1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kishindo kiko mkiani katika Ligue 1

18 Mei 2017

Kishindo katika Ligue 1 ya Ufaransa kiko katika chini ya jedwali huku raundi ya mwisho ya mechi ikielekea kuchezwa mnamo wikendi.

https://p.dw.com/p/2dCFV
Alexandre Lacazette Olympique Lyonnais
Mshambuliaji wa Lyon Alexandre LacazettePicha: Getty Images/AFP/J. Pachoud

Nancy, Bastia, Lorient, Caen na Dijon ni timu zitakazoelekea katika mechi ya mwisho ya msimu zikiwa bado hazifahamu mustakabali wao katika ligi hiyo kuu ya Ufaransa.

Bado kuna matumaini hata kwa timu iliyo mkiani Nancy, ambayo inatakiwa kutoa ushindi dhidi ya Saint-Etienne na matokeo ya mechi za wapinzani wao yaende upande wao. Iwapo mambo yatakuwa hivyo basi Nancy watamaliza wakiwa katika nafasi ya kumi na nane ambayo ndiyo nafasi inayotoa nafasi ya kucheza mechi ya mchujo ya kuwania iwapo timu inasalia katika ligi hiyo kuu ya Ufaransa. Mechi hiyo itakuwa dhidi ya timu iliyomaliza katika nafasi ya tatu katika ligi ya daraja la pili. Mechi hizo za mchujo nchini Ufaransa ndio zinachezwa kwa mara ya kwanza msimu huu na mfumo huo sasa unachukua nafasi ya ule mfumo wa zamani wa timu tatu kushuka daraja na tatu kupanda.

Ligue 1 ina bingwa mpya pia kwa kuwa Monaco walilinyakua taji la ubingwa usiku wa Jumatano, hilo likiwa ni taji lao la kwanza tangu mwaka 2000. Paris Saint Germain wamejihakikishia nafasi ya pili na Nice wakaichukua nafasi ya tatu na ya mwisho ya moja kwa moja kushiriki ligi ya vilabu bingwa Ulaya.

Lyon itakayokuwa inacheza na Nice Jumamosi, imeshaipata nafasi ya nne tayari na kujikatia tiketi ya kushiriki ligi ya Ulaya msimu ujao. Chini yao lakini Bordeaux wanapambana na Marseille kuwania nafasi ya pili ya kushiriki moja kwa moja ligi ya Ulaya. Marseille kwa sasa wanaishikilia nafasi ya tano katika msimamo na watakuwa wanacheza na Bastia katika mechi ya mwisho nao Bordeaux wawe na kibarua dhidi ya Lorient.

Mwandishi: Jacob Safari/APE

Mhariri: Bruce Amani