1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Le Pen anaweza kushinda uchaguzi wa Ufaransa

17 Novemba 2016

Waziri Mkuu wa Ufaransa Manuel Walls amesema kiongozi wa sera kali za mrengo wa kulia Marine Le Pen ana fursa ya kushinda uchaguzi wa rais mwakani kutokana na msukumo wa ushindi wa fadhaa wa Donald Trump Marekani.

https://p.dw.com/p/2SqlC
Brexit Reaktionen Archivbild Marine Le Pen
Marine Le Pen kiongozi wa chama cha National Front.Picha: Reuters/H.-P. Bader

"Inawezekana" hivyo ndivyo alivyojibu waziri mkuu huyo wa Ufaransa Manuel Valls wakati alipoulizwa katika mkutano wa uchumi mjini Berlin Alhamisi (17.11.2016) iwapo mgombea wa chama kinachopinga uhamiaji nchini Ufaransa cha National Front Marine Le Pen anaweza kushinda uchaguzi huo kwa kuzingatia kile kilichotokea Marekani kwa ushindi wa Trump.

Le Pen anawekewa matumaini makubwa ya kuingia duru ya pili ya uchaguzi huo hapo Mei 7 ambapo aidha atakabiliana na mgombea wa chama kikuu kilichozoeleka kiwe cha mrengo wa kulia au kushoto.

Valls anasema jambo hilo limaanisha urari wa kisiasa utabadilika kabisa na kuonya juu ya hatari inayotokana na sera kali za mrengo wa kulia.

Wasi wasi umekuwa ukiongezeka nchini Ufaransa kwamba wimbi lile lile la sera kali za mrengo wa kulia na ghadhabu za kupinga utandawazi ambalo limemuingiza Trump Ikulu linaweza kumkabidhi Le Pen funguo za Kasri la Elysee yaani Ikulu ya Ufaransa.

Hatari ilioko Ufaransa

Deutschland Manuel Valls Wirtschaftsgipfel der Süddeutschen Zeitung
Waziri Mkuu wa Ufaransa Manuel Valls akizungumza katika mkutano wa uchumi mjini Berlin 17.11.2016.Picha: Getty Images/AFP/J. MacDougall

Valls amekiri kwamba kuna hatari nchini Ufaransa na kushtushwa na kauli zinazosikika katika midahalo ya umma.Amesisitiza kwamba kuna tafauti kati ya Trump na Le Pen kwa kusema kwamba tajiri huyo wa Marekani alikuwa mgombea wa chama kikuu juu ya kwamba kauli zake na mapendekezo yake yalikuwa yakizusha mashaka.

Kukabiliana na ghadabu zilizopelekea Uingereza kufikia uamuzi wa kujitowa Umoja wa Ulaya na ushindi wa uchaguzi wa Trump Waziri Mkuu huyo wa Ufaransa amesihi kuwepo kwa mtizamo mpya katika suala la utandawazi ambapo amesema yeye binafsi anaunga mkono aina ya utandawazi ambao unawatumikia wananchi.

Leo jioni wagombea wa sera za mrengo wa kulia watashiriki katika mdahalo wa mwisho kati ya midahalo mitatu kabla ya duru ya kwanza ya uchaguzi wa mchujo wa kumteuwa mgombea wao ambaye anategemewa sana kushinda katika uchaguzi wa rais hapo mwakani.

Suala la ushindi wa Trump unamaanisha nini kwa chama cha Le  Pen cha National Front linatazamiwa kujitokeza sana katika mdahalo huo.

Uzoefu ni muhimu

Schweiz Emmanuel Macron
Waziri wa uchumi wa zamani Emmanuel Macron.Picha: picture alliance/dpa/J.-C. Bott

Hapo jana Emmanuel Macron waziri wa uchumi wa zamani katika utawala wa rais Francois Hollande aliekuwa akin'gara  ametangaza kujibwaga katika kinyan'ganyiro hicho ingawa Hollande mwenyewe bado hakusema iwapo atawania muhula wa pili.

Akimzungumzia mgombea huyo Walls anasema "Uzoefu unahitajika.Uzoefu ulioandama na mitihani.Kunahitajika nguvu sio kuyachukulia mambo kwa wepesi. Madaraka ni maadili ya wajibikaji. Ni kujuwa namna ya kuvumilia, kujuwa maana ya utashi wa jumla na utashi wa jamii na kukataa kufuata njia ya kibinafsi."

Rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy na waziri mkuu wa zamani Alain Juppe wanadai  wako katika nafasi nzuri ya kumzuwiya Le Pen asiingie madarakani, kwa upande wa Sarkozy kwa kuchukuwa baadhi ya fikra za chama National Front kuhusu uhamiaji na Uislamu na kwa upande wa Juppe kwa kujaribu kuwaunganisha wapiga kura wa Ufaransa dhidi ya mama huyo.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AFP/

Mhariri :Gakuba Daniel