1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongamano la vyama vya CDU/CSU na FDP huko Meseberg

Oumilkher Hamidou19 Novemba 2009

Majadiliano ya siku mbili hayajasaidia kumaliza mivutano

https://p.dw.com/p/Kb14
Baraza la mawaziri lajaribu kusawazisha mivutano huko katika kasri la MesebergPicha: AP

Kongamano la serikali kuu ya muungano huko Meseberg,hatima ya shughuli za wanajeshi wa Ujerumani kutumikia amani nchi za nje na mgomo wa wanafunzi ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Tuanze lakini na kongamano la Meseberg ambalo wahariri wanakubaliana washirika wa serikali ya muungano wamejitokeza kana kwamba wanasikilizana,kumbe kindani ndani wanaficha mivutano.Gazeti la Stuttgarter Zeitung linaandika:

Hata huko Meseberg mada zinazozusha mabishano hazikusawazishwa hata kidogo-zimeakhirishwa tuu.Na ikiwa zimetajwa basi ni kwa kupanga ratiba ya kupatiwa ufumbuzi na kwa namna hiyo kumaliza mivutano.Haijulikani lakini vipi serikali ya muungano ya nyeusi na manjano inapanga kugharimia mfumo wa afya na kuwatunza wazee na wagonjwa,sawa na jinsi wanavyofikiria kuleta wezani sawa kati ya kupunguza mzigo wa madeni na kupunguza kodi ya mapato.Bado ni mapema kuashiria vipi serikali hii ya muungano inapanga kuanza kutawala.Kinachojulikana ni kwamba wakati umewadia!

Gazeti la "Sächsische Zeitung " la mjini Dresden lina maoni sawa na hayo na linaandika.

Kule ambako kawaida mabweha na sungura wanajificha usiku unapoingia,ndiko kansela Merkel, Westerwelle na wengine walikoamua kukutania ili kuipatia ufumbuzi mivutano ya vyama vyao.Muhimu kwa kansela ilikua kusaka msimamo wa pamoja katika masuala kadhaa.Lakini kongamano hilo la siku mbili halikuleta tija iliyokua ikitarajiwa.Badala ya kufafanua vifungu vinavyozusha mabishano vya mkataba wa serikali ya muungano uliotiwa saini hivi karibuni,vyama ndugu vya CDU/CSU na washirika wao wa FDP wametumia ile mbinu ya kuachia kamati maalum zishughulikie mada ambazo hazikuweza kupatiwa ufumbuzi.

Mada yetu ya pili inahusu hatima ya shughuli za kulinda amani za vikosi vya jeshi la Ujerumani nchi za ng'ambo.Gazeti la General Anzeiger linaandika:

Ni ishara bayana ya mshikamano pamoja na washirika wa jumuia ya kujihami ya magharibi NATO:Serikali mpya ya muungano imeshatamka,licha ya mjadala ndani nchini na kero linalozidi miongoni mwa jumuia ya kimataifa kutokana na udhaifu wa rais Hamid Karzai,Ujerumani itaendelea na jukumu lake nchini Afghanistan.Bunge litaunga mkono mpango huo.Muhimu kwa jeshi la shirikisho ni kupata hakikisho vifaa vya kutosha vitapatikana kudhamini usalama wao.Msaada timamu kwa wanajeshi hao wanaotumikia amani nchi za nje ni muhimu zaidi badala ya matamshi matupu ya kudai mshikamano.

Studentenproteste an der Uni Duisburg Essen
Wanafunzi wakalia ukumbi wa mhadhara katika chuo kikuu cha Duisburg EssenPicha: DW/Kapustina

Mada yetu ya mwisho magazeti inahusu maandamano ya wanafunzi na gazeti la Abendzeitung la mjini Münich linaandika:

Vugu vugu la mwaka 2009 la wanafunzi halina maingiliano makubwa na maandamano ya miaka ya nyuma ya wanafunzi.Wanafunzi wa leo hawadai ulimwengu bora.Wanataka nafasi za kutosha katika kumbi za mihadhara na shahada itakayowafungulia mustakbal mwema.Hiyo inaingia akilini.Pengine masharti ya kusoma hayajawahi kuwa mabaya kama hivi sasa.Zaidi ya hayo wanalazimika kulipa karo .Kwamba hivi sasa kuna wanasiasa wanaoonyesha kuzielewa hasira za wanafunzi ni jambo la kutia moyo.Lakini wanafunzi wasikubali kudanganywa kwa ahadi tupu.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir (Inlandspresse)

Mhariri:Abdul-Rahman