1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kupotea kwa Serengeti - Ardhi ya Wamaasai

Josephat Charo
15 Mei 2018

Ripoti mpya iliyotolewa na Taasisi ya Oakland mjini Carlifonia nchini Marekani inafichua jinsi kampuni zinazoratibu safari za watalii zinavyotumia machafuko na vitisho kudhibiti ardhi nchini Tanzania.

https://p.dw.com/p/2xVoo
Tanzania - Serengeti und Loliondo
Picha: DW/A. Mittal

Ripoti hiyo iliyopewa jina "Losing the Serengeti, The Maasai Land that was to be run forever - Kuipoteza Serengeti - Ardhi iliyotakiwa kuwepo milele, inaziangazia kampuni mbili moja ikiwa ni Ortelo Business Corporation, OBC, kampuni inayoendesha shughuli za uwindaji wa wanyamapori kwa niaba ya familia ya kifalme yenye makao yake makuu katika Umoja wa Falme za Kiarabu, na nyingine ni Tanzania Conservation Limited, TCL, ambayo ni kampuni ya biashara inayoratibu safari za watalii inayoendeshwa na wamiliki wa kampuni ya Thomson Safari yenye makao yake mjini Boston nchini Marekani.

Suala nyeti linaloibua wasiwasi ni kwamba jamii ya Wamasai wana haki waliyorithi ya umiliki wa ardhi ya Serengeti, neno la kimasai ambalo maana yake ni ardhi iliyotakiwa kuwepo milele. Swali linaloulizwa katika ripoti hiyo ni vipi haki hiii ilivyokanyagwa na kunyimwa Wamasai, kiasi kwamba leo hawaruhusiwi hata kulima na kupanda vyakula katika mashamba madogo karibu na nyumba zao, jambo linalosababisha njaa inayoenea, utapiamlo na magonjwa. Hawana tena maeneo ya malisho kwa ajili ya mifugo yao. Ghafla mambo yamebadilishwa na swali linaloulizwa katika ripoti hiyo ni nani aliyepitisha maamuzi hayo, kufikia kiwango cha Wamaasai wakati mwingine kupewa vibaruwa na ajira katika kambi za watalii.

Anuradha Mittal, Mtafiti Mwandamizi wa taasisi wa Oakland mjini Carlifonia aliyehusika kufanya utafiti nchini Tanzania alisema, "Ripoti hii inaangazia jinsi Wamaasai wa Tanzania wanavyokabiliwa na ukiukaji wa haki za binadamu ikiwemo vitisho, kufukuzwa kwa nguvu kutoka makao yao, kukamatwa, kupigwa, na njaa. Na hii ni kutokana na sera za serikali ya Tanzania na baadhi ya makampuni yanayoratibu safari za watalii yanayoendesha shughuli zake nchini humo."

Uharibifu kwa kisingizio cha uhifadhi

Ripoti ya taasisi ya Oakland inaangazia hali katika maeneo ya Serengeti na Loliondo kaskazini mwa Tanzania. Watafiti wa taasisi hiyo wanatoa ushahidi kuhusu vijiji vinavyotambuliwa rasmi na serikali ya Tanzania, lakini kwa kisingio cha kushajiisha uhifadhi, Wamaasai hawaruhusiwi hata kuwa na vijishamba vidogo vya kukuza mboga nje ya nyumba zao. Wameahidiwa msaada wa chakula ambao haujawasili, kwa hiyo watu wanalazimika kutegemea vikombe viwili vya uji kwa siku unaotengenezwa kutokana na unga wa mahindi, bila maziwa kwa kuwa maziwa yanawekewa watoto, wanapofaulu kuwa nayo.

Ripoti inasema uharibifu huu unaofanyika kwa kisingizio cha uhifadhi na kuwafukuza Wamaasai kutoka kwenye ardhi yao unasababisha janga. Ripoti hii haihusu tu serikali au kampunifulani. Ukweli ni kwamba jamii za watu asili kote ulimwenguni katika maeneo mengi, serikali na kampuni kubwa kubwa na hata mashirika makubwa ya uhifadhi wa mazingia yanashirikiana kwa kisingizio cha uhifadhi na kuwalazimisha wakazi kutoka ardhi yao na kuwapokonya kipato chao.

Tanzania - Serengeti und Loliondo
Jamii ya Wamaasai wakiwapatia maji mifugo waoPicha: DW/A. Mittal

Anuradha Mittal afisa wa taasisi wa Oakland anasema ripoti yao haina nia ya kuichafulia jina serikali wala kampuni yoyote ile. "Hii haihusiani na kuifachulia jina serikali ya Tanzania wala kampuni fulani. Inachokigusia ripoti hii ni kuwa huku utalii ukiendelea kuwa moja wapo ya sekta zinazokua kwa kasi katika uchumi wa Tanzania, shughuli za safari za watalii na mbuga za wanyama zinavuruga maisha na kipato cha Wamaasai. Wamaasai wako wazi katika ripoti hii, wanasema hawataki ajira hizi, wanataka ardhi yao, wanataka waweze kuwalisha mifugo wao, wayafikie maji, haki ya msingi kwa wote."

Wamaasai wamewasilisha madai yao

Kwa mujibu wa ripoti hiyo jamii ya Wamasai imewasilisha mambo kadha wa kadha yanayotakiwa kufanyiwa kazi. Wanataka vitisho na hofu ya kutiwa mbaroni vikome mara moja. Bi Mittal amedokeza kuwa leseni ya uwindaji iliyotolewa kwa kampuni ya OBC ilifutwa na wizara mpya ya Tanzania inayohusika na raslimali, mali asili na utalii mnamo mwaka uliopita, lakini utafiti uliofanywa na taasisi ya Oakland umebaini kuwa bado kampuni hii inaendesha shughuli zake katika eneo hilo. Wamasai wanataka suala hilo lichunguzwe na kampuni ya OBC iamriwe kuondoka.

Bi Anuradha Mittal anasema,  "Matumaini yetu ni kuwa ripoti hii itakuwa ya msaada kwa serikali ya Tanzania na kampuni ya Tanzania Conservation Limited, TCL na OBC, ziheshimu haki za Wamaasai na kufanya wanachotakiwa kufanya. Badala ya wageni kuingia nchini na kutwaa ardhi ya watu ambao wamekuwa wakiishi hapo vizazi hadi vizazi."

Katika ripoti hiyo Wamaasai wamenukuliwa wakisema kuna watu wanaotishia kuzichoma nyumba zao wakidai ardhi ni yao. Wamaasai wanasema wamechoka kuishi kwa hofu katika ardhi yao. Mwaka 2009 vyombo vya habari viliripoti juu ya matukio ya maboma ya Wamaasai kuchomwa moto na watu kulazimishwa kuyahama makazi yao. Matukio mengine yakaripotiwa tena mwaka uliopita 2017 huku takriban Wamaasai takriban 20,000 wakiachwa bila makazi.

Mwandishi:Josephat Charo/https://www.oaklandinstitute.org/tanzania-safari-businesses-maasai-losing-serengeti/ Anuradha Mittal

Mhariri:Iddi Sessanga