashitaka yanayomkabili, Jacob Zuma anabakia kuwa kiongozi mwenye haiba kubwa anayeonekana kuwavutia wafuasi wengi wa mashinani.