1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa upinzani Msumbiji Afonso Dhlakama afariki

4 Mei 2018

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Msumbiji, Afonso Dhlakama, amefariki dunia ghafla akiwa na umri wa miaka 65, akiuawacha mchakato wa mazungumzo ya amani na serikali njia panda.

https://p.dw.com/p/2xAGl
Mozambique Government Renamo peace agreement
Picha: picture-alliance/dpa/A. Silva

Ingawa Rais Filipe Nyusi amesema mpango huo haustahili kuvunjika kwa kifo hicho cha Dhlakama, ambaye alikuwa anatarajiwa kupambana na Rais Nyusi mwaka ujao katika kuwania urais wa nchi hiyo.

Rais Nyusi amemsifu Dhlakama kama raia ambaye siku zote aliweka juhudi zake Msumbiji kuhakikisha kwamba amani inapatikana nchini humo na amesema amehuzunishwa sana na kifo chake. Kiongozi huyo wa waasi wa Vuguvugu la Renamo alipatikana akiwa amefariki katika mji wa Gorongosa ambao ni ngome ya upinzani.

Kwa miaka 39 Dhlakama aliongoza Renamo ambacho kilikuwa kikundi cha waasi kilichopigana katika vita vya miaka 16 dhidi ya chama tawala Frelimo hadi mwaka 1992 kilipoibuka kama chama cha upinzani ambacho kilisalia na wapiaganaji wake waliojihami.

Kifo chake kinaibua maswali kuhusiana na mustakabali wa chama hicho

Tangu mwaka 2013 kiongozi huyo alikuwa mafichoni katika milima ya Gorongosa baada ya mapigano kuzuka tena nchini humo. Lakini katika siku za hivi majuzi Dhlakama alifanya mikutano na Rais Nyusi na alionekana kuwa na jukumu muhimu katika mpango wa amani wa nchi hiyo.

Mosambik Präsident Filipe Jacinto Nyusi
Rais wa Msumbiji Filipe Jacinto NyusiPicha: Imago/Christian Thiel

Kifo chake kinaibua maswali kuhusiana na mustakabali wa chama hicho alichokiongoza kwa karibu miongo minne. Haijulikani kwa sasa nani atakayeendelea na mazungumzo ya amani na serikali na kipi kitakachofanyika kuhusu wapiganaji wa chama hicho waliojihami na ambao bado wapo katika milima ya Gorongosa.

Silvestre Baessa ambaye ni mtaalam wa utawala bora kutoka Msumbiji ameiambia DW, "hiki kifo kina athari kubwa katika mchakato wa siasa za kitaifa. Kwanza kabisa tumepoteza mtu muhimu katika mazungumzo ya amani. Katika miaka michache iliyopita imebainika kwamba juhudi za rais wa Renamo kwa makubaliano ya amani yaliyotiwa saini ni kutokana na dhamira yake," alisema Baessa. "Sidhani kwamba Dhlakama alifikiria kuhusu mrithi wake ambaye angefuatilia suala hili. Nafikiri hii itakuwa changamoto kubwa. Rais Filipe Nyusi atahisi kutokuwepo kwa Dhlakama kwa sababu alikuwa rafiki yake mkuu katika mazungumzo ya amani," aliongeza mtaalam huyo.

Kwa sasa bunge linajadili mabadiliko ya katiba Msumbiji

Desemba mwaka 2016, Dhlakama aliwashangaza wengi kwa kutangaza kusitishwa kwa mapigano na serikali katika hatua ya kwanza kuu ya uwezekano wa kutiwa saini kwa mkataba rasmi wa amani. Mara ya mwisho Rais Filipe Nyusi kukutana na Dhlakama ilikuwa ni mwezi Februari mjini Gorongosa ambapo walijadili masuala ya kuacha matumizi ya silaha na mapatano, na walionekana kukubaliana kuhusu mabadiliko ya katiba.

Dokument  Friedensvereinbarung zwischen Mosambikregierung und Renamo
Mkataba wa amani uliotiwa saini 1992 kati ya serikali ya Msumbiji na RENAMOPicha: DW/R.Belincanta

Mabadiliko ambayo kwa sasa yanajadiliwa bungeni yatawakubalia wapiga kura wawachague moja kwa moja magavana wa mikoa ambao kwa sasa wanateuliwa na rais. Lakini matakwa ya Renamo ya kujumuishwa kwa wafuasi wake katika polisi na jeshi inasalia kuwa hoja muhimu katika majadiliano.

Msumbiji itaandaa uchaguzi wa rais, bunge na mikoa Oktoba mwaka 2019 wakati ambapo waandalizi wanasema chama cha Renamo kimeongeza idadi ya wafuasi wake katika siku za hivi majuzi.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef