1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kikao cha kilele cha Baraza la UN kuanza rasmi

23 Septemba 2009

Mkutano wa kilele wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa unatarajiwa kuanza rasmi hii leo mjini Newyork.Ajenda kuu ya kikao hicho inajumuisha majadiliano ya masuala ya ugaidi,kusambaa kwa silaha za nuklia pamoja na umasikini

https://p.dw.com/p/JmzI
Wanachama wa baraza la UN kikaoniPicha: AP

Kiasi cha zaidi ya viongozi 120 watakutana kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa yaliyoko mjini Newyork.Hii ni mara ya kwanza kwa rais wa Marekani Barack Obama kulihutubia baraza hilo.

Kikao hicho cha kilele kinafanyika ikiwa ni siku moja baada ya viongozi 100 wa mataifa na serikali kukutana pamoja kuyajadili masuala ya ongezeko la viwango vya joto ulimwenguni kadhalika jinsi ya kufikia makubaliano mapya yaliyo na azma ya kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya anga.Baadhi ya viongozi walio na misimamo mikali wanatarajiwa kulihutubia baraza hilo la 64 lililo na nchi 192 wanachama.

Wito wa kususia hotuba

UN USA Libyen Muammar al Gaddafi bei der Volversammlung
Kiongozi wa Libya Muammar GaddafiPicha: AP / United Nations

Israel tayari imewashawishi viongozi wa mataifa na serikali pamoja na wajumbe wanaoandamana nao kuisusia hotuba ya Rais wa Iran Mahmoud Ahmedinejad anayeendelea kukanusha kuwa mauaji ya halaiki ya Wayahudi,Holocaust yaliyofanyika wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia hayakutokea.Taarifa zinaeleza kuwa bado haijafahamika iwapo wito huo utaitikiwa au la.Kiongozi wa Libya Muamar Gaddafi anatarajiwa kupanda jukwaani ikiwa ni mara ya kwanza tangu achukue hatamu za uongozi miongo minne iliyopita.Ifahamike kuwa kiongozi huyo hajapewa idhini ya kuipiga hema yake mjini Newyork au katika ardhi ya ubalozi wa Libya wa Marekani.Kauli za viongozi hao zinasubiriwa kwa hamu wakati ambapo viongozi wa ulimwengu watakuwa katika harakati za kutafuta suluhu ya matatizo yanayougubika ulimwengu.Rais Obama ameorodheshwa kulihutubia baraza hilo baada ya Kiongozi wa Libya Muamar Gaddafi.

Hatua za pamoja

UN Generalsekretär Ban Ki Moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: picture-alliance/ dpa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ataufungua rasmi mkutano huo muhimu na kuwasisitizia viongozi wa ulimwengu umuhimu wa kuchukua hatua za pamoja ili kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya anga na umasikini''Huu ndio wakati wa kuchukua hatua.Baadhi yetu wanasema kwamba mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya hali ya anga yatagharimu kiasi kikubwa cha fedha.Wanakosea kinyume chake ndio sahihi.Tutapata athari nyingi zitakazokuwa na gharama kubwa zaidi kama hatutachukua hatua wakati huu.

Hotuba ya Rais Obama inasubiriwa kwa hamu kwani anatarajiwa kutoa ahadi mpya za ushirikiano na Umoja wa Mataifa kinyume na mtangulizi wake George Bush.''Ikiwa tunabadili mitazamo kuendana na wakati.Ikiwa tutaazimia kufanya kazi kwa pamoja bila shaka tutafanikiwa katiia malengo yetu ya pamoja.Hilo litatuwezesha kuwa na ulimwengu ulio salama,safi na unaongunga mkono masuala ya afya na mustakabal wa kizazi kijacho.alisisitiza.

Joto kufukuta

Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva anatarajiwa kuipa msukumo zaidi hoja ya kuyapa nafasi matiafa yanayoinukia kiuchumi.Baraza hilo linatarajiwa kufukuta kwasababu ya masuala nyeti yatakayowasilishwa na viongozi.Waandamanaji nao walioko nje wanaripotiwa kujiandaa kuutangaza msimamo wao dhidi ya uongozi wa Iran.

Urusi nayo inajiandaa kuliwasilisha suala la Afghanistan pamoja na mpango wa nuklia wa Iran unaozua utata.Taarifa za hivi punde zinaeleza kuwa Rais wa Iran Mahmoud Ahmedinejad amemnyooshea mkono wa urafiki Rais Obama wa Marekani na amesisitiza kuwa nchi yake ni rafiki wa la sio adui.

Mwandishi: Thelma Mwadzaya/ AFPE-RTRE

Mhariri:Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi