1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya maoni jimbo la Crimea

16 Machi 2014

Wapigakura katika jimbo la Crimea leo wanapiga kura ya maoni kuhusiana na iwapo jimbo hilo lijitenge na Ukraine na kujiunga na Urusi, na kuzusha mzozo ambao ni sawa na uliokuwa wakati wa vita baridi.

https://p.dw.com/p/1BQRB
Krim Referendum / Plakat
bango la kampeni ya kura ya maoni CrimeaPicha: picture-alliance/dpa

Mzozo huo katika eneo hilo la pembe ya mashariki mwa bara la Ulaya umeiweka hali ya diplomasia katika mtafaruku.

Kiasi ya watu milioni 1.5 wanapiga kura katika eneo hilo, ambalo lina idadi kubwa ya watu wenye asili ya Urusi.

Uchaguzi ni kati ya kuwa sehemu ya Urusi ama kuchukua madaraka zaidi lakini kubakia Ukraine, lakini hakutakuwa na nafasi ya kuchakua kubakia kama ilivyo hivi sasa.

UN-Sicherheitsrat stimmt über Krim-Resolution ab
Baraza la usalama la Umoja wa mataifa limepinga kura hiyoPicha: Reuters

Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa saa 12 asubuhi na vitafungwa saa kumi na mbili jioni kwa saa za Ulaya ya mashariki, ambapo matokeo yatapatikana mara baada ya kufungwa vituo vya kupigia kura, licha ya kuwa kumekuwa na kauli mbiu inayosema "tuko Urusi" , mabango hayo yakiwa katika majengo ya serikali, hali ambayo inatoa ishara juu ya matokeo.

Mataifa ya magharibi

Mataifa ya magharibi yamesema hayataitambua kura hiyo ya maoni, wakati Urusi ikisisitiza kuwa ni mfano wa kuamua kujitawala kama ilivyofanya Kosovo.

Majeshi ya Urusi na wanamgambo wanaounga mkono Urusi wamedhibiti eneo hilo la rasi muda mfupi baada ya rais anayeungwa mkono na serikali ya Urusi Viktor Yanukovich kuondolewa madarakani mwezi uliopita baada ya miezi mitatu ya maandamano dhidi ya serikali yake ambayo yamesababisha umwagikaji wa damu.

Bildergalerie Krim Referendum 10.03.2014 Checkpoint
Ulinzi mkali kabla ya kura hiyo ya maoniPicha: Alisa Borovikova/AFP/Getty Images

Vituo vya kijeshi vya Ukraine katika eneo hilo, ambalo ni mahali Urusi ilipoweka meli zake za kivita tangu katika karne ya 18, vimezingirwa lakini hakuna mapambano ya silaha na haijafahamika ni nini kitatokea kwa vituo baada ya kura hiyo ya maoni.

Waandishi washambuliwa

Kumekuwa na mashambulizi kadha dhidi ya waandishi habari pamoja na wanaharakati wanaopendelea umoja , mashambulizi ambayo yameshutumiwa na shirika linalotetea haki za binadamu la Amnesty International kuwa yanatia wasi wasi mno.

Marekani imepuuzia kura hiyo ikiita "kura kwa mtutu wa bunduki" na serikali mpya ya Ukraine imeiita kura hiyo ya maoni kuwa ni batili na ina wasi wasi kuwa Urusi inajaribu kuchochea uasi mkubwa zaidi katika eneo lenye wakaazi wengi kutoka Urusi upande wa mashariki ya Ukraine.

Wanaharakati watatu wameuwawa katika miji wa mashariki ya Donetsk na Kharkiv muda kuelekea kura hii ya maoni kwa jimbo la Crimea na waungaji mkono wa Urusi wametoa wito wa kuwa na aina hiyo ya kura katika majimbo mengine ya Ukraine.

Russische Kriegsschiffe Krim 2013
Meli za kivita za Urusi katika rasi ya CrimeaPicha: imago/Russian Look/Fotoimedia

Wabunge wa Urusi wameidhinisha rais Vladimir Putin kuivamia Ukraine wakati akipenda , wakidokeza haja ya kuwalinda watu wenye asili ya Urusi dhidi ya watu wenye msimamo mkali wa kizalendo.

Ukraine iko katika hali kamili ya tahadhari kijeshi na katika mkesha wa kura hii ya maoni imeyashutumu majeshi ya Urusi kwa kukamata kijiji nje kidogo ya Crimea , ikisema, " Ukraine ina haki ya kutumia hatua zozote zinazowezekana kuzuwia uvamizi wa kijeshi wa Urusi.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Amina Abubakar