1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kizungumkuti cha serikali mpya nchini Libya

3 Machi 2022

Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake juu ya ripoti kwamba kura iliyopigwa katika bunge la Libya kuidhinisha serikali mpya nchini humo haikutimiza masharti yanayokubalika kisheria.

https://p.dw.com/p/47wFr
Libyen | Fathi Bashagha kandidiert als Präsident
Picha: Hazem Turkia/AA/picture alliance

Matamshi hayo yametolewa wakati kuna hofu ya kuzuka migawanyiko mipya nchini Libya katika mpambano wa kuwania madaraka. 

Katika taarifa kwa njia ya baruapepe msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuna ripoti zinazoonesha kwamba kura iliyopigwa bungeni nchini Libya siku ya Jumanne kuidhinisha serikali mpya haikukidhi masharti ya uwazi  na kanuni za kibunge.

Kuna madai pia zilitumika njia za ubabe na vitisho dhidi ya wabunge kabla ya zoezi la kupiga kura kufanyika.

Bunge lapanga kumwapisha waziri mkuu mpya

Libyen | Parlament in Sirte
Picha: AA/picture alliance

Bunge la Libya linapanga hivi leo kumwapisha Fathi Bashagha kuwa waziri mkuu mpya huku waziri mkuu aliye madarakani Abdulhamid al-Dbeibah akikataa katakata kukabidhi hatamu za uongozi. Pande zote mbili za serikali inayotarajiwa kuapishwa na ile iliyo madarakani zina ushawishi fulani wa kijeshi nchini Libya

Mivutano yao kuhusu nani anapaswa kuiongoza nchi hiyo tayari inatishia kuzusha mapigano mapya au kulirejesha taifa hilo kwenye migawanyiko ya kimaeneo.

Umoja wa Mataifa kwa upande wake umechagua kurejesha shinikizo la kufanyika uchaguzi nchini humo ukisema hivi karibuni unatarajia kuzialika pande mbili zinazovutana yaan bunge na Baraza Tawala la Libya kwa ajili ya mazungumzo.

Msimamo wa jumuiya ya kimataifa utakuwa muhumi katika siku zinazokuja kwenye kuamua  juu ya mvutanowa udhibiti wa serikali ya Libya ambao wachambuzi wanatahadharisha  huenda utazusha vita mpya au kuleta mpasuko mwingine baina ya pande hasimu zinazowania madaraka.

Hatma ya serikali mpya bado kitanzini

Haijafahamika hadi sasa iwapo serikali mpya chini ya Fathi Bashagha anayetazamiwa kuwa waziri mkuu itaapishwa hii leo au la.

Ägypten Kairo | Libyscher Premierminister Abdul Hamid Mohammed Dbeibah
Waziri Mkuu wa Libya Abdul-Hamid DbeibahPicha: Hazem Ahmed/AP Photo/picture alliance

Shaka shaka hizo zinafuatia taarifa iliyotolewa leo kwamba vikosi venye mafungamano na waziri mkuu aliye madarakani vimewakamata mawaziri wawili wa serikali mpya inayotarajiwa kuapishwa. Taarifa hizo ni kulingana na vyanzo viwili vilivyo karibu na waziri mkuu mteule Fathi Bashagha.

Mawaziri hao wa masuala ya mambo ya kigeni na utamaduni walikamatwa huko Misrata wakiwa njiani kwenda mji wa Tobruk wakitumia magari.

Walitumia njia hiyo baada ya hapo jana waziri mkuu mteule Bashagha kusema waziri mkuu Dbeibah aliamuru kufungwa kwa anga yote nchini Libya kwa lengo la kuwazuia mawaziri wapya kusafiri kwenda mji wa Tobruk, yaliko makao makuu ya Bunge ili kuapishwa.

Msemaji wa serikali ya Dbeibah hakupatikana kuzungumzia madai hayo.

Bunge lashikilia msimamo serikali ya Dbeibah iondoke

Libyen nach dem Tode Gaddafis Flash-Galerie
Picha: dapd

Bunge la Libya liliamua kuingilia kati na kutwaa hatamu za uongozi wa serikali baada ya kushindakana kufanyika uchaguzi uliopangwa Disemba iliyopita.

Chombo hicho kinasema serikali ya Dbeibah iliyoingia madarakani mwaka mmoja uliopita kwa dhima ya kuandaa uchaguzi wa kidemokrasia ambao ulishindikana imemaliza muhula wake na haipaswi kuendelea kubakia madarakani.

Bunge linataka serikali mpya ya waziri mkuu Bashagha ianze kazi mara moja na kisha iandae kura ya maoni ya katiba na tarehe mpya ya uchaguzi mwaka 2023. Lakini Dbeibah anapinga msimamo huo akisema anataka kuandaa uchaguzi mwingine mnamo mwezi Juni.