1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kucheza dhidi ya Brazil ni ndoto ya wachezaji wa Ubelgiji

Sekione Kitojo
4 Julai 2018

Michezo ya robo fainali ya kombe la dunia mwaka  2018 nchini Urusi  inaanza  rasmi Ijumaa kwa  pambano kati  ya Uruguay na Ufaransa. Lakini pambano  linalosubiriwa kwa hamu kubwa ni  kati ya Brazil dhidi ya Ubelgiji.

https://p.dw.com/p/30oGw
Fußball WM 2018 Kolumbien vs England
Picha: Getty Images/AFP/M. Antonov

Brazil wanaonekana  kupigiwa  upatu kushinda  pambano  hili katika kile  ambacho  kocha  wa  Ubelgiji Roberto Martinez alichokieleza kuwa  ni "ndoto" kwa wachezaji  wake wakati  mataifa  hayo  mawili yatakapokutana  katika  mchezo  wa  robo  fainali mjini  Kazan siku ya  Ijumaa.

Fußball WM 2018 Brasilien vs Mexiko Torjubel
Firmino (kushoto) na Neymar (kulia) wakishangiria bao la BrazilPicha: Reuters/M. Dalder

"Timu  hizi  mbili zimejengwa kufunga  mabao  na  kushinda  michezo. Dhidi ya  Brazil, haitakuwa  juu  ya  umiliki  wa  mpira, lakini kile unachoweza  kufanya  na  mpira. Hicho ndio kila  kitu  katika kombe hili  la  dunia,"  Wahispania  waliviambia  vyombo  vya  habari  vya Ubelgiji leo Jumatano(04.07.2018).

"Tunafahamu  kile  tunachokiweza lakini  Brazil wako  mbele, wakituweka  katika  nafasi tofauti  kabisa," aliongeza  Martinez.

"Lakini  ni mchezo  ambao  kama tumo  katika  ndoto kwa  wachezaji wetu, wamezaliwa  kucheza  katika  mchezo  kama  huu. Kwa kawaida  tunataka  kushinda lakini  hatutarajiwi  kufanya  hivyo  na hii  ndiyo  tofauti  muhimu."

Martinez alishuhudia  kikosi  chake  kikiwa  katika  ukingo wa kuondolewa  mashindanoni na  kupata  ushindi  wa  dakika  za mwisho wa  mabao 3-2 dhidi  ya  Japan  katika  duru  ya  timu  16 siku  ya  Jumatatu, na kukata  tikiti  ya kukutana  na  mabingwa mara  tano  wa  kombe  la  dunia Brazil.

Fußball WM 2018 Brasilien vs Mexiko Tor
Brazil wakishangiria bao dhidi ya MexicoPicha: Reuters/P. Olivares

Katika  baadhi  ya  nyakati mjini  Rostov - on - Don, Ubelgiji ilionekana  kukwazika  na  mbinu  za mbinyo za  Japan  na  walihitaji zaidi  ya  saa  nzima  kujitoa  na kuweza  kurejea  katika  mchezo kutoka  nyuma  baada  ya  kutandikwa  mabao 2-0 na  Japan.

Kwa mchezo  wa  Ijumaa  mbinu  huenda  zitakuwa  rahisi.

"Dhidi  ya  timu  kama  Brazil , ni  lazima  ushambulie na  kulinda lango na  wachezaji 11. Hatuzungumzii juu  ya  mfumo lakini kufahamu  kile  tunachopaswa  kufanya wakati  tuna  mpira," kocha huxo  alisema.

Sidhani  iwapo utakuwa  mchezo wenye siri nyingi. Tunapaswa kulinda  kandri  tunavyoweza na kisha  kuwasababishia  maumivu makali  wakati  tukiwa  na  mpira. Itakuwa  rahisi  hivyo na  kikosi hiki kiko  tayari kwa  hilo."

Uingereza  ilielekeza  hisia zake  katika  mchezo  mgumu  wa  robo fainali  dhidi ya  Sweden  wakati  wakilenga  kuendeleza  ushindi wake  dhidi  ya  Colombia, katika ushindi  wake  wa  kwanza  kupitia mikwaju  ya  penalti  katika  kombe  la  dunia.

Fußball WM 2018 Kolumbien vs England
Kocha wa England Gareth SouthgatePicha: Reuters/K. Pfaffenbach

England haibweteki baada  ya  ushindi  huo wakati  ikijitayarisha kupambana na  Sweden  katika  mchezo  wa  robo  fainali siku  ya Jumamosi.

"Ni  wagumu  sana  kupambana  nao," kocha Gareth Southgate alisema  kuhusiana  na  kikosi  cha  Sweden. "Kwa  wakati  huu tuko juu  kama tiara lakini  nadhani  ni  lazima  tushuke. Ni  mchezo mkubwa  kushiriki. "Nawaheshimu  sana Sweden. rekodi  yetu  dhidi yao  sio  nzuri. Mara kadhaa tumewadharau."

Pambano  la Jumamosi mjini  Samara  ni  la  tatu  baina  ya  timu  hizo  katika kombe  la  dunia, kufuatia  sare  katika awamu  ya  makundi  mwaka 2002 , bao (1-1) na  2006 bao (2-2). Pia  walikutana  mara  mbili katika  ubingwa  wa  bara  la  Ulaya , ambapo  Sweden  ilishinda kwa  mabao 2-1 mwaka  1992 na  Uingereza  ikashinda  kwa  mabao 3-2  mwaka  2012.

Fußball WM 2018 Kolumbien vs England
Wachezaji wa Uingereza wakishangiria ushindi wa mikwaju ya penalti dhidi ya ColombiaPicha: Getty Images/M. Hangst

Michezo  mingi  ya  kirafiki baina  ya  timu  hizo imekuwa ngumu  kwa kila  upande kwa  hiyo  mambo  madogo  madogo  yanaweza  kuleta mabadiliko, kama  vile Sweden  ilicheza  mchezo  wake  wa  kundi  la 16 bora  masaa  manne  kabla  ya  uingereza  na  ilihitaji dakika 90 tu kuwaondoa  Uswisi kwa  bao 1-0. Uingereza kwa  upande  wake ilihitaji  dakika 120 , baada  ya  goli  la  dakika  za  mwisho  la Colombia la  kusawazisha baada ya bao  la  kuongoza la  nahodha wa  England, Harry Kane kwa  mkwaju  wa  penalti.

Lakini  usiku  wa  jana ulikuwa  muhimu  sana  kwa  kikosi  hiki kichanga cha  kocha  Southgate , ambaye  binafsi  alikosa  mkwaju wa  penalti  katika  nusu  fainali ya  Euro 1996  dhidi  ya  Ujerumani.

Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae

Mhariri: Iddi Ssessanga