1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya: Jumuiya ya kimataifa ipo njia panda

11 Machi 2011

Libya imeendelea kushuhudia mashambulizi ya vikosi vya Muammar Gaddafi dhidi ya waasi, huku Jumuiya ya Kimataifa ikiwa haijaamua nini hasa cha kufanya kuzuia umwagikaji damu kwenye taifa hilo lenye utajiri wa mafuta.

https://p.dw.com/p/10XPs
Waasi wa Libya
Waasi wa LibyaPicha: dapd

Vikosi vya Muammar Gaddafi vinapambana kuudhibiti mji wa bandari ya mafuta wa Ras Lanuf kutoka mikononi mwa waasi. Mji huu uko umbali wa maili 300 kutoka ngome kuu ya Gaddafi, na mapema vikosi hivyo viliripotiwa kuingia hapo vikitumia vifaru na mashua za kijeshi.

Waasi wanakisia kuwa, kwa uchache, wanajeshi 1,000 wa Gaddafi wamo mjini humo hivi sasa, ingawa wameapa kuendelea na mapambano. Hata hivyo, ni wazi kuwa waasi hawa wameelemewa kwa nguvu, vifaa na uwezo wa kuratibu mapigano.

Mashambulizi haya yanafuatia yale ya jana (10.11.2011), ambapo mabomu kutoka vikosi vya Gaddafi viliyalenga maeneo ya waasi katika Ras Lanuf na mji mwengine wenye mafuta wa Brega, ulio umbali wa maili 50 mashariki mwa mji mkuu wa Tripoli.

Tayari vifo vya watu wanne na majeruhi wapatao 40, vimethibitishwa kwa upande wa waasi.

Saif al-Islam aapa kushinda

Mtoto wa Muammar Gaddafi, Seif al-Islam Gaddafi
Mtoto wa Muammar Gaddafi, Seif al-Islam GaddafiPicha: ap

Tayari mtoto wa Gaddafi, Saif al-Islam, ambaye kwa siku za karibuni amejitokeza kama msemaji rasmi wa utawala wa baba yake, ameshaonya kuwa sasa jeshi litafanya mashambulizi makali dhidi ya waasi na kwamba hakutakuwa na kurudi nyuma, na kwamba si Jumuiya ya Kujihami ya NATO wala majeshi yoyote ya kigeni, yatakayowazuia kuzima uasi.

"Wale wanaojifanya kutegemea NATO, na meli za Kimarekani, tunawaambia kuwa si Marekani wala NATO atakayewasaidia na sisi tutashinda kwa idhini ya Mungu." Saif al-Islam aliwaambia wafuasi wa baba yake waliokusanyika jana mjini Tripoli.

Kauli hii ya Saif al-Islam inaonekana kufanana, kwa kiasi fulani, na hali halisi ilivyo kwenye uwanja wa mapambano na kwenye jumuiya ya kimataifa.

Ambapo kwenye uwanja wa mapambano, majeshi ya Gaddafi yanazidi kujiimarisha kwa mashambulizi ya angani, kwenye jumuiya ya kimataifa hakujakuwa, hadi sasa, na makubaliano ya hatua gani hasa ichukuliwe kunusuru umwagikaji damu mkubwa unaoendelea.

Jumuiya ya Kimataifa ipo njia panda

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine AshtonPicha: AP

Si Marekani wala nchi za Umoja wa Ulaya zenye sauti moja juu ya namna ya kuushughulikia mgogoro huu, ambao sasa unaanza kuchukua vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Hapo jana, Ufaransa iliutambua upinzani wa Libya wenye makao yake makuu Benghazi, mashariki ya Libya, kuwa wawakilishi halali wa watu wa Libya, lakini Italia ikasema hayo ni maamuzi binafsi ya Ufaransa na si ya Umoja wa Ulaya.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya na wale wa Ulinzi wa NATO wanaendelea kukutana katika vikao tafauti mjini Brussels, lakini vyenye lengo moja la kujadili hatua za kuichukulia Libya. Tayari kuna dalili za kutokufikiwa makubaliano juu ya suala la kuiwekea vikwazo vya anga nchi hiyo.

Katika hatua nyengine, Gaddafi ameendelea na jitihada zake za kutafuta uungwaji mkono wa kimataifa. Mjumbe wake, Umran Abu-Kra'a, yupo mjini Cairo kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, licha ya jumuiya hiyo kusitisha uwanachama wa Libya, ukipinga mashambulizi ya utawala wa Gaddafi dhidi ya wapinzani.

Gaddafi pia amewaachilia huru maafisa wawili wa jeshi la majini la Uholanzi waliokuwa wanashikiliwa nchini mwake. Imeripotiwa pia kuwa kiongozi huyo amekuwa akiwasiliana na serikali ya Malta, kuiomba nchi hiyo iwe msuluhishi wa mgogoro unaoendelea nchini mwake, ombi ambalo limekataliwa na serikali ya Malta.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE/Reuters
Mhariri: Othman Miraji