1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yairipuwa ofisi ya pamoja na Korea Kusini

Saleh Mwanamilongo
16 Juni 2020

Korea Kaskazini imesema inaliweka jeshi lake kwenye hali ya kivita, siku moja baada ya kuiripuwa ofisi ya pamoja kati yake na Korea Kusini.

https://p.dw.com/p/3ds1W
Korea ya Kaskazini imeripuwa ofisi ya pamoja na jirani wake wa kusini kwenye eneo la mpaka la Kaesong.
Korea ya Kaskazini imeripuwa ofisi ya pamoja na jirani wake wa kusini kwenye eneo la mpaka la Kaesong.Picha: Reuters/Yonhap

Korea Kaskazini imesema inaliweka jeshi lake kwenye hali ya kivita, siku moja baada ya kuiripuwa ofisi ya pamoja kati yake na Korea Kusini,ikiutuhumu upande wa kusini kuruhusu wanaharakati kurusha maputo yenye ujumbe wa uchochezi kuelekea kaskazini.Korea ya kusini imelaani vikali kitendo hicho na kuahidi kujibu ikiwa Pyongyang itaendeza uchokozi.

Ofisi hiyo iliyofunguliwa Septemba 2018 kama sehemu ya makubaliano kati ya kiongozi wa kaskazini Kim Jong Un na Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini, ilikuwa kwenye mji wa Kaesong, ulio mpakani upande wa kaskazini. Mkuu wa jeshi la Korea Kaskazini amesema wanaandaa mkakati wa kuingia maeneo ambayo yaligeuzwa kuwa yasiyo na shughuli za kijeshi mwaka 2018, akitishia kuyageuza magofu. Jengo hilo la ghorofa nne lilikuwa linatumiwa na kampuni kadhaa za Korea Kusini, ambazo zimeajiri wafanyakazi kutoka kaskazini,na ambao mishahara yao hulipwa kwa serikali ya Korea Kaskazini.

Afisa wa usalama wa Korea ya kusini kwenye mpaka na Korea ya kaskazini kwenye mji wa  Kaesong.
Afisa wa usalama wa Korea ya kusini kwenye mpaka na Korea ya kaskazini kwenye mji wa Kaesong. Picha: Reuters/K.Hong-Ji

Kwenye kikao cha dharura,baraza la usalama la Korea ya Kusini lilitangaza kwamba litajibu vikali ikiwa serikali ya korea ya kaskazini itaendelea kuchukuwa hatua za uchokozi.

Kim You-guen,naibu mkuu wa baraza la kitaifa la usalama nchini Korea ya kusini.

''Serikali ya Korea ya Kusini inaweka wazi kwamba Korea ya Kaskazini itabeba dhamana ya hali yote itakayojiri. Na tunatahadharisha kwamba ikiwa Korea ya kaskazini itaendeleza vitendo vitakavyoathiri hali ya kiusalama.Tutajibu vikali''.

Baadhi ya wataalamu wanashuku kwamba Korea ya Kaskazini inatafuta kueko na mzozo baina ya nchi mbili hizi ili kuipumbaza jumuiya ya kimataifa, kufuatia kusuasua kwa mazungumzo kuhusu silaha za Nyuklia.

Jengo hilo lilikuwa ni alama ya kwanza ya kuboresha uhusiano baina ya Korea ya kusini na jirani wake wa Kaskazini na vilevile Marekani katika juhudi za kupunguza uhasama wa kijeshi.

Uhusiano baina ya Korea hizo mbili ulianza tena kudhoofika kufuatia kutofanikiwa kwa mkutano wa pili baina rais wa Marekani Donald Trump na kiongozi wa Korea Kusini Kim Jong UN,mwezi februari mwaka jana mjini Hanoi (Vietnam).

Cheong Seong-Chang, mkuu wa kituo cha utafiti kuhusu Korea ya Kaskazini kilichoko mjini Seoul,anasema kwamba Kim Jong Un hajaridhishwa na Korea ya Kusini ambayo anaamini imeshindwa kuchangia kama mpatanishi katika mazungumzo yake na Marekani.Kazi za ujenzi wa ofisi hiyo ya pamoja zilisitishwa mwezi Januari kutokana na mripuko wa ugonjwa wa Corona.