1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa Taiwan aiambia China vita sio chaguo

Admin.WagnerD10 Oktoba 2022

Kiongozi wa Taiwan Tsai Ing-wen, amesema vitisho vya China vya kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Taiwan sio chaguo kabisa na vitazidi kuzitenganisha pande hizo mbili

https://p.dw.com/p/4I0Zr
Nationalfeiertag in Taiwan I Tsai Ing Wen
Picha: picture alliance/AP/Chiang Ying-ying

 

Akizungumza wakati wa siku ya kitaifa ya Taiwan Jumatatu (10.10.2022), Tsai ameionya China kwamba kisiwa hicho kinachojitawala hakitaachana na mfumo wake wa kidemokrasia na kufananisha hali hiyo na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Tsai alifananisha uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na lengo la China la kuidhibiti Taiwan siku moja hatua ambayo China imeapa kufanya kwa nguvu ikiwa itahitajika.

Tsai aionya China kutoichukulia Taiwan kuwa dhaifu

Tsai ameongeza kusema China haipaswi kufanya makosa ya kuchukulia kimakosa ushindani ndani ya mfumo wa demokrasia ya vyama nchini humo kuwa udhaifu na kujaribu kuwagawanya raia wa Taiwan. Tsai pia amesema anataka kuweka wazi kwa mamlaka ya China kuwa ni kwa kuheshimu tu kujitolea kwa watu wa Taiwan kwa uhuru na demokrasia ndipo kunaweza kuwa na msingi wa kuanza tena mwingiliano mzuri na kisiwa hicho cha Taiwan.

Hotuba ya Tsai pia iliangazia ufanisi wa Taiwan katika kuimarisha usalama wa kijamii kwa wazee na kuendelea kukuza uchumi wake wa teknolojia ya juu licha ya janga la virusi vya corona.

China Xi Jinping
Rais wa China- Xi JinpingPicha: Song Jianhao/HPIC/dpa//picture alliance

Wakati wa hafla hiyo, ndege za kivita na helikopta aina ya Chinook zilizokuwa zikionesha bendera ya Taiwan zilipaa angani huku bendi kutoka shule ya upili ya wasichana ya Taipei ikicheza nyimbo mbali mbali. Wageni mbali mbali ikiwa ni pamoja na rais wa Palau- SAurangel S. Whipps Jr ambaye bendera ya taifa lake yenye rangi ya samawati na manjano ilipeperushwa pembeni ya bendera ya Taiwan, walihudhuria sherehe hiyo.

Licha ya sikukuu hiyo almaarufu 'Double Ten' kuonesha ustahimilivu wa Taiwan kama taifa huru la kisiasa lenye demokrasia iliyostawi na uhuru wa vyombo vya habari, pia inaadhimisha maandamano ya mwaka 1911 ya vikosi vya kijeshi katika mji wa Wuhan nchini China ambayo hatimaye yalisababisha kuangaka kwa utawala wa Qing.

China yasema Taiwan ni sehemu yake

Wakati huohuo, akiongea mjini Beijing, msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China Mao Ning amesema kuwa sababu kuu ya mvutano ulioko kwasasa katika mlango wa bahari wa Taiwan inatokana na msisitizo wa mamlaka ya chama cha Democratic Progressive kuhusu uhuru na kujitenga kwa Taiwan . Mao Ning ameongeza kuwa wako tayari kutengeneza nafasi ya kuunganishwa tena kwa amani lakini hawawezi kutoa nafasi ya uhuru wa Taiwan na shughuli za kujitenga.