1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leipzig yashindwa kuiwekea mbinyo Bayern mbio za ubingwa

Bruce Amani
15 Machi 2021

RB Leipzig iliwapiga jeki vinara Bayern Munich katika mbio za ubingwa wa Bundesliga wakati walipobanwa kwa sare yya 1 – 1 nyumbani dhidi ya nambari nne kwenye Eintracht Frankfurt.

https://p.dw.com/p/3qepq
Bundesliga - RB Leipzig v Eintracht Frankfurt
Picha: Ronny Hartmann/REUTERS

Kocha Julian Nagelsmann alisikitishwa na matokeo hayo ijapokuwa wana fursa ya kuwawekea mbinyo Bayern watakapocheza dhidi ya Arminia Bielefeld Ijumaa. Mabingwa watetezi Bayern walipata ushindi wa 3 – 1 dhidi ya Werder Bremen Jumamosi na sasa wako kileleni na mwanya wa pointi sita dhidi ya Leipzig huku kukiwa na mechi tisa zilizobaki. Kocha wa Bayern Hansi Flick amekuwa akihusishwa na uvumi wa kumrithi Jogi Loew katika tetesi ambazo amepuuzilia mbali

"Nina mkataba hadi 2023, Na ninanuia kuendelea kwa mafanikio kufanya kazi na Bayern Munich, na kushinda mataji kadhaa. Na kazi yangu ipo hapa na klabu hii. Na bila shaka klabu inatarajia kuwa nijitolee kwa asilimia 100 kuihudumia FC Bayern Munich na timu. Na hii ni haki yao kabisa. Kwa hiyo nadhani sio wakati..au tetesi kuhusu mustakabali wangu havina maana.

Nambari sita Bayer Leverkusen huenda wangeenda nafasi ya nne na kuwawekea mbinyo Frankfurt lakini msimu wao wa kuyumbayumba uliondelea baada ya kufungwa 2 – 1 na vibonde Bielefeld ikiwa ni pigo kubwa katika kusaka tiketi ya Champions League.

Borussia Dortmund iliendeleza matokeo yake mazuri kwa kuibwaga Hertha Berlin 2 – 0 na kurejea katika mbio za kutafuta tiketi ya nne bora ikiwa katika nafasi ya tano kwenye ligi. Nambari tatu Wolfsburg iliupigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la washika mkia Schalke kwa kuwanyeshea kipigo cha 5 – 0. Shalke huenda wakashushwa daraja kwa mara ya kwanza katika miaka 30.

AFP, DPA, AP, Reuters