1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura zahesabiwa Gambia

2 Desemba 2016

Katika jumla ya asilimia 75 za kura ambazo zilihesabiwa mgombea wa upinzani Adama Barrow ameongoza kwa kushinda katika majimbo 22 ya uwakilishi bungeni kati ya maeneo 53.

https://p.dw.com/p/2Tcmw
Gambia Wahlen Yahya Jammeh
Picha: Getty Image/AFP/M. Longar

Vikosi vya usalama nchini Gambia vimeimarisha usalama huku kura zikiendelea kuhesabiwa baada ya uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali. Matokeo ya awali yanamweka mbele rais Yahya Jammeh ambaye alipoteza ushawishi katika jiji kuu ambalo lilikuwa ngome yake tangu zamani. Wananchi wamelalamika kwa kuzimwa kwa intaneti hivyo kulemaza mawasiliano na huduma za mitandaoni.

Shughuli ya kuhesabiwa kura katika taifa hilo la Afrika Magharibi, imeendelea polepole tangu upigaji kura ulipokamilika jana. Hadi tukienda hewani katika jumla ya asilimia 75 za kura ambazo zilihesabiwa mgombea wa upinzani Adama Barrow alikuwa akiongoza kwa kushinda katika majimbo 22 ya uwakilishi bungeni kati ya maeneo 53. Hayo ni kwa mujibu wa tume huru inayosimamia uchaguzi nchini humo. Rais Jammeh alikuwa ameshinda katika maeneo bunge 14.

Haya yanafanyika huku intaneti katika nchi hiyo ndogo ikiwa imezimwa. Hatua ambayo imeshutumiwa na Marekani na makundi ya kutetea haki za binadamu pamoja na baadhi ya raia. Chunro Jallow, ambaye ni msanii nchini humo amesema."Sijui kwa nini wamezima intaneti. Watu wengi wanajikimu kimaisha kwa kutoa huduma za intaneti . Kwa maoni yangu hawapaswi kuzimia watu internet bali waachilie watu. Kwa hivyo kwa ndugu na dada zangu, wale wanaosema mambo mbalimbali, hii nchi imebarikiwa. Hakuna litakalofanyika. Wacheni kila mtu akae kwa amani."

Raia wa gambia karibu na kituo cha upigaji kura
Raia wa gambia karibu na kituo cha upigaji kuraPicha: picture alliance/AP Photo/J. Delay

Mawasiliano ya internet zimwa

Upinzani umekuwa ukitegemea pakubwa huduma za mitandao kufikisha ujumbe wa mikutano yao. Waziri wa habari Sheriff Bojang alisema kuwa kuzimwa kwa huduma za mitandao kunalenga kukinga usambazaji wa habari potofu kuhusu matokeo hivyo kuitaja kama mkakati wa kiusalama.

Kiongozi wa upinzani Adama Barrow ambaye ni mshindani mkuu wa rais Jammeh alipata ushindi katika jiji kuu Banjul kwa asilimia 50 dhidi ya rais Jammeh anayewania muhula wake wa tano kupitia chama chake cha Alliance for Patriotic Reorientation and Construction APRC, aliyepata  asilimia 43. Jiji hilo limekuwa ngome ya Jammeh tangu zamani. Mgombea wa tatu Mama Kandeh alipata asilimia 7.6.

Kabla ya kupambazuka leo wakati raia wakilala huku wengine wakifuatilia kuhesabiwa kwa kura kupitia runinga, wanajeshi na maafisa wa polisi ambao baadhi yao walijifunika nyuso, waliweka vizuizi barabarani kila baada ya mita mia moja nje ya jiji kuu.

Katika mkutano wake wa mwisho wa kampeni, rais Jammeh alionya kuwa maandamano yoyote kuhusu matokeo ya uchaguzi huo hayataruhusiwa. Mshindi miongoni mwa wagombea hao watatu ataihudumia nchi hiyo ndogo kwa miaka mitano.

Mwandishi: John Juma/AFPE/DPE

Mhariri: Josephat Charo