1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lawama za Trump dhidi ya Merkel zakosolewa

Oumilkheir Hamidou
17 Januari 2017

Kansela Angela Merkel amejibu lawama za rais mteule wa Marekani Donald Trump dhidi ya siasa yake ya kiliberali kuelekea wakimbizi na tuhuma zake dhidi ya jumuiya ya kujihami ya NATO anayosema "imepitwa na wakati".

https://p.dw.com/p/2VuIc
Klausurtagung CDU-Bundesvorstand - Merkel
Picha: picture-alliance-dpa/O. Dietze

"Nnaamini sisi wa-Ulaya, mustakbali wetu tunao mikononi mwetu. Nitaendelea kwa nguvu kufanya juhudi na kuhakikisha mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya tunaendelea kushirikiana kwa kuzingatia sera zinazotilia maanani hali ya siku za mbele. Nguvu za kiuchumi na maamuzi ya maana ya kimkakati, kufikiwa malengo pamoja na kupatiwa ufumbuzi changamoto za karne ya 21."

Amesema kansela Angela Merkel akijibu lawama za rais mteule wa Marekani kuhusu wimbi la wakimbizi ambalo Trump amelitaja kuwa ni kosa kubwa kupita kiasi."

Kuhusu lawama za Trump dhidi ya jumuiya ya jumihami ya NATO ambayo Trump anasema imepitwa na wakati, kansela Merkel anajibu: "Msimamo wangu  kuhusu jumuiya ya kujihami ya NATO unajulikana. Rais mteule wa Marekani amefafanua msimamo wake kwa mara nyengine tena. Tutaangalia atakapokabidhiwa uongozi, kwa sababu kwa sasa bado, na bila ya shaka tutashirikiana na serikali mpya ya Marekani. Hapo ndipo tutakapojua makubaliano ya aina gani tunaweza kuafikiana."

Lawama za Trump hazina maana anasema John Kerry

Rais wa Ufaransa Francois Hollande ameshadidia msimamo wa kansela Merkel na kusema Ulaya haihitaji ushauri kutoka nje.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani anayemaliza muhula wake, John Kerry amezitaja lawama za Trump kuwa "hazina maana" na kumtaja kansela Merkel kuwa kiongozi jasiri.

Katika wakati ambapo kansela Merkel amemtuma mmojawapo wa washauri wake wakubwa nchini Marekani kuzungumza na maafisa wa serikali mpya, serikali mjini Berlin inasema hakuna mipango yoyote ya mkutano kati ya kansela Merkel na Donald Trump.

Katika mahojiano na maripota wa magazeti ya Times la Uingereza na Bild la Ujerumani, rais mteule wa Marekani Donald Trump ametishia kuyatoza ushukuru mkubwa makampuni ya magari ya Ujerumani yanayouza magari yao Marekani ikiwa yataendelea kufungua viwanda vya magari ng'ambo, ameonya pia mataifa mengine yatafuata mfano wa Uingereza na kujitoa katika Umoja wa Ulaya.

Vitisho vya Trump havaimshitui waziri wa fedha wa Ujerumani

Hisa za makampuni ya magari ya Ujerumani zilitetereka kidogo baada ya Trump kutishia kuyatoza ushuru wa asilimia 35 magari yatakayoingizwa Marekani na hasa kutoka Mexico. Waziri wa fedha wa serikali kuu ya Ujerumani Wolfgang Schäuble anasema hatilii maanani vitisho vya Trump vya kuyatoza makampuni ya magari ya Ujerumani ushuru mkubwa.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa

Mhariri:Josephat Charo