1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kurejeshwa adhabu ya kifo Pakistan kwawapa wasiwasi Amnesty

24 Desemba 2014

Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif ametangaza kurejeshwa adhabu ya kifo kwa kunyongwa, kwa watakaokutwa na hatia ya ugaidi ingawa Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International linapinga sheria hiyo.

https://p.dw.com/p/1E9az
Pakistan Taliban-Überfall auf Schule in Peshawar 16.12.2014
Mashambulizi ya Taliban ya shule Peshawar, PakistanPicha: Reuters/K. Parvez

Pakistan imetoa uamuzi wa kurejesha sheria ya kunyonga watakaokutwa na hatia ya ugaidi. Hatua hiyo ilitangazwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Nawaz Sharif, siku moja baada ya mashambulizi yaliyofanywa na wanamgambo wa Taliban na kusababisha vifo vya watu 150, wakiwemo wanafunzi 135. Mashambulizi hayo yalitokea tarehe (16.12.2014), katika shule inayomilikiwa na jeshi ilioko mjini Peshawar.

Lakini makundi ya kutetea haki za binadamu yanasema kurejeshwa kwa adhabu ya kifo, hakutaisaidia Pakistan kupambana na Ugaidi.

Azimio hilo lilipitishwa bila ya pingamizi tarehe (17.12.2014), katika mkutano uliojumuisha vyama vyote vya siasa vya nchi hiyo. Pakistan imesema kuwa kurejesha kwa sheria ya kunyonga walio na hatia ya ugaidi ni hatua muhimu, kwani katu haiwezi kuonyesha huruma yoyote kwa wale wanaohusika na matendo ya ugaidi na kuua watu wasio na hatia.

“Nimetangaza kurejeshwa kwa sheria ya adhabu ya kifo leo, na taifa zima liko pamoja na sisi,” alisema Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif.

Tangu tangazo hilo kutolewa na serikali ya Pakistan, watu wanne tayari wameshanyongwa katika jimbo la Punjab. Watu hao walikutwa na hatia za kushiriki katika mashambulizi dhidi ya Rais wa zamani Jenerali Pervez Musharraf, mwaka 2003 na Jenerali wa Makao Makuu ya Jeshi la Pakistan mwaka 2009.

Hata hivyo, Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema kuanza tena kunyonga watu baada ya sheria hiyo kusimamishwa mwaka 2008 sio suluhisho ya kuzuia matatizo ya ugaidi.

David Griffiths Amnesty International
David Griffiths wa Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty InternationalPicha: Amnesty International

“Hii ni hatua ya kijinga. Serikali inataka kuficha kushindwa kukabiliana na suala la msingi lililooneshwa na mashambulizi ya Peshawar, yaani ukosefu wa ulinzi madhubuti kwa raia wa maeneo ya kaskazini-magharibi mwa Pakistan," alisema Naibu Mkurugenzi wa Amnesty International wa Asia-Pacific David Griffiths katika taarifa yake.

Aliongeza kwa kusema, adhabu ya kifo inakiuka haki za kibinaadamu. Hali hii inatupa wasiwasi mkubwa , kwani itasababisha ukiukwaji wa sheria mbalimbali za kimataifa wakiendelea kutekeleza mpango wao.

Lakini serikali kwa upande wake imejitetea kwa kusema kuwa nchi hio ipo katika wakati mgumu wa kupambana na ugaidi, hivyo hakuna njia nyengine bali kurejesha sheria ya kunyonga, huku makundi ya kidini pamoja na ya kisiasa yakikubaliana na uwamuzi huwo wa serikali.

"kunyongwa kwa magaidi wawili tarehe 19 Disemba ilikuwa ni ushindi kwa sheria ya nchi," Rais wa zamani wa Pakistan Jenerali Musharraf aliliambia shirika la habari la IPS, na kuongeza " Hatimaye serikali imewatendea haki magaidi."

Pakistan ina wafungwa 8000 ambao wamekuwa wakisubiri adhabu ya kifo tangu mwaka 2008. 17 kati yao walifungwa kwa mashtaka ya ugaidi, na adhabu yao ya kifo kwa kunyongwa itatekelezwa katika siku saba zijazo.

"Kutokana na hali ilivyo nchini humo, maisha ya watu wengi yapo hatarini. Serikali ya Pakistan inalazimika kufuta tena sheria ya adhabu ya kifo," alionya Griffiths wa shirika la Amnesty International.

Mwandishi: Yusra Buwayhid

Mhariri: Gakuba Daniel