1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kroos awakosoa wachezaji baada ya kipigo cha Brazil

Iddi Ssessanga
28 Machi 2018

Toni Kroos amewanyooshea kidole cha lawama wachezaji wenzake kufuatia kipigo cha goli 1-0 dhidi ya Brazil, lakini Kocha Joachim Loew amesisitiza timu yake itakuwa tayari kwa mashindano ya kombe la dunia.

https://p.dw.com/p/2v8wc
Freundschaftsspiel Deutschland Brasilien Toni Kroos
Picha: picture-alliance/GES/T. Eisenhuth

Kroos ndiye mshindi wa karibuni wa kombe la dunia kuikemea timu ya Ujerumani kwa uchezaji mbovu, baada ya goli la kipindi cha kwanza la Gabriel Jesus kuihakikishia Brazil ushindi wa 1-0 katika mechi ya kirafiki iliyochezwa Jumanne usiku mjini Berlin.

Baada ya Jerome Boateng kucharuka na kusema "kila kitu" kinahitaji kuboreshwa kufuatia sare ya 1-1 dhidi ya Uhispania siku ya Ijumaa, Kroos naye pia ameshindilia.

"Tulikuwa na baadhi ya wachezaji uwanjani ambao walikuwa na fursa ya kujionyesha kwa ngazi hii - lakini hawakutumia fursa hiyo," Kroos alilalamika, na kuongeza kuwa "tuliruhusu kudhibitiwa na kisha tuliona kwamba hatuko vizuri kama tunavyoambiwa kila mara - na pengine baadhi yetu tunavyodhani tupo."

Kipigo hicho cha nyumbani kiliwagharimu mabingwa hao wa dunia rekodi yako ya kutofungwa kwa mechi 22 mfululizo inayoanzia kwenye kipigo cha Ufaransa katika nusu fainali ya michuano ya kombe la Ulaya ya 2016.

Kwa sare zilizotangulia dhidi ya Uingereza, Ufaransa na Uhispania, Wajerumani wameshindwa kupata ushindi katika mechi zao nne zilizopita -- hali inayozusha wasiwasi mnamo wakati kombe la dunia linakaribia.

Fußball Länderspiel Deutschland - Brasilien
Toni Kroos (kushoto) na wenzake baada y akupigwa 1-0 na Wabrazil mjini Berlin.Picha: picture-alliance/dpa/A. Gebert

Brazil ilichezesha karibu timu kamili, ikimkosa tu Neymar, huku Loew akichaguwa kuwapa fursa wachezaji wa akiba fursa ambayo hawakuitumia vizuri. Wachezaji wawili tu kutoka kikosi cha ushindi wa kombe la dunia -- Kroos na kaimu nahodha Boateng, walianza dhidi ya Selecao.

Kocha huyo aliyeiongoza Ujerumani kwenye ushindi wa kombe la dunia alikuwa na orodha ndefu ya malalamiko: Mipira mingi sana ilipotezwa dhidi ya Brazil, upangaji mbaya, udhaifu katika kujibu mashambulizi na changamoto.

Hata lugha ya mwili ilikuwa mbovu, alisema Loew, na wakati Jesus alipofunga bao la ushindi katika dakika ya 38, "tulikuwa wabaya katika kila idara."

Hata hivyo kocha huyo wa Ujerumani bado hajakata tamaa na kazi inayotakiwa kufanywa kabla ya mechi yao ya kwanza dhidi ya Mexico Juni 17.

"Hapana sina wasiwasi kuhusu jambo lolote kwa sababu timu hii ina uwezo wakufanya jambo lolote tofauti kabisaa," alihakikisha Loew. "Huwezi kutaka kupoteza mechi kama hiyo, lakini naweza kukubali matokeo hayo na kufanyia kazi masuala matatu au manne."

Hakuna mechi nyingine hadi Loew atakapokitaja kikosi chake cha kombe la dunia Mei 15, kabla ya mechi za kirafiki za kujipima nguvu dhidi ya Austria Juni 2, na Saudi Arabia siku sita baadae.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe.

Mhariri: Josephat Charo.