1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kocha wa Barca ana furaha kuwa mwalimu wa Messi

Bruce Amani
17 Julai 2017

Kocha mpya wa Barcelona Ernesto Valverde amekiri kuwa ana furaha kwamba hatoweza tena kucheza dhidi ya mchezaji mahiri zaidi duniani Lionel Messi. Amezungumza leo kwa mara ya kwanza na wahabari

https://p.dw.com/p/2gg1q
Ernesto Valverde - neuen Trainers des FC Barcelona
Picha: picture-alliance/dpa/EFE/L. Tejido

Akizungumza katika kikao chake cha kwanza cha waandishi wa habari tangu alipochukua usukani, kocha huyo wa zamani wa Athletic Bilbao ameulizwa anajihisi vipi kuwa mwalimu wa Messi "ni hisia ya furaha kuwa na Messi. wakati ukiwa kwenye benchi kama mpinzani inakubidi kutafakari cha kufanya ili kumzuia na wakati mwingine unawakosa wachezaji wa kumdhibiti. kwa sasa, nnachojaribu kufanya ni kuzoea namna yeye na wenzake wanavyofanya mazoezi".

Valvarde amepuuza wazo la kuwasajili wachezaji wapya akisema kuwa tayari wachezaji bora zaidi ni wale alionao katika timu yake kwa sasa "klabu hufanya bidii kuwa na timu bora lakini wazo langu, zaidi ya vyote, kawaida huwa ni kufanya kazi na nilichonacho. ndivyo nnavyofanya kazi na wachezaji nilionao hapa. Tunaifahamu klabu yetu na wachezaji wengi wanataka kuja. tunataka kuwa na wachezaji bora duniani na hakika tunao sasa".

Barca watasafiri kwenda Marekani Jumatano kama sehemu ya ziara ya maandalizi ya kabla ya msimu na watakutana na watani wao wa jadi Real Madrid katika mchuano wa kirafiki jijini Miami mnamo Julai 29 katika classico ya kwanza kuchezwa nje ya Uhispania kwa miaka 35

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Yusuf Saumu