1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa zamani wa Urusi Yeltsin afariki dunia.

Mohammed Abdul-Rahman23 Aprili 2007

Anatajwa kuwa muasisi wa demokrasia na mageuzi ya kiuchumi nchini mwake.

https://p.dw.com/p/CB4V
Boris Yeltsin akiangalia mechi ya tennis ya kombe la Davis mjini Moscow Desemba mwaka jana.
Boris Yeltsin akiangalia mechi ya tennis ya kombe la Davis mjini Moscow Desemba mwaka jana.Picha: AP

Aliyekua Rais wa Urusi Boris Yelstin amefariki dunia. Yeltsin atakumbukwa kuwa mwanasiasa aliyetoa msukumo ulioleta demokrasia na uchumi unaotegemea masoko katika taifa hilo kubwa lililokua zamani la kikoministi.

Ni sauti ya Marehemu Boris Yeltsin katika mkutano na waandishi habari,wakati wa ziara ya rais wa zamani wa Makani Bill Clinton mjini Moscow Aprili 1996.

Msemaji wa Ikulu ya Urusi-Kremlin Alexander Smirnov aliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba kiongozi huyo wa zamani amefariki dunia, lakini hakutoa maelezo zaidi juu ya sababu za kifo chake. Hata hivyo shirika la habari la Interfax lilizinukuu duru za hospitali zikisema alifariki kutokana na matatizo ya moyo.

Licha ya kwamba Yeltsin alikua kivutio kikubwa nchi za nje, lakini wengi Urusi kwenyewe watamkumbuka kwa kuwa chanzo cha kuanguka taratibu kwa taifa hilo kubwa.

Yeltsin alikua ni kiongozi aliyezusha mabishano wakati wote, akichomoza kama mwanasiasa wa enzi ya ukoministi aliyejitolea kupambana na rushwa, lakini akashindwa hatimae kuzuwia ubadhirifu wa mali , hasa wakati wa zoezi la ubinafsishaji wa viwanda vya dola.

Sambamba na hayo alikua rais wa kwanza aliyechaguliwa kidemokrasi na kuitawala Urusi kwa muda wa miaka tisa, kabla ya kumuachia madaraka rais wa sasa Vladimir Putin aliyemteuwa na kumpigia debe kuwa mrithi wake.

Miongoni mwa shutuma kali alizopambana nazo ni msimamo wake wa kuiingiza Urusi vitani dhidi ya waasi katika jimbo la Chechnya, waliokua wakipigania kujitenga jimbo hilo—vita ambavyo viliitia aibu Urusi na kulazimika kujiondoa.

Makubaliano ya amani baina ya serikali kuu mjini Moscow na waasi wa Chechnya ambapo iliafikiwa kwamba watapewa nafasi ya kujiamulia hatima yao, yalivunjwa , wakati Putin alipoingia madarakani na kuanza tena mapigano yaliosababisha jeshi la Urusi kulidhibiti tena jimbo hilo.

Boris Yeltsin aliyesumbuliwa na matatizo kadhaa ya moyo wakati alipokua madarakani alijiuzulu mnamo mkesha wa mwaka mpya 1999, miezi michache kabla ya kipindi chake cha utawala kumalizika.

Jeltsin alizaliwa februari 1, 1931 katika kijiji cha Butka kwenye eneo la Ural. !961 akiwa mhandisi wa ujenzi alijiunga na chama cha kikoministi na 1975 akachaguzliwa mkuu wa chama cha kikoministi huko Swerdlowsk mji unaojulikana leo kama Jekaterinburg. Kiongozi mkuu wa chama Michail Gorbachov akamhamishia Moscow wakati wa kuanza kwa sera yake ya mageuzi PERESTROIKA na kwa kiongozi wa chama mjini humo.

Alianza hatua zake za kupigania mageuzi 1987 na 1990 akakihama chama cha kikoministi. Alisimama kidete kuzuwia jaribio la mapinduzi dhidi ya kiongozi mkuu wa taifa Gorbachov Juni 1991, lakini huo ukawa manzo wa kusambaratika iliokua Soviet Union na kumlazimisha Gorbachov kujiuzulu. Yeltsin akadhibiti hatamu kamili za uongozi wa Urusi, baada ya Ukraine na Belaruss kujitoa Desemba 1991 katika umoja wa Kisovieti.

Kiongozi huyo wa zamani wa Urusi amefariki akiwa na umri wa miaka 76.