1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuwawa kwa Kiongozi wa Hamas Dubai

17 Februari 2010

Timu ya wauaji 11 inasakwa.

https://p.dw.com/p/M3lj
Dubai Burj DubaiPicha: picture-alliance/ dpa

Polisi ya Dubai, katika Umoja wa Falme za Kiarabu, iliwahoji jana wapalestina 2 kuhusu mauaji ya Kiongozi mashuhuri wa chama cha Hamas.Hii imefuatia hatua ya Dubai, kuitaja timu ya wauaji 11 waliosafiri na kuingia Dubai na pasi za nchi tofauti za ulaya zinazobainika ni bandia.

Wapalestina hao 2 waliohujiwa wote wakaazi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Emirates) "walikimbilia Jordan" mara tu baada ya Bw.Mahmud al-Mabhuh, kukutikana amefariki katika hoteli moja ya Dubai mwezi uliopita-hii ni kwa muujibu alivyoliambia shirika la habari la AFP , mkuu wa polisi Dahi Khalfan.Alisema kuwa, kuna shaka shaka nyingi kuwa mmoja kati ya wapalestina hao 2 alikutana na mmoja wa timu hiyo ya wauaji kabla ya kitendo chenyewe kufanyika.

Khalfan alitangaza juzi Jumatatu kuwa ,Polisi ya Dubai, inawasaka watu 6 walioingia Dubai na paspoti za Uingereza,watatu wengine wenye pasi za Ireland,miongoni mwao mwanamke mmoja na mmoja mwenye pasi ya kijerumani na mwengine mwenye pasi ya Ufaransa.Wote hao waliweza kuondoka Umoja wa Falme za Kiarabu baada ya mkasa huo.

Maafisa wa Uingereza,Ireland na Ufaransa, waliarifu hapo jana kuwa pasi hizo ni feki au za udanganyifu.Vyombo vya habari vya Israel, vimetangaza kwamba kiasi ya waisraeli 6 wenye uraia wa nchi 2-Uingereza na Israel wamo katika orodha ya kundi hilo la watu 11.

Mjini Dublin,msemaji wa wizara ya nje amesema pasi hizo zinazosemekana kuwa za Ireland si za kweli. Akaongeza kusema kwamba, wamechunguza nambari za pasi na majina na kugundua hakuna pasi za majina hayo wala nambari hizo.

Msemaji wa wizara ya nje ya Ufaransa, Bernard Valero, ameliambia shirika la habari la AFP baada ya uchunguzi kufanywa kuwa wamegundua hata pasi ya kifaransa iliotumika si ya kweli.

Nchini Israel, kituo cha TV cha Channel 10 kimearifu kwamba ,waisraeli 6 na muisraeli mwenye uraia wa kijerumani wamekuwa wahanga wa njama hiyo.Kituo cha TV cha channel 2, kimetaja waisraeli 4 tu wenye uraia wa nchi 2 na kwamba picha zao tu zimebadilishwa.

Chama cha wapalestina cha HAMAS kinachotawala mwambao wa Gaza ,kimeituhumu Israel ndio iliomuua bw.Mahmud Mabhuh,aliekuwa na umri wa miaka 50 na kikaahidi kulipiza kisasi.

Wanachama wa HAMAS wamearifu kwamba, Mabhuh aliepiga maskani yake mjini Damascus,Syria, alikuwa ziarani huko Dubai kwa madhumuni ya kununua silaha kwa ajili ya tawi la kijeshi la chama cha HAMAS ambalo yeye ndie aliolianzisha.

Juzi Jumatatu, msemaji wa kikosi cha polisi cha Mamlaka ya ndani ya Palestina,jamadari Adnan al-Dameeri, aliliambia shirika la habari la AFP huko Ramallah kuwa, wakuu wa usalama wa kipalestina wamethibitisha taarifa kuwa maafisa 2 wa Hamas, walihusika na mauaji ya Mahmud Mabhuh.

Wauaji wa Mabhuh, waliondoka Dubai masaa tu baada ya mauaji baada ya kupitisha masaa 24 tu huko Dubai na hawakutumia silaha yoyote,wala (credit cards ) au simu za Dubai wakati walipokuwa huko.Picha za timu hiyo ya wauaji 11 zilioneshwa baada ya kuchukuliwa na kamera za upelelzi.

Mwandishi: Ramadhan Ali /AFPE

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed