1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Laurent Gbagbo akana mashtaka ICC

Isaac28 Januari 2016

Rais wa zamani wa Cote d'Ivoire Laurent Gbagbo amekana kuwa na hatia katika mashataka manne ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu katika mahakama ya ICC, miaka mitano baada ya nchi yake kukumbwa na vurugu za uchaguzi.

https://p.dw.com/p/1Hl8D
Elfenbeinküste Präsident Laurent Gbagbo
Picha: Reuters/L. Gnago

Gbagbo pamoja na aliyekuwa waziri wake wa vijana Charles Ble Goude wote wawili wameyakanusha mashtaka yanayowakabili kuhusiana na kuhusika kwao katika machafuko yaliyotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2010 ambayo yalisababisha vifo vya watu 3,000 nchini humo. Charles Ble Goude amekanusha mashtaka dhidi yake akisema hayatambui.

Gbagbo mwenye umri wa miaka 70 pamoja na waziri huyo wa zamani wa vijana ambaye anadaiwa kuwa mshirika wake wa karibu wote wanakabiliwa na mashitaka manne ya ukiukaji wa haki za binadamu yakiwemo ya mauaji na ubakaji yanayodaiwa kufanywa na wanajeshi watiifu kwa rais huyo wa zamani mwishoni mwa mwaka 2010 na mapema mwaka 2011 baada ya kushindwa katika uchaguzi uliomuweka madarakani Rais Alassane Ouattara.

Bensouda akanusha uvumi kuhusu mashahidi

Awali mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC Fatou Bensouda alisema lengo la kesi hiyo ni kuhakikisha kuwa inafichua ukweli kupitia njia za kisheria na kukanusha uvumi ulioonea kuwa kuna mashahidi wa uapande wa mashitaka katika kesi hiyo waliojitoa.

"Ningependa kutahadharisha dhidi ya uvumi ulionea. Kwa bahati mbaya nchini Cote d'Ivoire umeenea uvumi uliolenga kuwababaisha wananchi nchini na ngambo," alisema Bensounda. Ndio maana nataka kuweka wazi kabisa kuhusiana na habari za uwongo zinazoenezwa na mitandao ya kijamii. Hakuna hata shahidi mmoja wa upande wa mashitaka aliyejitoa. Kinyume na baadhi ya uvumi, hatuijawahi hata mara moja kufikiria uwezekano wa kuahirisha tarehe ya kufunguliwa kesi."

Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Fatou Bensouda.
Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Fatou Bensouda.Picha: picture-alliance/dpa

Jiji la Abidjan, moja ya majiji maarufu barani Afrika lilitumbukia katika vita katika kipindi cha kati ya mwaka 2010 na 2011 baada ya mapambano yaliyohusisha wapiganaji wapande zote mbili.

Jumuiya ya kimataifa ikiwemo Ufaransa ambayo Ivory Coast ilikuwa chini ya himaya yake wakati wa utawala wa kikoloni ilimuunga mkono Alassane Ouattara kama mshindi halali katika uchaguzi huo hatua iliyofuatiwa pia na kukamatwa kwa Gbagbo na vikosi tiifu kwa Ouattara kwa msaada wa vikosi vya Umoja wa Mataifa pamoja na Ufaransa na baadaye kufunguliwa mashitaka katika mahakama hiyo ya uhalifu ya kimataifa ya ICC.

Wakili asema ni kesi muhimu

Wakili wa Gbagbo, Emmanuel Altit alisisitiza siku ya Jumatano kuwa hiyo ni kesi muhimu sana kwa Cote d`Ivoire na Afrika kwa ujumla na kwamba itasaidia kuweka bayana ukweli wa mambo kuhusiana na machafuko hayo yaliyotokea nchini humo katika kipindi hicho.

Wafuasi wa mtawala huyo wazamani wa taifa linaloongoza kwa uzalishaji wa zao la kakao duniani wamekuwa wakiishutumu Ufaransa kwa kuhusika moja kwa moja na mipango ya kumuondoa madarakani Gbagbo na kudai kuwa haki haijatendeka kwa pande zote zilizohusika katika machafuko hayo kwa vile upande wa Alassane Ouattara haujahojiwa na vyombo vya kisheria kuhusiana na machafuko hayo.

Wakili wa Gbagbo Emmanuel Altit.
Wakili wa Gbagbo Emmanuel Altit.Picha: picture-alliance/dpa/P. Dejong

'Pande zote zilihusika katika machafuko'

Makundi ya haki za binadamu yamekuwa pia yakidai kuwa pande zote mbili zilizokuwa na ushindani mkubwa katika uchaguzi huo zilihusika katika machafuko hayo ingawa hadi sasa hakuna mashitaka yoyote yaliyokwisha funguliwa dhidi ya upande wa Rais Ouattara ambaye alishinda muhula wa pili wa uzongozi wa taiafa hilo.

Hata hivyo upande wa utetezi wa Gbagbo umekuwa ukiendelea kukanusha kuwa kulikuwa na mpango wa makusudi wa kuondoa utulivu nchini humo na kusisitiza kuwa kiongozi huyo wa zamani wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi hana hatia na alitoa mchango mkubwa kwa kusimamia demokrasia kupitia mfumo wa vyama vingi nchini humo.

Mwandishi: Isaac Gamba/ ape

Mhariri: Yusuf Saumu