1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni ziarani Ufaransa

Hamidou, Oumilkher12 Septemba 2008

Mjadala kuhusu kutenganishwa ya dini na yale ya dunia umepamba moto nchini Ufaransa

https://p.dw.com/p/FH9m
Rais Sarkozy na Papa Benedikt wa 16Picha: AP



Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni,Papa Benedikt wa 16 amewasili Paris hii leo kwa ziara ya siku nne.Mara baada ya kuwasili Papa Benedikt wa 16 alikaribishwa katika kasri la Elysée na rais Nicholas Sarkozy na kuzungumza pia na waandishi habari.


Akihutubia huko Elysée hii leo,kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni,ametetea haja ya kutafakariwa upya utaratibu wa kutenganisha mambo ya dini na yale ya dunia.Hapo alikua akijibu hoja za rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy aliyezungumzia kabla ya hapo kuhusu "utaratibu wa maana wa kutenganisha ya dini na ya dunia".


Hoja za Sarkozy zinazusha hofu hasa kwa vile zinatokana na kiongozi wa nchi ambayo tangu mwaka 1905 imekua ikitenganisha kikamilifu mambo ya kanisa na yale ya taifa.


"Itakua kichaa pindi Ufaransa itaachana na mdahalo pamoja na waumini wa dini nyenginezo-ndio maana nnahimiza pawepo utaratibu wa maana wa kutenganisha mambo ya kidini na yale ya kidunia,"amesema rais Sarkozy.


Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni Benedikt wa 16,aliyepokelewa katika uwanja wa ndege wa Orly na rais Sarkozy na mkewe,aliamkiwa pia na waziri mkuu Francois Fillon,mawaziri kadhaa wa serikali na wakaribu  kadhaa wa rais.


Suala la kutenganisha dini na dunia,alianza kulizungumzia kiongozi huyo wa kanisa katoliki tangu alipokua njiani kuelekea Paris.


"Imani ya kidini si siasa na siasa si dini" alisema Papa Benedikt wa 16 mbele ya waandishi habari.


"Hizi ni nyanja mbili zinazobidi kuwa wazi.Ni muhimu kwa mtu kuweza kutekeleza bila ya pingamizi imani yake.Ni dhahiri kwamba kutenganisha ya dini na ya dunia si kinyume na imani ya kidini" ameshadidia kiongozi huyo wa kanisa katoliki ulimwenguni.


Mjadala kuhusu kutenganishwa yadini na ya dunia umepamba moto nchini Ufaransa tangu mwaka jana pale Nicolas Sarkozy alipoonekana kutaka kuuwekea suala la kuuliza utaratibu huo.Wakati ule Nicholas Sarkozy alisema tunanukuu" mtindo wa kutenganishwa ya dini na ya dunia hauwezi kuuitenganisha Ufaransa na mizizi yake ya kikristo.Jaribio lilifanyika lakini limeshindwa" Mwisho wa kumnukuu kiongozi huyo wa ufaransa.


Baada ya kupokelewa Elysée,kiongozi wa kanisa katoliki amepangiwa kuwahutubia wawakilishi wa tamaduni tofauti za dunia katika chuo cha Bernardins,mjini Paris.


Baadae leo usiku Papa Benedikt wa 16 ataongoza misa ya vijana katika kanisa kuu la Notre Dame mjini Paris.


Baada ya misa katika uwanja wa Les Invalides kesho asubuhi,Papa Benedikt wa 16 atakwenda Lourdes kusherehekea miaka 150 tangu Bernadette Soubirou alipomuona bikira Maria.


Asili mia 75 ya wafaransa wanasemekana wamebatizwa lakini wachache tuu ndio wanaojitambulisha na dini ya kikatoliki na asili mia 10 tuu ndio wanaotajikana kua waumini wa kweli.