1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kila mgombea adai kushinda uchaguzi Indonesia

Mjahida10 Julai 2014

Wagombea wote wawili katika uchaguzi wa rais Indonesia amedai ushindi , hali inayozua wasiwasi kisiasa na kisheria, katika taifa hilo lililojitoa kutoka utawala wa kidikteta na kuingia utawala wa kidemokrasia

https://p.dw.com/p/1CZ0s
Mgombea wa Urais Joko "Jokowi" Widodo
Mgombea wa Urais Joko "Jokowi" WidodoPicha: Reuters

Kulingana na matokeo ya awali yaliotolewa, gavana wa Jakarta Joko Widodo ameshinda uchaguzi katika taifa kubwa kwa uchumi Kusini Mashariki mwa bara Asia, kwa takriban asilimia 52 ya kura, lakini mpinzani wake Prabowo Subianto amesema matokeo mengine yanamuonesha yeye kuwa mshindi.

Widodo ni mgombea wa kwanza kutokuwa na mahusiano ya aina yoyote na utawala wa Suharto, dikteta wa zamani kuanzia mwaka wa 1966 hadi mwaka wa 1998.

Akiwahutubia wafuasi wake Widodo amesema huu sio ushindi wa chama chake wala ushindi wa timu yake ya kampeni bali ni ushindi wa watu wa Indonesia.

Mpiga kura akipiga kura yake
Mpiga kura akipiga kura yakePicha: Reuters

Baadaye wafuasi wake walionekana wakishangiria huku wakipeperusha bendera na kuwasha fataki.

"Ninafuraha sana na kuridhika kwa ushindi, natumai matokeo rasmi yatamthibitisha Jakowo kuwa rais wetu mpya." Alisema mmoja wa wafuasi wake Widodo.

Vyombo tofauti vya habari nchini Indonesia vimeripoti matokeo ya kwanza yaliohesabiwa yamempa Joko kati ya asilimia 52 na 53 ya kura, huku Prabowo akijipatia asilimia 47 na 48 ya kura zilizopigwa hii leo.

Bado matokeo rasmi hayajatolewa

Hata hivyo matokeo rasmi ya uchaguzi wa taifa hilo lililo na idadi ya watu milioni 240 na taifa linalojulikana kwa ukubwa wa waumi wa kiislamu, yanatarajiwa kutangazwa Julai 22.

Kwa upande wake rais anayeondoka Susilo Bambang Yudhoyono amezihimiza pande zote mbili kujizuwia na kutokubali wafuasi wao kutangaza ushindi hadi pale tume ya uchaguzi itakapoamua na kumtangaza rasmi mshindi wa uchaguzi huo.

Yudhoyono, ambaye aliwahi kuwa jenerali katika utawala wa dikteta Suharto, alichukua madaraka mwaka wa 2004. alitumikia kipindi cha miaka mitano mara mbili lakini kulingana na katiba ya nchi, hakuweza kugombea tena .

Licha ya Widodo kutokuwa na uzoefu wa siasa za kitaifa anaonekana kuwa mtu anayependwa na wengi anayetaka kuwepo kwa mabadiliko ya kidemokrasia, na hajahusishwa na jeshi linalodaiwa kukumbwa na ufisadi mambo yalioendelea Indonesia kwa miongo kadhaa.

Mgombea wa Urais Prabowo Subianto
Mgombea wa Urais Prabowo SubiantoPicha: Reuters

Prabowo Subianto naye anasemekana kuwa na rekodi isiyoeleweka ya uvunjifu wa haki za binaadamu, lakini anaonekana kuwa mtu mwenye nguvu kama kiongozi.

Takriban watu milioni 190 waliandikishwa na kuwa na haki ya kupiga kura katika uchaguzi wa tatu na tangu kuanguka kwa utawala wa dikteta Suharto mwaka wa 1998. Uchaguzi ulianza saa moja asubuhi katika takriban vituo vyote 480,000 katika maeneo yote nchini humo. Kwa upande wa usalama, polisi 350, 000 na wanajeshi 23,000 walisambazwa kuhakikisha zoezi la uchaguzi na kusesabu kura linafanyika kwa amani.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP/dpa
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman