1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kujiuzulu kwa Rumsfeld, maoni ya D.Scheschkewitz

9 Novemba 2006

Kutokana na chama chake cha REPUBLICAN kushindwa katika uchaguzi wa bunge rais George W.Bush amemwondoa waziri wake wa ulinzi Donald Rumsfeld.Jee hayo ni mabadiliko ya sura ama ya sera?

https://p.dw.com/p/CHLC

Kujiuzulu kwa bwana Rumsfeld ni hatua ya aherini . Kwa muda mrefu rais Bush alikuwa anamtetea waziri wake lakini sasa kisu kimefika mfupani baada ya mtokeo ya uchaguzi wa bunge kufahamika.

Kwani uchaguzi huo ulikuwa kura ya maoni juu ya vita vya Irak. Bwana Rumsfeld amekuwa anaulumiwa kwa muda mrefu kwa kuendesha vita vya Irak kwa njia ya utobwe, yaani bila ya ustadi, pia amekuwa analaumiwa kwa kuvielekeza vita hivyo katika vurumai. Kama waziri wa ulinzi yeye ndiye alieviandaa na kuviongoza.

Hayo yalisababisha apoteze umaarufu miongoni mwa wananchi na miongoni mwa majeshi.

Majenerali wanane wa jeshi la Marekani pamoja na magazeti maarufu yalimlitaka waziri huyo wa ulinzi ajiuzulu kutokana na jinsi aliyvokuwa anaendesha vita vya Irak.

Bwana Rumsfeld mwenyewe siku nyingi alitashatambua kwamba maji yalikuwa yashamefika utosini. Mara tu baada ya picha juu ya jela ya Abughraib nchini Iraka kutolewa hadharani aliomba kujiuzulu.

Picha hizo zilizonesha jinsi wafungwa katika jela hiyo walivyokuwa wanateswa na kudhalilishwa. Katika harakati za kupambana na ugaidi Marekani imechepuka kidogo kutoka kwenye njia ya uungwana. Mateso yametendeka katika harakati hizo na wizara ya ulinzi imehusika.

Lakini baya zaidi kwa bwana Rumsfeld ni ukaidi aliokuwa anafanya juu ya mapendekezo yaliyokuwa yanatolewa na majenerali wake. Kwa mfano majenerali hao walitaka idadi kubwa ya askari ili kuweza kuleta utengemavu nchini Irak. Lakini waziri wao alileta kichwa - ngumu. Alisema ingeliwezekana kuidhibiti Irak kwa kutumia kiasi kidogo cha fedha.

Kama mpangaji wa vita vya Irak waziri Rumsfeld alifanya kosa jingine kubwa sana.

Mara tu baada ya majeshi ya Marekani kuivamia Irak na kumng’oa Saddam Hussein, hatua ya kwanza kuchukuliwa ilikuwa kulivunja jeshi la nchi hiyo, japo Marekani haikuwa na askari wa kutosha wa kuweza kuidhibiti Irak inayoendelea kusambaratika.

Jee isingeliwezekana kuliweka jeshi la Irak la wakati huo chini ya uongozi mwingine?

Matokeo ya kosa hilo ni kwamba sasa wapiganaji wa jamii mbalimbali wanauana katika kuwania mamlaka ; na jeshi la Marekani halina uwezo wakuzuia mauaji hayo-kwani askari wengi wa jehi hilo bado wana ubwabwa wa shingo!

Rumsfeld anabeba lawama juu ya Irak kizidi kudidimia mnamo vita vya wenyewe kwa wenyewe. Hayo yametokana na mipango yake ya kufanya mageuzi katika jeshi kwa gharama za chini. Japo ilishatambulika siku nyingi kuwa askari zaidi wanahitajika nchini Irak.

Na sasa rais Bush amemwondoa waziri wake, Donald Rumsfeld kufuatia kushindwa katika uchaguzi wa bunge. Lakini uchaguzi huo umeonesha kuwa wananchi wa Marekani wanataka sera mpya juu ya vita vya Irak na siyo sura mpya .!

Imetafsiriwa na Abdu Mtullya