1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimbunga Irma chatua Florida

Bruce Amani
10 Septemba 2017

Kimbunga Irma kimepiga nyanda za chini za mlolongo wa visiwa vya Florida Keys mapema leo, kikiandamana na upepo mkali wa kilomita 215 kwa saa. Mamia ya maelfu ya wakazi hawana huduma za nguvu za umeme

https://p.dw.com/p/2jg6a
USA Hurrikan Irma in Miami
Picha: Reuters/C. Barria

"Ombeni...Ombeni...kila mtu jimboni Florida”. Gavana Rick Scott aliiambia televisheni ya Fox News. Huku karibu watu 227,000 wakikusanyika katika vituo vya hifadhi ya muda jimboni humo, kimbunga hicho kilipiga visiwa vya Florida Keys kikiandamana na mvua na kukata umeme kwa watu milioni moja kote Florida.

Karibu watu 30,000 waliutii wito wa kuwataka kuhama visiwa vya Keys wakati kimbunga hicho kikikaribia, lakini idadi isiyojulikana ya wakazi walikataa kuondoka, kwa sehemu, kwa sababu kwa wakazi wengi ambao wemeshuhudia vimbunga na kuzoea hali hiyo, kutoondoka wakati kukiwa na hatari ya aina hiyo kunawapa fahari.

Hurrikan Irma | USA, Florida | Miami Beach
Kimbunga Irma kimesababisha uharibifu mkubwaPicha: Reuters/C. Barria

Wakati utabiri wa mkondo wa kimbunga Irma ukionyesha kuwa kitayaathiri majimbo ya Pwani ya Ghuba, watabiri wanaonya kuwa rasi nzima ya Florida – ikiwemo eneo la Miami lenye watu milioni 6 – yapo katika hatari kubwa ya kukumbwa na kimbunga hicho kikubwa Zaidi. Karibu watu milioni 7 katika eneo la Kusini mashariki walionywa kuondoka katika barabara inayopita kimbunga hicho, wakiwemo watu milioni 6.4 jimboni Florida pekee.

Gavana Rick Scott wa Republican ameiambia televisheni ya NBC kuwa amezungumza na Rais Donald Trump, na kila kitu alichoomba kutoka kwa serikali kuu, rais amehakikisha kuwa amepewa.

Amesema mara baada ya kumalizika kimbunga hicho, watahitaji msaada mkubwa. Irma kwa wakati mmoja kilikuwa kimbunga kikubwa Zaidi kuwahi kurekodiwa katika bahari ya Atlantic, kikiwa na upepo wa kasi ya kilomita 300 kwa saa wiki iliyopita. Kilisababisha vifo vya watu 20 katika eneo zima la Caribbean. Watabiri wa hali ya hewa wanasema Irma huenda ikayapiga maeneo ya Tampa-St Petersburg mapema Jumatatu.

Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: John Juma