1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kosovo haijakiuka sheria ya kimataifa

22 Julai 2010

Hatua iliyochukuliwa na Kosovo kujitenga na Serbia mwaka 2008 haijakiuka sheria ya kimataifa. Hivyo ndio Mahakama ya Kimataifa ilivyoamua hivi punde mjini The Hague.

https://p.dw.com/p/ORtz
President of the court Judge Owada, centre, accompanied by Vice-President of the Court Judge Peter Tomka, left, and Judge Awn Shawkat Al-Khasawneh, right, are seen in the Great Hall of Justice at the World Court in The Hague, Netherlands, Thursday, July 22, 2010. The United Nations' highest court is issuing an advisory opinion on whether Kosovo's 2008 declaration of independence from Serbia was legal, a ruling that could set a precedent for separatist regions around the world. (AP Photo/Evert-Jan Daniels)
Jaji Owada (kati) akieleza maoni ya Mahakama Kuu ya Umoja wa Mataifa mjini The Hague, kuhusu Kosovo.Picha: AP

Uamuzi huo huenda ukawa na athari zake miongoni mwa makundi yanayopigania kujitenga kote ulimwenguni. Vile vile huenda ukazipa moyo nchi zaidi kutambua uhuru wa Kosovo na hivyo kusaidia nchi hiyo kupokewa kama mwanachama katika Umoja wa Mataifa. Uamuzi wa Mahakama Kuu, ambao kisheria, si lazima kuheshimiwa, unahusika na dai lililotolewa na Serbia katika mwaka 2009 kuwa Kosovo haikuheshimu mipaka yake ilipojitangazia uhuru. Marekani na nchi nyingi zingine za magharibi zimetambua uhuru wa Kosovo uliotangazwa Februari mwaka 2008. Lakini Serbia na mshirika wake Urusi zimepinga kuitambua Kosovo kama taifa huru.

Kabla ya kupitishwa uamuzi wa Mahakama Kuu ya Umoja wa Mataifa, Rais wa Serbia Boris Tadic alinukuliwa akisema kuwa uamuzi wa mahakama hiyo ukiweka msingi mpya, basi kote duniani kutazuka wimbi la kuundwa mataifa mapya. Kwa maoni yake, hiyo itasababisha machafuko katika maeneo mbali mbali duniani. Kwa upande mwingine,Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden, hiyo jana alipokutana na Waziri Mkuu wa Kosovo, Hashim Thaci, mjini Washington, alisisitiza kuwa Marekani inaunga mkono uhuru wa Kosovo.

Serbia ilitimuliwa Kosovo mwaka 1999, kufuatia kampeni ya mashambulio ya siku 78 yaliyofanywa na majeshi ya NATO. Kampeni hiyo, ilimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka miwili, kati ya Serbia na Wakosovo wenye asili ya Kialbania. Baadae, eneo hilo liliwekwa chini ya uongozi wa Umoja wa Mataifa naamani kulindwa na majeshi ya NATO. Maelfu ya watu waliuawa katika mgogoro huo wa Kosovo na wengi wao walikuwa wenye asili ya Kialbania. Asilimia 90 ya wakaazi wa Kosovo wapatao milioni 2, wana asili ya Kialbania.

Hadi sasa, Kosovo imetambuliwa kama nchi huru, na mataifa 69. Miongoni mwa nchi hizo, ni Marekani na mataifa 22 kutoka jumla ya nchi wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya. Urusi iliyo mshirika wa Serbia haikutambua uhuru wa Kosovo na China pia inakataa kutambua uhuru wa Kosovo. Serikali ya Serbia mjini Belgrade inataka kuwa na majadiliano kuhusu hatima ya Kosovo, ikishikilia kuwa hilo ni jimbo lake la Kusini. Lakini Kosovo, imeondosha kabisa uwezekano wa kufanywa majadiliano hayo na inatoa mwito kwa mataifa zaidi kutambua uhuru wake.

Mwandishi:P.Martin/AFPE

Mhariri: Charo,Josephat