1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini kupeleka washangiliaji Olimpiki

Lilian Mtono
17 Januari 2018

Korea Kaskazini itatuma washangiliaji 230 katika michezo ya Olimpiki nchini Korea Kusini mwezi ujao, hii ikiwa ni kulingana na Korea Kusini baada ya mazungumzo wakati kukiwa na mahusiano mabaya kati ya Korea hizo mbili.

https://p.dw.com/p/2qy2N
Südkorea Logo Olympische Winterspiele 2018
Picha: Getty Images/K. Nagahama

Korea Kaskazini itatuma timu ya washangiliaji 230 katika michezo ya Olimpiki itakayofanyika Korea Kusini mwezi ujao, hii ikiwa ni kulingana na Korea Kusini baada ya pande zote kufanya mazungumzo wakati kukiwa na mahusiano mabaya kati ya Korea hizo mbili, na wakati Japan ikiomba kuchukuliwa tahadhari kuhusiana na ishara za kirafiki kutoka kwa Korea Kaskazini. 

Korea Kaskazini na Kusini zimekuwa kwenye mazungumzo tangu wiki iliyopita, ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka miwili, na wakati huu wakizungumzia michezo ya Olimpiki, hatua inayoleta nafuu kutokana na mvutano uliodumu kwa miezi kadhaa juu ya mipango ya kinyuklia na makombora ya Korea Kaskazini, ambayo imeendelea kuifanya na kukaidi vikwazo vya Umoja wa Mataifa.  

Mataifa 20 yanayokutana katika mji mkuu wa Canada, Vancouver yamekubaliana hapo jana kuiwekea vikwazo vikali zaidi ili kuiminya Korea Kaskazini kuachana na silaha za kinyuklia huku waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Rex Tillerson akiionya Korea Kaskazini kwamba itawafanya kuchukua hatua za kijeshi, kama haitakubali kuchagua mazungumzo.  

Korea Kaskazini bado inaendeleza mipango yake ya nyuklia licha ya vikwazo vya UN.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Japan Taro Kono amesema dunia haitakiwi kuuchukulia juu juu urafiki unaonekana kuanzishwa na Korea Kaskazini.

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amekataa kuachana na mipango yake ya kutenegeneza makombora ya nyuklia yenye uwezo wa kuishambulia Marekani, pamoja na kuongezeka kwa vikwazo vikali zaidi vya Umoja wa Mataifa, hali inayoongeza wasiwasi wa kuibuka kwa vita vipya  katika rasi ya Korea. Korea Kaskazini ilifanya majaribio ya makombora katika anga ya Japan.

Deutschland Eiskunstlauf Nebelhorn Trophy- Tae Ok Ryom und Ju Sik Kim
Wachezaji wa mchezo wa kuteleza kwenye barafu kutoka Korea Kaskazini wanaoshiriki michezo ya Olimpiki.Picha: picture-alliance/dpa/P. Kneffel

Katika taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari wiki hii, Korea Kaskazini iliionya Korea Kusini kwa kuvuruga mahusiano kati ya nchi hizo mbili kwa kusisitiza kuwa iachane na mipango yake ya silaha za nyuklia. 

Duru kutoka wizara ya Korea Kusini inayohusika na masuala ya umoja wa nchi hizo mbili imesema pande zote mbili zimebadilishana mawazo kuhusu masuala kadhaa, ambayo ni pamoja na ukubwa wa kikosi cha wanariadha wa Korea Kaskazini na namna watakavyoshirikiana katika michezo ya pamoja ya Kitamaduni. 

Korea Kusini imependekeza kuwepo kwa kikosi cha pamoja na Korea Kaskazini cha mchezo wa mpira wa magongo, hatua iliyosababisha ghadhabu kutoka kwa wanariadha wa Korea Kusini, ambao walitaarifiwa ghafla kwamba wanatakiwa kucheza pamoja na watu wasiojuana kabisa.

Idadi ya maombi yaliyowasilishwa katika tovuti ya Ikulu ya rais wa Korea Kusini, yanayopinga kuwepo kwa timu ya pamoja yamepanda na kufikia 100 wiki hii, huku ombi maarufu zaidi likipata zaidi ya kura 11,000.

China ambayo haikuhudhuria mkutano huo wa Vancouver imesema hii leo kwamba mkusanyiko huo unaonyesha mtazamo wa vita baridi na utadidimiza hatua za kutatua tatizo la Korea Kaskazini.

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE.
Mhariri:Yusuf Saumu