1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kitengo cha uhamiaji Ujerumani chakumbwa na kashfa ya visa

Daniel Gakuba
23 Mei 2018

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Horst Seehofer ameizuia ofisi ya uhamiaji mjini Bremen kushughulikia kesi za hifadhi nchini, baada ya shutuma kwamba iliwapa hifadhi mamia ya wahamiaji ambao hawakutimiza vigezo.

https://p.dw.com/p/2yCzH
Deutschland Bundesinnenminister Seehofer besucht BAMF
Horst Seehofer (kulia) Waziri wa mambo ya ndani wa Shirikisho la UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa/D. Karmann

Hatua hiyo isiyo ya kawaida imechukuliwa baada ya uchunguzi wa ndani juu ya maombi 4,568 ya hifadhi kudhihirisha kwamba maafisa wa uhamiaji katika ofisi ya Bremen walikwenda kinyume na utaratibu unaokubalika, tena kwa makusudi. Kutokana na kashfa hiyo, waziri wa mambo ya ndani wa shirikisho la Ujerumani Horst Seehofer, amesema imani kwa ofisi hiyo ya Bremen imeharibika vibaya.

Ripoti ya waandeshamashitaka iliyotolewa mwezi uliopita wa Aprili, ilisema kesi zipatazo 1,200 za waomba hifadhi, hususan zile za watu kutoka jamii ya Wayazidi ambao ni wachache nchini Iraq, zilikubaliwa kimakosa kati ya mwaka 2013 na 2016.

Wakimbizi Takriban milioni 1.6 wameingia nchini Ujerumani tangu mwaka 2014, wengi wao wakiwa ni kutoka eneo la Mashariki ya Kati. Mmiminiko huo wa wakimbizi umekuwa suala lenye utata mkubwa katika siasa za Ujerumani, ambalo limesaidia kuimarika kwa chama chenye sera kali za kizalendo na chenye kuhamasisha hisia za umma cha Mbadala kwa Ujerumani, AfD.

Uchunguzi wa kina kuendelea

Deutschland - Bamf-Chefin Jutta Cordt
Mkuu wa Kitengo cha Uhamiaji cha Ujerumani, Jutta Cordt ambaye anakabiliwa na shinikizoPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrcenka

Akizungumza baada ya kikao cha mawaziri kilichogubikwa na kashfa hiyo, mkuu wa kitengo cha uhamiaji ngazi ya shirikisho la Ujerumani (BAMF) Jutta Cordt amesema uchunguzi unaendelea kuhusu maamuzi yote ya hifadhi yaliyofanyika katika ofisi ya Bremen.

''Tunaendelea kuchunguza maombi yote yaliyokubaliwa kupitia ofisi ya Bremen, ambayo ni takriban 18,000 hivi, ukijumuisha maamuzi yote yaliyofanywa kuanzia mwaka 2000'' Amesema Cordt.

Tangazo la wizara ya mambo ya ndani imethibitisha kuwa waziri Seehofer atashiriki katika kikao cha dharura cha kamati ya mambo ya ndani katika bunge la shirikisho mjini Berlin Jumanne wiki ijayo, ambacho huenda kikahudhuriwa pia na Bi Jutta Cordt ambaye anakabiliwa na shinikizo kubwa.

AfD yaja juu

Georg Pazderski ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama cha AfD amezungumza na vyombo vya habari, akasema haamini kwamba waziri wa mambo ya ndani anafanya vya kutosha kuiwajibisha ofisi ya uhamiaji ya Bremen, akisema anataka kila kitu kiwekwe wazi.

Flüchtlinge Landroute Türkei Griechenland
Mmiminiko wa wakimbizi kutoka Mashariki yan Kati umekuwa sumu katika siasa za UjerumaniPicha: picture-alliance/AP Photo/T. Starvakis

Pazderski amesema na hapa namnukuu, ''Tunavyoona kashfa hii inazidi kupanuka, na mimi nadhani kuundwa kwa kamati ya uchunguzi litakuwa jambo jema.'' mwisho wa kumnukuu.

Taarifa zimeeleza kuwa ofisi ya mwendeshamashitaka wa serikali wa Nuremberg na Fuerth inachunguza tuhuma dhidi ya afisa huyo, zinazomshuku kurahisisha kwa njia zisizo halali, utoaji wa ruhusa ya kuishi nchini Ujerumani.

Aliyekuwa mkurugenzi wa kitengo cha uhamiaji ngazi ya shirikisho kati ya mwaka 2015 na 2016 Frank-Juergen Weise, ameliambia gazeti la Redaktionsnetwerk Deutschland, kwamba tatizo kubwa katika kitengo hicho ni la raslimali na miundombinu. Amesema wanapokea idadi kubwa ya maombi ya hifadhi, huku ikiwa na mfumo duni wa komputa, na ushirikiano wa idara ambao haukuwianishwa vyema.

 

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae,rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga