1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kipi chanzo cha mzozo wa Pakistan na Afghanistan?

Thelma Mwadzaya30 Julai 2010

Kashfa ya kuvuja kwa hati za siri za kijeshi kwenye mtandao wa WikiLeaks imezua masuala mapya hususan katika vita na mzozo kati ya Afghanistan na Pakistan.Jee ujumbe wa vikosi vya kigeni ulioko Afghanistan umeshindwa?

https://p.dw.com/p/OXyQ
Nembo ya Taliban-Pakistan

Wasiwasi umezuka kuwa tukio hilo la hati kuvuja huenda likayahatarisha maisha ya raia  wa kawaida.Yote hayo yanajitokeza wakati  ambapo Waziri  Mkuu wa Uingereza David Cameron amekamilisha ziara yake siku mbili iliyompeleka India.Katika ziara yake ya kwanza  ya Asia,kiongozi huyo pamoja  na mwenyeji wake India wameitolea wito Pakistan  kupambana na  wapiganaji wa kundi la Taleban.Jee,kipi  chanzo cha mzozo wa Afghanistan na Pakistan?

Wakazi  milioni 22

 Eneo la kaskazini  magharibi mwa Pakistan lina  kiasi cha  wakazi milioni 22 wengi wao  wa kabila la Pashtun.Inaaminika kuwa maeneo hayo ndiyo maficho ya viongozi wakuu  wa mtandao wa kigaidi,Mullah Omar  na Osama  bin Laden.Wapiganaji wa  kundi la Taleban wameyaimarisha mashambulio yao wanayoyaendesha kutokea eneo hilo la Pakistan.Harakati za wapiganaji  hao  zinauathiri mchakato mzima wa kutafuta amani Afghanistan na pia kutisha kuuvuruga uongozi wa Pakistan.Pakistan  na  Afghanistan zimekuwa zikilaumiana kwasababu ya hali ya usalama katika eneo hilo.Rahimullah Samandar,mchambuzi  wa masuala  ya  uhusiano kati ya  Afghanistan na Pakistan na mwandishi anaamini kuwa,''  

Uhusiano kati ya Afghanistan na Pakistan unatatizwa na kutoaminiana.Mazungumzo rasmi ya  ushirikiano yamekuwa yakiendelea ila hali halisi inaonyesha kuwa harakati hizo hazipo,''jambo linalochangia katika hali jumla ya usalama.       

Osama Bin Laden Flash-Galerie
Osama bin Laden:Inaaminika amejificha kaskazini mwa PakistanPicha: AP

Tatizo hilo lilianza wakati wa  ukoloni wakati mipaka ya eneo  hilo ilipochorwa na Uingereza.Kwa upande wake Afghanistan ilikataa katakata kuitambua mipaka  hiyo na ikadai kuwa azma ya hatua  hiyo ni kuliteka eneo la waPashtun.Kufuatia hilo,wakazi hao wa Kipashtun waliamua kupambana na Pakistan ili kulinyakua eneo lao.Chini ya uongozi wa Zia-ul-Haq,madrassa nyingi zilijengwa katika eneo hilo ili  kuyaendeleza maadili ya utawala wa Kiislamu.

Ni katika madrassa hizo,vijana walifunzwa itikadi kali.Mmoja wa vijana   hao ni  Osama bin  Laden.

Mwanya  wa mashambulio

Uingereza iliutumia mwanya huo wa kushambuliana kuichokoza Urusi,kuivuruga Pakistan iliyoiona kuwa kitisho na kwa upande mwengine kuimaliza nguvu serikali ya Afghanistan yenyewe.Pakistan ilizibadili mbinu zake na kuanza kuwatumia  vijana waliosoma kwenye madrassa waliojazwa itikadi kali badala  ya viongozi wa kitamaduni.Makundi ya Mujahideen ya Afghanistan yaliamua kujisimamia  yenyewe ili kuivutia Pakistan.Hata hivyo yalizongwa  na mivutano  ya ndani na baada  ya hapo kundi la  Taleban  lilizinduliwa na likachukua hatamu ya uongozi wa  Afghanistan.Pakistan na Saudi Arabia  pekee ndizo zilizoutambua utawala wa Taleban.

Kufuatia shambulio la mabomu la tarehe  11 mwezi wa Septemba mwaka 2001,Marekani iliamua kuivamia Afghanistan kwa lengo la kupambana na  wapiganaji wa Taleban na magaidi wa  Al-Qaeda.Kulingana na Sayfuddin  Sayhun,mchambuzi wa masuala ya kisiasa  na mhadhiri ,njia  ya  kufuata ni moja tu ya,''Kupata suluhu ya kisiasa.Wakazi  wa eneo hilo wanahitaji suluhu  ya  kudumu itakayowawezesha kuwa  na miradi ya maendeleo,elimu na kuishi  maisha ya kawaida kwa jumla.Bila ya hayo hakuna amani yoyote itakayopatikana,''alieleza.



Indien David Cameron Manmohan Singh
Manmohan Singh na David Cameron-wakiwa New Delhi, IndiaPicha: AP

Kauli hizo zimeungwa  mkono na  Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron aliyeihitimisha Alhamisi usiku ziara  yake ya India.Katika tamko  lao la pamoja,viongozi wa India na Uingereza  wameitolea wito  Pakistan kupambana na uasi katika eneo hilo unaozivuruga harakati  za kutafuta amani.

Mwandishi:Thelma  Mwadzaya-ZPR-Shamel Ratbil

Mhariri:Josephat Charo