1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Khofu ya madhara ya vyandarua Zanzibar

20 Machi 2012

Visiwani Zanzibar kumezuka khofu juu ya vyandarua vya mbu kusababisha madhara ya kiafya.

https://p.dw.com/p/14O8N
Chandarua cha kujikinga dhidi ya mbu
Chandarua cha kujikinga dhidi ya mbuPicha: picture-alliance/ dpa

Vyandarua hivyo vilivyogaiwa bure kwa wananchi zaidi ya laki saba, chini ya mpango wa shirika la Marekani la Global Fund ili kupambana na ugonjwa wa malaria visiwani humo vinadaiwa kusababisha muwasho na hata vifo kwa watumiaji.

DW ilifanya mahojiano na Meneja wa Mradi wa kudhibiti Malaria visiwani Zanzibar, bwana Abdalla Suleiman, ambae kwanza anaelezea khofu zilizozagaa mitaani Zanzibar juu ya athari za vyandarua hivyo.

Tumepata taarifa kutoka kwa watu ambao hatuwaelewi… taarifa ambazo hazieleweki, kwamba baadhi ya watu wamepata madhara ya vyandarua hivi na wengine wamelazwa hospitali na wengine wamekufa. Hizo ni taarifa ambazo aidha unapigiwa simu... ukimuuliza mtu wewe ni nani na uko sehemu gani anakata simu. Uongozi wa Wizara ya Afya kupitia kitengo cha malaria tumefuatilia taarifa hizi katika mahospitali yote ya Zanzibar Unguja na Pemba na kwa kweli hakuna taarifa ya uhakika ya watu waliolazwa au waliofariki. Taarifa hizo sio za kweli na sisi tunakanusha.

Mbu wanaosababisha Malaria
Mbu wanaosababisha MalariaPicha: Bayer CropScience AG

Swali

Kumekuweko na taarifa zenye utata kuhusiana na matumizi ya vyandarua hivyo. Sijui ungeweza kueleza nini kuhusu matumizi yake?

Jibu

Matumizi ya vyandarua siyo mageni katika nchi za Afrika ya Mashariki, na zaidi Zanzibar. Chandarua kwa kawaida, baada ya mtu kukipata ni kukitumia moja kwa moja hakuna matumizi zaidi yanayohitaji maelezo ya ziada. Ni kukitundika chandarua na kuhakikisha kwamba kimekaa kama ni chini ya godoro, mkeka au sehemu yoyote ya kulalia. Hakuna matumizi ya ziada yanayohitaji kuelezewa isipokuwa ni hayo niliyossema.

Swali

Bwana Suleima hata hivyo kuna ripoti ya baadhi ya madaktari ambao wanasema kwamba vyandarua hivi vina dawa ambayo inaweza kuzusha athari, kwa mfano muwasho mwilini na kadhalika, je mumepata malalamiko yoyote ya aina hiyo hadi sasa?

Jibu

Ni sahihi. Vyandarua hivi ili viweze kufanya kazi inayotakiwa vinakuwa na dawa aina ya Permethrin au Deltamethrin, dawa ambayo inakuwemo kwenye chandarua. Ni aina ya pareto, na ni dawa salama. Kama ilivyo kawaida, kuna baadhi ya watu katika jamii wanakuwa na allergy (madhara yanayopatikana na baadhi ya watu kutokana na kutumia kitu au dawa fulani). Kuna baadhi ya watu ambao walipewa vyandarua hivi walipata hiyo allergy baada ya kuvitumia kwa siku ya mwanzo; mwili kuwasha au uso unakuwa unawasha. Lakini nataka kusema kwamba hili ni jambo la kupita. Wananchi wanashauriwa kwamba, kama mtu anajua ana allergy, akichukue chandarua hicho, akifungue kwenye plastiki yake ili kiweze kupata upepo, kasi ya ile dawa ipungue kidogo, baada ya siku mbili tatu anaweza kukitumia na kitakuwa ni salama upande wake.

Wafanyakazi wa mradi wa Malaria
Wafanyakazi wa mradi wa MalariaPicha: AP

Swali

Na kutokana na sakata hili, ungesema nini hatma ya mradi huu ambao umegharimu mamilioni ya fedha kupambana na malaria huko Zanzibar wakati visiwa hiyvo vinatajwa kuwa ni mfano wa mafanikio katika kuutokomeza ugonjwa wa malaria?

Jibu

Huu mradi kwa kweli hadi sasa unakwenda vizuri, kwa hivyo wito wetu ni kwamba wananchi waendelee kutumia hiyo mikakati iliyowekwa. Hiyo ndio itatupelekea sisi kumaliza malaria Zanzibar. Pindipo wananchi wataacha kutumia vyandarua, au watakataa majumba yao kupigwa dawa, mradi huu unaweza kuwa na hatma mbaya. Lakini hadi sasa tunaendelea vizuri na tunafanya kazi vizuri.

Swali

Na mwisho ungesema nini kuhusu khofu hiyo iiliyozagaa visiwani kuhusu vyandarua?

Jibu

…nawatoa khofu wananchi, na waendelee kutumia vyandarua kama wanavyoshauriwa.

(Kusikiliza mahojiano hayo tafadhali bonyeza alama ya spika za masikioni)

Mwandishi: Hamad Hamad

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman