1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Kutana na Sarah Baartman kutoka Cape Town Afrika Kusini

Sylvia Mwehozi
25 Julai 2018

Kutana na Sarah Baartman kutoka mjini Cape Town Afrika Kusini mwaka 1810. Mwanamke mdogo wa Khoikhoi aliyefanya kazi katika nyumba ya "mtu huru mweusi". Alitumikishwa kama mnyama na kuwa muhanga wa ubaguzi wa kisayansi. Alikufa akiwa maskini katika umri wa miaka 55. Kwa zaidi ya karne wageni wa makumbusho ya taifa ya Ufaransa, waliutizama ubongo wake, mifupa na viungo vya uzazi.

https://p.dw.com/p/2rh1d

Sarah Baartman aliishi miaka gani?

Sarah Baartman ambaye pia akifahamika kama Saartjie Baartman alizaliwa kiasi kama mwaka 1789 katika eneo la mto Gamtoos katika kile ambacho sasa Waafrika Kusini wanakiita mkoa wa Cape Mashariki. Alikuwa akitokea kwenye jamii ya watu wa Khikhoi. Aliachwa mtoto yatima akiwa na umri mdogo kabisa, Baartman alihamia mjini CapeTown ambako alifanya kazi kama mtumishi wa ndani kwa mtu mweusi aliyekuwa akiishi kwa uhuru na baadae alihamia ulaya pamoja na mwajiri wake huyo. Baada ya kuitembelea Uingereza alikwenda  nchini Ufaransa mjini Paris ambako baadaye alikufa akiwa ni mtu maarufu kabisa lakini masikini mnamo mwaka 1815. 

Kitu gani kilichompa Umaarufu Sarah Baartman?

Barani Ulaya alioneshwa kama kiumbe cha aina yake kinachovutia. Maumbile yake ambayo hayakuwa ni kitu kipya kwa wanawake wa  jamii ya Khoikhoi ya Afrika Kusini, yaliangaliwa kwa jicho tafauti nchini Uingereza na Ufaransa: Baartman alikuwa na kiuno chembamba na makalio makubwa na viungo vikubwa vya sehemu zake za siri. Alipachikwa jina ''Mungu wa mapenzi wa Khoikhoi''.

African Roots Sarah Baartman
Picha: Comic Republic

Je Sarah Baartman alikuwa mhanga wa ubaguzi?

Sio wazi ikiwa alisafiri kwenda London kwa ridhaa yake au ikiwa alilazimishwa. Na wala haifahamiki hasa ni kwa kiasi gani alikuwa na usemi kama mtu binafsi pale alipokuwa akihitajika kujionesha mbele ya watazamaji. Lakini bila shaka Baartman alikuwa mhanga kutokana na nadharia ya ubaguzi iliyokuwa imetawala mitazamo ya watu wa Ulaya kuhusu dunia katika kipindi cha mwanzoni mwa karne ya 19. Kwa ujumla kufuatia tamaduni na kibayologia  waafrika walikuwa wakitazamwa kuwa viumbe ambavyo havijaendelea. Baada ya kifo chake mtaalamu maarufu chini ya utawala wa Napoleon, kuhusu masuala ya viumbe asili na wanyama Georges Cuvier alivitenganisha viungo vya mwili wa Baartman na kujiridhisha kwamba alikuwa ana maumbile yaliyofanana na yale ya sokwei. Kwa takriban miaka 160 mabaki ya Baartman yamekwa katika makumbusho ya kitaifa ya Ufaransa mjini Paris na kumfanya kiumbe huyo kuwa mhanga wa ubaguzi wa kisayansi.

Sarah Baartman aliwahi kurudi tena Afrika Kusini?

Baada ya kumalizika kwa utawala kulionekana hamu ya kulifufua suala la kisa cha Baartman. Afrika Kusini chini ya Nelson Mandela ilianza kupambana kutaka mabaki yake yarudishwe nchi humo. Lakini ilikwenda hadi mwaka 2002 ndipo mabaki hayo hatimae yaliporudishwa nyumbani. Maziko yake nyumbani kwao katika mkoa wa Cape Mashariki ndiyo yaliyokifikisha mwisho kipindi cha takriban karne mbili za Baartman kuweko nje ya nchi yake.

DW Videostill Projekt African Roots | Sarah Baartman, Südafrika
Picha: Comic Republic

Je anakumbukwa vipi leo hii?

Mapambano ya kupigania Baartman arudishwe nyumbani yalikuwa ni mapambano dhidi ya vurugu za kibaguzi.  Ushindi aloupata baada ya kifo chake Sarah Baartman anabakia kuwa nembo ya ushidni dhidi ya ukandamizaji kwa waafrika Kusini leo hii. Wilaya alikotokea huko Mkoa wa Cape Mashariki imepewa jina lake Sarah Baartman. Mjini CapeTown waafrika Kusini wanamkumbuka kwa kuweko kituo kinachofahamika kama Saartjie Baartman kituo cha wanawake na watoto kinachoshughulikia wale walionusurika udhalilishaji.


Mwandishi:Jane Ayeko-Kummeth/Thuso Khumalo/Gwendolin Hilse

Tafsiri: Saumu Mwasimba
Mhariri: Mohammed Khelef


Jane Ayeko-Kümmeth, Thuso Khumalo na Gwendolin Hilse wamechangia katika makala hii. Ni sehemu ya makala maalum za  mfululizo wa "Asili ya Afrika", ushirikiano kati ya shirika la DW na taasisi ya Gerda Henkel.