1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kumbukumbu ya Kofi Annan: Msuluhishi hodari na mtu makini

Zainab Aziz
18 Agosti 2018

Kofi Annan kwa miaka 10 alikuwa kwenye kilele cha siasa za ulimwengu. Aliendelea kufanya kazi kama balozi wa amani hata baada ya kuondoka kwenye nafasi ya ukatibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/33Mez
Kofi Annan ist verstorben
Picha: Reuters/D. Balibouse

Kofi Annan mtu mwenye umbo dogo na ndevu za kijivu, akitabasamu nyuma ya meza yake ya kazi huko jijini New York wakati fulani aliikumbuka siku yake ya kwanza kama katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa na kuifananisha na siku yake ya kwanza shuleni.

Alizaliwa katika familia maarufu mnamo mwaka 1938 huko Kumasi, jiji la pili kwa ukubwa nchini Ghana. Baba yake alikuwa gavana wa jimbo la Ashanti chini ya utawala wa kikoloni wa Waingereza. Annan alihudhuria shule za daraja la juu nchini Ghana, Uswisi na baadaye Marekani.

Annan alijiunga na Umoja wa Mataifa akiwa na umri wa miaka 24, kwanza kufanya kazi kama msimamizi katika Shirika la Afya Duniani WHO na kisha akawa mkuu wa watumishi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa Misri, Cairo, baadae alihudumu kama naibu mkurugenzi wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR huko Geneva, Uswisi na hatimaye akawa naibu mkurugenzi wa Umoja wa Mataifa.

Katibu mkuu wa zamani wa Mataifa kofi Annan aliyeaga dunia tarehe 18.08.2018
Katibu mkuu wa zamani wa Mataifa kofi Annan aliyeaga dunia tarehe 18.08.2018Picha: Reuters

Mnamo 1993, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa wakati huo Boutros Boutros-Ghali alimteua Annan kuwa naibu katibu mkuu katika masuala ya kulinda amani, alisimamia jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa lililokuwa na askari 75,000 duniani kote.

Kama mkuu wa askari wa ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa, Annan alipata kibano cha kwanza katika kazi yake mwaka mnamo wa 1994 wakati wanamgambo wa Kihutu wenye msimamo uliokithiri walipowaua zaidi ya Watutsi 800,000 na Wahutu waliokuwa na msimamo wa wastani. Baadaye mauaji hayo yalitajwa  kama mauaji ya kimbari ya Rwanda.

Annan alilaumiwa kwa kushindwa kutoa msaada wa kutosha katika nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika licha ya onyo la awali juu ya kuongezeka kwa ukatili lililotolewa na Romeo Dallaire, mkuu wa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa nchini Rwanda.

Kusita kwake kulitokana na ukweli kwamba Marekani na Ulaya zilionekana kuwa na maslahi madogo ya kujihusisha au kushiriki katika masuala ya Rwanda.

Annan aliomba radhi kwa niaba ya Umoja wa Mataifa miaka 10 baadaye kwa kusema: "Jumuiya ya kimataifa imeshindwa kuinusuru Rwanda, na hiyo inatupasa daima kuwa na hisia za majuto, uchungu na huzuni ya kudumu."

Msuluhishi wa amani asiyekata tamaa

Mauaji ya kimbari ya Rwanda hayakusitisha kuendelea kukwea katika nyadhifa za juu kwa Kofi Annan katika Umoja wa Mataifa. Alichaguliwa kuwa katibu mkuu mnamo Desemba mwaka 1997, baada ya Marekani kushinikiza, na hivyo akawa Mwafrika wa kwanza kutoka eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara kuchukua nafasi hiyo.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, alieleza kuwa hakutaka tu kufanya kazi za utawala kama mkuu wa Umoja wa Mataifa lakini pia alitaka kuunda upya siasa za kimataifa. Ajenda yake ilikuwa ni pamoja na kupambana na umaskini wa kimataifa, kiwango cha kuongezeka joto duniani, na UKIMWI, na pia ufumbuzi wa migogoro ya kisiasa.

Boutros Boutros-Ghali katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa
Boutros Boutros-Ghali katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa MataifaPicha: Imago/Xinhua

Baadaye, alieleza kuhusu kusainiwa kwa Malengo ya Maendeleo ya Milenia ya mwaka 2000 kuwa ni kielelezo kikuu cha kipindi chake katika ofisi. Annan pia alisimama kama mwakilishi katika mgogoro wa Cyprus na Iran juu ya mpango wake wa nyuklia. Alikuwa mkosoaji mkubwa wa mashambulizi yaliyofanywa na wanamgambo wa Sudan Janjaweed katika jimbo la Darfur.

Mwaka wa 2001, Kamati ya tuzo ya kimataifa ya Amani ya Nobel ya Norway iliitambua michango ya Annan, na kumtunukia yeye na Umoja wa Mataifa kwa Tuzo ya Amani ya Nobel.

Mwenyekiti wa jopo la Oslo, Gunnar Berge, aliiambia DW katika mahojiano kwamba Kofi Annan alikuwa mwakilishi bora wa Umoja wa Mataifa na pengine katibu mkuu aliyefanya kazi kwa ufanisi mkubwa kabisa katika historia ya Umoja wa Mataifa.

Kofi Annan raia wa Ghana, aliyeishi nchini Uswisi, alikuwa mwanadiplomasia, mpole na mtu makini. Aliaga dunia mjini Geneva, uswisi Jumamosi tarehe 19.08.2018 baada ya kuugua kwa muda mfupi. Amemwacha nyuma mkewe bi Nane na watoto Ama, Kojo na Nina waliyekuwa pamoja naye wakati umauti ulipomfika.

Mwandishi: Zainab Aziz/DW

Mhariri: Lilian Mtono.