1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kishindo cha Brexit Magazetini

Oumilkheir Hamidou
10 Julai 2018

Kujiuzulu mawaziri wawili kutokana na mvutano kuhusu sera ya Brexit na uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi za Umoja wa Ulaya na China kwa upande mmoja na ule pamoja na Marekani. kwa upande wa pili

https://p.dw.com/p/3182Q
London Unterhaus berät über Brexit
Picha: picture-alliance/AP/Parliamentary Recording Unit

Tunaanzia njia panda inayoiunganisha Uingereza na Umoja wa Uaya. Gazeti la "Rheinpfalz" linazungumzia kuhusu hatari ya kuvunjika serikali ya waziri mkuu Theresa May. Gazeti linaendelea kuandika:" Pumzi zimeanza kumuishia waziri mkuu Theresa May. Viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels lakini wanahisi hakuna sababu ya kufurahikia. Kwasababu majadiliano, na hilo limebainika, huleta tija tu, yanapoendeshwa na viongozi imara. Serikali ya Uingereza  lakini inazozana  kwa hivyo imedhoofika. Na hali hiyo haiashirii mema."

Kishindo cha Theresa May ni kikubwa zaidi

Gazeti la "Oberhessische Presse" linalinganisha hali iliyokuwa imemzonga kansela wa Ujerumani Angela Merkel na hii inayomsumbuwa waziri mkuu wa Uingereza Theresa May. Gazeti linaandika:" Ukizingatia hali ya mambo humu nchini unaweza kusema mtihani uliokuwepo umeshamalizika, mnamo wakati ambapo Theresa May anatapa tapa vibaya sana na kujaribu kuyanusuru maisha yake ya kisiasa.Tofauti kubwa inakutikana katika sura yenyewe ya mizozo: Nchini Ujerumani ulikuwepo na ungalipo bado mvutano uliokuzwa kuhusu sera ya wakimbizi. Nchini Uingereza hali ni nyengine kabisa, mzozo ni mkubwa zaidi, unahusiana na masharti ya maisha ambayo kila raia wa Uingereza atalazimika kukabiliana nayo kwa namna moja au nyengine pale nchi yao itakapojitoa katika Umoja wa ulaya."

Zimwi likujualo halikuli likakumaliza

 Na hatimae wahariri wa magazeti wametupia jicho uhusiano wa kibiashara  kwa upande mmoja kati ya nchi za Umoja wa ulaya na Marekani na kwa upande wa pili kati ya nchi hizo na jamhuri ya Umma wa china. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaandika: "Katika wakati ambapo mshirika wa jadi Amerika anatishia kuzitoza nchi za umoja wa ulaya ushuru ziada na kutishia kuziadhibu, Jamhuri ya umma wa China inamimina vitega uchumi na kurahisisha shughuli za kibiashara. Mbinu za Mashariki ya mbali zinapokelewa kwa moyo mkunjufu na viongozi wa nchi za Ulaya wanaohisi wamefedheheshwa. Kimoja watu wanabidi wakijue. China haitoi kitu bure. Kwa miaka sasa viongozi wa mjini Peking wanaendeleza sera kali za kiuchumi sera zinazofuata mwongozo mmoja tu:"Kinachoruhusiwa ni kile tu kitakacho kuwa na faida na china". Zaidi ya hayo linazuka suala la haki za binaadam.Takriban katika kila suala linalohusiana na haki na madili, Marekani iko karibu zaidi na Umoja wa ulaya kuliko China. Na ukweli huo hata Donald Trump hawezi kuubadilisha."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu