1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kocha wa Ujerumani Joachim Loew bado akuna kichwa

2 Juni 2014

Kocha wa Ujerumani Joachim Loew akiri kuwa anakabiliwa na matatizo kadha baada ya Ujerumani kushindwa kung'ara mbele ya Cameroon katika mchezo wa majaribio jana(01.06.2014). Atangaza kikosi chake cha wachezaji 23.

https://p.dw.com/p/1CAh0
Fußball Freundschaftsspiel Deutschland Kamerun 01.06.2014
Cameroon walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia Eto'oPicha: picture-alliance/dpa

Kocha Joachim Loew wa timu ya taifa ya Ujerumani amekiri kuwa anakabiliwa na matatizo kadha ya kuyatatua baada ya Ujerumani kushindwa kung'ara katika mchezo wao dhidi ya Cameroon ambao umemalizika kwa sare ya mabao 2-2 wakati akipunguza kikosi hicho hadi wachezaji 23 leo Jumatatu.

Kocha Joachim Loew anakwenda Brazil bila wachezaji chipukizi Kevin Volland kutoka Hoffenheim na Shkodran Mustafi pamoja na mlinzi wa kushoto Marcel Schmelzer ambaye bado ana maumivu ya goti, ambapo wamezaji hao wamekatwa kutoka orodha ya wachezaji 26 waliokuwapo hapo kabla katika kambi ya mazowezi.

Fußball Freundschaftsspiel Deutschland Kamerun 01.06.2014
Samuel Eto'o akishangiria bao lakePicha: picture-alliance/dpa

Wachezaji 23 wa kikosi cha taifa

Loew hata hivyo amemjumuisha katika kikosi hicho mlinzi wa kushoto wa Borussia Dortmund Erik Durm , ambaye baada ya kucheza mchezo wake wa kwanza jana Jumapili na timu ya taifa dhidi ya Cameroon ,na pia amemjumuisha mlinda mlango namba moja Manuel Neuer na nahodha Philipp Lahm, ambao bado wanakabiliwa na maumivu.

Ujerumani inaikaribisha Armenia katika mchezo wa mwisho wa kujipima nguvu siku ya Ijumaa usiku mjini Mainz kabla ya kusafiri kwenda Brazil siku inayofuata, lakini kocha Loew anasema marekebisho yanapaswa kufanyika haraka iwezekanavyo.

Fußball Freundschaftsspiel Deutschland Kamerun 01.06.2014
Samuel Eto'oPicha: JOHN MACDOUGALL/AFP/Getty Images

Ujerumani inataanza kampeni yake ya kuwania ubingwa wa kombe la dunia dhidi ya Ureno mjini Salvador Juni 16 na pia inakabiliwa na changamoto kutoka Marekani na Ghana katika kundi lake la G.

Mashabiki walioshuhudia pambano la jana wana wasi wasi na kikosi chao, baada ya kutoka sare bila kuonesha mchezo wa matumaini na Cameroon jana mjini Gladbach.

Dirk Hartmann mmoja kati ya mashabiki walioshuhudia pambano hilo mjini Gladbach alikuwa na hisia hizi baada ya mchezo huo.

"Siamini kuwa tunaweza kufika mbali mwaka huu. Bahati mbaya , katika miaka kumi na mbili iliyopita nilikuwa na hisia nzuri. Kwa sasa sina."

Matarajio ya juu

Kwa upande mwingine kocha wa Cameroon Mjerumani Volker Finke amesema mshambuliaji nyota wa kikosi hicho Samuel Eto'o amekipa kikosi hicho msukumu muhimu kwa ajili ya fainali za kombe la dunia kwa kuonesha mchezo safi katika sare hiyo ya mabao 2-2 dhidi ya Ujerumani jana.

Deutschland Fußball Manuel Neuer Bayern München Schulterverletzung
Mlinda mlango namba moja wa Ujerumani Manuel NeuerPicha: Getty Images

Mshambuliaji huyo wa Cameroon mwenye umri wa miaka 33 ambaye ni nahodha wa Simba hao wa nyika amekuwa na maumivu ya paja wakati wa matayarisho katika kambi yao iliyokuwa nchini Austria.

Lakini mshambuliaji huyo nyota , ameonesha mchezo safi kwa muda wa dakika 92 dhidi ya Ujerumani jana Jumapili, ambapo kikosi hicho kilipata bao lake la kusawazisha kupitia Eric Maxim Choupo-Moting ambaye alisema baadaye kuwa lengo la Cameroon ni kupata nafasi ya kusonga mbele kutoka katika kundi lao.

"Kwasababu Cameroon kawa kawaida ni moja kati ya mataifa makubwa katika soka barani Afrika, lengo letu ni kucheza vizuri na kuweza kuibuka katika kundi letu moja ya timu zitakazosonga mbele katika duru nyingine."

Simba hao wa nyika Cameroon watacheza mchezo wao wa mwisho wa majaribio dhidi ya Moldova mjini Yaounde siku ya Jumamosi. Pambano lao la ufunguzi katika fainali za kombe la dunia litakuwa dhidi ya Mexico Juni 13 katika kundi A ambapo pia wanakutana na Brazil na Croatia.

Fußball Freundschaftsspiel Deutschland Kamerun 01.06.2014
Eric Maxim Choupo Moting wa CameroonPicha: Simon Hofmann/Bongarts/Getty Images

Rooney ana mzigo mkubwa wa matarajio

Wachezaji wachache wa Uingereza watakuwa na mbinyo mkali kuliko ilivyo kwa mshambuliaji nyota Wayne Rooney wakati kikosi hicho cha kocha Roy Hodgson kitakapokuwa mjini Miami kwa matayarisho ya kombe la dunia.

Mbinyo kila mara unaongezeka kwa mshambuliaji huyo kuonesha uwezo wake kwa Uingereza ambao umempatia mkataba mnono katika hostoria ya Manchester United msimu uliopita.

Rooney amepachika wavuni mabao 38 katika michezo 89 aliyoshiriki akiwa na timu hiyo ya taifa. Lakini hivi karibuni ameshindwa kutikisa nyavu katika michezo minne ya kimataifa aliyoshiriki na timu hiyo.

Wayne Rooney
Wayne RooneyPicha: picture alliance / empics

Ndio sababu taifa hilo lina wasi wasi mkubwa na nyota huyo kuweza kuonesha umahiri wake wiki mbili kabla ya kuanza kwa fainali hizo nchini Brazil .

Kocha wa England Roy Hodgson hata hivyo , anajaribu kuhakikisha kuwa Rooney habebi mzigo mkubwa wa matarajio katika nchi hiyo ambayo haijashindaq kombe hilo tangu mwaka 1966 ama hata kufikia nusu fainali katika muda wa miaka 24 iliyopita.

Kocha wa Japan Alberto Zaccheroni anaongeza mbinyo kwa wachezaji wake kufikia viwango vinavyohitajika kabla ya fainali hizo za kombe la dunia kwa wachezaji wake nyota kama Shinji Kagawa na Keisuke Honda , wakati timu hiyo ikikabiliwa na mchezo muhimu wa majaribio leo Jumatatu dhidi ya Costa Rica.

Shirikisho la kandanda la Italia limetangaza kikosi cha wachezaji wake 23 watakaoshiriki katika fainali za kombe la dunia mwaka huu nchini Brazil bila mashujaa wao Giuseppe Rossi na Riccardo Montolivo ambaye ameumia. Kocha Cesare Prandelli ameamua kutomtegemea mshambuliaji wa Fiorentina , ambaye ameumia goti mwezi Januari na alirejea uwanjani mwezi Aprili.

Neuseeland - Italien WM Weltmeisterschaft Fußball
Ricardo MontolivoPicha: AP

Kuondolewa kwa mchezaji wa kati ya AC Milan Montolivo hakukuwa na budi kwani alivunjika mguu katika mchezo wa majaribio dhidi ya Ireland mwishoni mwa juma.

Cote D'Ivoire na matumaini yao

Kolo Toure amejumuishwa katika kikosi cha kombe la dunia cha Cote D'ivore licha ya kuwa anaugua malaria , akijiunga na mdogo wake Yaya Toure na mshambuliaji wa siku nyingi Didier Drogba katika kikosi cha wachezaji 23 wa timu hiyo ambacho kitaelekea huko Brazil.

Shirikisho la soka la kimataifa FIFA limeshuhudia mchezo wa mwisho wa majaribio katika uwanja ambao utatumika katika mchezo wa ufunguzi wa fainali za kombe la dunia Juni 12 nchini Brazil. Kiasi ya mashabiki 37,000 waliingia kushuhudia pambano kati ya Corinthians na Botafogo mpambano uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Uwanja huo una uwezo wa kuingiza mashabiki 68,000 ambao wanatarajiwa kushuhudia pambano la ufunguzi kati ya Brazil na Croatia hapo Juni 12.

FIFA Präsident Sepp Blatter und Vizepräsident Issa Hayatou
Issa Hayatou (kulia) na rais wa FIFA Sepp BlatterPicha: picture alliance/AP Photo

Baadhi ya sehemu za uwanja huo bado hazijafanyiwa majaribio na maeneo mengine yatafanyiwa mabadiliko katika siku zijazo, amesema Toago Paes , meneja wa kamati ya maandandalizi nchini Brazil.

Qatar yakabiliwa na shutuma

Kura ya kuamua ni nchi gani itakuwa mwenyeji wa fainali za kombe la dunia mwaka 2022 huenda ikarejewa kutokana na madai ya rushwa yanayozunguka ushindi wa Qatar , iwapo ushahidi utakuwa sahihi, Lord Goldsmith , mjumbe wa tume huru ya FIFA ya utawala amesema leo.

Gazeti moja la Uingereza limedai jana kuwa lina ushahidi kwamba kiasi cha dola milioni 5 zililipwa kwa maafisa ili kupata kura kwa ajili ya ombi hilo la Qatar kupata kuwa mwenyeji wa fainali hizo, madai ambayo watayarishaji wa fainali hizo Qatar wanayapinga kwa nguvu zote.

Goldsmith , mwanasheria mkuu wa serikali wa zamani wa Uingereza , amesema kuwa iwapo shirikisho hilo la kandanda la dunia linataka kuzuwia kashfa kuhusiana na maombi ya kuwa mwenyeji wa fainali za kombe la dunia, linapaswa kutoa ushahidi na jibu lenye uwazi kwa madai kama hayo.

Nae Issa Hayatou, rais wa shirikisho la kandanda barani Afrika CAF na ambaye ni makamu rais wa FIFA amekana kabisa madai ya gazeti hilo la Uingereza la Sunday Times kuwa amepokea takrima na fedha kuunga mkono ombi la Qatar kuwa mwenyeji wa kombe la dunia mwaka 2022.

Nalo shirikisho la kandanda la Australia limesema leo kuwa huenda likawasilisha tena ombi lake la kuwa mwenyeji wa fainali za mwaka 2022, baada ya madai mapya ya rushwa kuzuka dhidi ya Qatar.

Mitgliederversammlung des FC Bayern München Uli Hoeneß 2.5.2014
Uli Hoeness rais wa Zamani wa Bayern MunichPicha: picture-alliance/dpa

Na mataifa ya Afrika yana nafasi nzuri ya kuwa mwenyeji wa michezo ya Olimpiki hapo baadaye iwapo mabadiliko yanayopendekezwa kuwania nafasi hiyo yataidhinishwa na kamati ya kimataifa ya Olimpiki IOC, amesema rais wa kamati hiyo Thomas Bach. Bach ambaye amefanya ziara ya mataifa matatu ya Afrika , Afrika kusini, Kenya na Ethiopia , baada ya kuhudhuria michezo ya vijana ya Afrika mjini Gaberone, Botswana , amesema matumaini yake ni kuona bara hilo likiwa mwenyeji wa mashindano hayo makubwa duniani.

Hoeness hatimaye aripoti jela

Na kwa upande mwingine rais wa zamani wa Bayern Munich Uli Hoeness ameanza kutumikia kifungo kwa kukwepa kulipa kodi. Hoeness alihukumiwa na mahakama ya mjini Munich Machi mwaka huu kwa kukwepa kulipa kodi baada ya kuwa na akaunti ya siri nchini Uswisi na kuhukumiwa kwenda jela miaka mitatu unusu. Wakili wake amesema kuwa Hoeness ameripoti katika jela ya Landsberg am Lech kusini mwa Ujerumani leo Jumatatu.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre / afpe / dpae

Mhariri. Mohammed Abdul Rahman.