1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yatishia kuufuta mkutano na Marekani

Sudi Mnette
16 Mei 2018

Korea Kaskazi imetishia kuufuta mkutano unaotarajiwa mwezi ujao kati ya kiongozi wa taifa hilo, Kim Jong Un na Rais wa Marekani Donald Trump ikisema haina maslahi katika mahusiano ya kutegemea matakwa ya upande mmoja

https://p.dw.com/p/2xnlG
Südkorea TV Donald Trump, Kim Jong Un
Picha ya Rais Donald Trump na Kim jong Un kama ilivyoonesha katika televisheni ya Korea KusiniPicha: picture-alliance/AP Photo/Young-joon

Awali, Korea Kaskazini iliufuta pia mkutano wa ngazi ya juu ambao ungefanyika leo kati yake na Korea Kusini.

Onyo hilo la Korea Kaskazini limetolewa na makamu wa kwanza wa waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, katika kipindi cha masaa kadhaa baada ya taifa hilo kusitisha ghafla mkutano wa maafisa wa ngazi ya juu na Korea Kusini, ikipinga  mazoezi ya kijeshi ya pamoja kati ya Marekani na Korea Kusini, ambayo kwa  muda mrefu serikali ya Pyongyang imekuwa ikidai ni maandalizi ya uvamizi.

Hatua ya kuondosha hofu

Korea-Gipfel 2018 Umarmung Kim und Moon
Kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un na Rais wa Korea Kusini Moon Jea-inPicha: Reuters

Hatua hiyo ya kushtukiza inapoza joto la hatua zisizo za kawaida za kuridhia mazungumzo kutoka taifa hilo ambalo kwa mwaka uliopita lilikuwa likifanya mfululizo wa majaribio ya makambora,na kuzua wasiwasi kwamba eneo hilo lipo katika hatua ya kuingia vitani. Wachambuzi wanasema sio kwamba Korea Kaskanzini  inataka kupingana na hatua zote za kidiplomasia lakini inataka kunufaika katika mazungumzo hayo kati ya kiongozi Kim na Rais Trump,iliyopangwa Juni 12 huko Singapore.

Katika taarifa yake iliyotangazwa na vyombo vya habari vya umma vya nchi hiyo makamu wa kwanza wa wizara ya mambo ya nje wa Korea Kaskanzini, Kim Kye Gwan amenukuliwa akisema "Hatuna tena maslahi katika mazungumzo ambayo yanatatuweka katika wakati mgumu na kufanikisha matakwa ya upande mmoja, ambayo itatulazimisha kulizingatia pale tutakapo ridhia mkutano wa kilele kati ya Korea Kaskazini na Marekani.

Mshauri wa Trump akosolewa

Aidha katika taarifa yake hiyo ameyakosoa kauli ya mshauri wa masuala ya usalama wa Trump, John Bolton, na maafisa wengine ambao walisema Korea Kaskazini wanapaswa kufuata namna ya Libya  iachane na shughuli zake za kinyuklia , sawa na  ilivyofanyika wakati wa Utawala wa kiongozi wa wakati huo Muammar Gaddafi. Na kutoa ushahidi wa utekelezaji wa hatua hiyo. Pia aligusia suala la maoni ya Marekani kwamba taifa lao linapaswa kuachana kabisa uundaji wa silaha za kibiolojia na kikemikali.

Baadhi ya wachambuzi wanasema kulizusha suala la Libya, ambayo iliiharibu mpango wake wa nyuklia katika miaka ya 2000 kwa masharti ya kupunguziwa  vikwazo iliyokewa katika kipindi hicho inaweza kuhatarisha mustakabali wa  mazungumzo hayo kati ya Korea Kaskazini na Marekani. Kim Jong Un aliingia madarakani majuma kadhaa baada ya kifo cha kiongozi wa zamani wa Libya Moammar Gadhafi kilichotokea katika mikono ya vikosi vya waasi Oktoba 2011.

Mwandishi: Sudi Mnette/APE
Mhariri: Gakuba, Daniel