1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lewandowski apiga hat-trick

17 Januari 2022

Robert Lewandowski ameendelea kuwapa wakati mgumu mabeki katika Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga baada ya kufunga magoli matatu kwenye mechi ya Bayern Munich iliyopita walipocheza na FC Köln.

https://p.dw.com/p/45ePV
1. FC Köln v FC Bayern München - Bundesliga
Picha: Alexander Scheuber/Getty Images

Mechi hiyo ilichezwa katika uwanja wa Rhein Energie mjini Cologne. Bayern walishinda 4 bila na Corentin Tolisso ndiye aliyewafungia hilo goli lengine.

Kwa magoli hayo aliyoyapachika wavuni Lewandowski sasa amefikia jumla ya mabao 300 katika Bundesliga, magoli 65 nyuma ya rekodi iliyowekwa na gwiji wa Bayern Munich Gerd Müller.

Ni ushindi ambao ulimpa furaha tele kocha wa Bayern Julian Nagelsmann.

"Cologne ni wazuri na wamekuwa na msimu mzuri lakini nafikiri tuliudhibiti mchezo vyema. Tulikuwa na bahati kidogo na krosi mbili ambazo zingekuwa mabao ila Cologne kawaida hufunga katika kila mechi. Kuwafunga mabao 4 tena bila jawabu ni jambo zuri sana na tulikuwa na nafasi ya kufunga mabao mengi pia katika kipindi cha kwnaza. Mwisho wa siku lakini ni kitu kizuri kufunga mabao mengi kwenye ligi. Ulikuwa ushindi muhimu kwa kuwa Dortmund nao walishinda baada ya kucheza vizuri sana jana," alisema Nagelsmann.

Haaland miongoni mwa waliofunga

Dortmund wao walicheza mechi yao dhidi ya Freiburg siku ya Ijumaa ambapo walipata ushindi mnono wa magoli 5-1 na kilichowafurahisha mashabiki wa BVB ni kumuona mshambuliaji wao mahiri Erling Haalland akiwa miongoni mwa wafungaji tena.

Fußball Bundesliga Borussia Dortmund - SC Freiburg
Erling Haaland akifunga mojawapo ya magoli yake dhidi ya FreiburgPicha: imago images/Moritz Müller

Haaland alikuwa amekwenda mechi mbili bila kufunga katika Bundesliga. Alifunga mabao mawili na beki wa kulia Thomas Meunier naye akapata mawili, mabao aliyoyafunga kupitia kichwa. Kufunga kwa Meunier lakini ndilo jambo lililozungumziwa sana baada ya mechi hiyo. Huyu hapa Michael Zorc, mkurugenzi wa michezo wa Dortmund.

"Kutoka mwanzo wa mechi, tulicheza vizuri sana, tuliudhibiti mpira vyema ila kilichopendeza zaidi ilikuwa ni shinikizo tulilowawekea wapinzani kila tulipopoteza mpira, hapo tulicheza vizuri sana, hatukuwapa nafasi hata kidogo. Nafikiri katika kipindi cha kwanza Freiburg hawakuwa na nafasi yoyote na kikubwa zaidi nimefurahishwa sana na Thomas Meunier," alisema Zorc.

Timu nyengine iliyopata matokeo muhimu mno katika michezo ya mwishoni mwa wiki ni RB Leipzig ambayo iliibamiza VfB Stuttgart 2-0. Kwa mara nyengine tena Andre Silva na Christopher Nkunku ndio waliowafungia Leipzig.

Peter Gulacsi ndiye aliyekuwa nyota

Lakini kila mmoja alimsifu sana mlinda lango wa Leipzig Peter Gulacsi kwa kuwaweka mchezoni na hatimaye kuipelekea timu yake kunyakua pointi tatu muhimu ugenini. Domenico tedesco ni kocha wa Leipzig.

"Bila shaka Gulacsi alitufanya tusalie mchezoni. Tulikuwa tunaongoza moja bila na akaokoa mara kadhaa magoli ya wazi kwa hiyo tunastahili kumshukuru kwa kuweza kufunga bao la pili na kupata ushindi," alisema Tedesco.

RB Leipzig - Manchester City | Fußball Champions League
Mlinda lango wa Leipzig Peter GulacsiPicha: Annegret Hilse/Reuters

Kwa sasa Bayern Munich wanaongoza jedwali wakiwa na pointi 46 pointi sita mbele ya Borussia Dortmund walio katika nafasi ya pili kisha nafasi ya tatu ikiwa inashikiliwa na Bayer Leverkusen wenye pointi 32 baadaya kuwafunga Borussia Mönchengladbach 2-1 huko Borussia Park katika mechi ya dabi ya Mto Rhein. Wa nne ni TSG Hoffenheim ambao wamefungana kialama na Union Berlin, wote wakiwa na pointi 39 ila Hoffenheim wana idadi kubwa ya magoli na ndio sababu wako kwenye nafasi ya nne.

Chini ya msimamo VfB Stuttgart na Arminia Bielefeld wanafuatana katika nafasi ya 16 na 17 wote wakiwa na pointi 18 halafu mkia unavutwa na Greuther Fürth ambao walilazimishwa sare na Bielefeld katika mpambano wao wa jana.